Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Michael Sallu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN M. SALLU K.n.y MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza:- Je, lini Serikali itazipandisha hadhi zahanati za Mkwajuni Chanika na Hedi Kwamagome kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga kituo cha afya kwenye Kata ya Mabanda ambapo ni Kata ya kimkakati kiafya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ndani ya Handeni DC kuna Tarafa tatu hazina kabisa vituo vya afya. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivyo vya afya kwenye Tarafa ya Mkumburu, Magamba na Kwamsisi?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, amefuatilia sana suala la Kituo cha Afya cha Kata ya Mabanda. Ninamhakikishia tu kwamba, kwa sababu alikwishawasilisha kwenye orodha ya vituo vya afya vya kimkakati, tayari imeshaingizwa kwenye orodha ya vituo vya afya vitakavyojengwa kila Jimbo na tutapeleka fedha kwenye Kata hii ya Mabanda kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Tarafa hizi tatu za Jimbo la Handeni Vijijini kwa Mheshimiwa Sallu, ni kweli hazina vituo vya afya, lakini tayari Serikali imeshaainisha kwenye Tarafa ya Kwamsisi zahanati ile itapandishwa hadhi na tayari ipo kwenye bajeti ya fedha za Benki ya Dunia, wakati wowote tunaamini kwamba fedha hizi zitapelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kata ya Mkumburu na Magamba, tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapeleka vituo vya afya, lakini Tarafa hii ya kumburu eneo la Segera na yenyewe imeingizwa kwenye mpango wa vituo vya afya kwa kila Jimbo. Ahsante sana.

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. JOHN M. SALLU K.n.y MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza:- Je, lini Serikali itazipandisha hadhi zahanati za Mkwajuni Chanika na Hedi Kwamagome kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 2

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Ni takribani miaka miwili sasa tangu Mheshimiwa Waziri alipokuja Vunta kuona Zahanati ya Vunta na ukaahidi kwamba kunajengwa Kituo cha Afya pale Vunta lakini mpaka sasa hivi sijaona hatua yoyote iliyochukuliwa ya kuanza Kituo cha Afya cha Vunta. Je, Mheshimiwa Waziri, anaweza kuwaambia nini wananchi wa Kata ya Vunta?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mama Anne Kilango Malecela kwa namna ambavyo amefuatilia sana ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ile ya Vunta. Ni kweli mwaka 2022 mimi na yeye tuliongozana, tukafanya ziara na mikutano ya hadhara pale. Namhakikishia Mbunge kwamba, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi yake makubwa kwa wananchi wa Same na Wananchi wa Vunta, tayari ameshatenga shilingi 623,000,000, zitaingia wakati wowote kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Vunta. Kwa hiyo nawahakikishia wananchi wa Vunta kwamba kazi itaanza hivi karibuni. Ahsante sana. (Makofi)