Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya kuunganisha Kongani ya Viwanda ya Kwala na Stesheni ya SGR ya Ruvu?

Supplementary Question 1

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; sasa, kwa kuwa Serikali iko kwenye mkakati wa kufanya uchambuzi wa kujua gharama, je, imefanya mawasiliano na mkandarasi wa ujenzi wa eneo hilo ili wasifunge barabara ili wananchi waweze kuendelea kulitumia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati wa ujenzi wa Reli ya SGR, limejengwa daraja pale kwenye Mto Ruvu ambalo limepitisha reli tu na hapakuzingatiwa eneo la kupita watu waendao kwa miguu na kwa magari. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja sasa la matumizi ya waendao kwa miguu na magari?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri kabisa haya kwa lengo la kuwasemea wapiga kura wake. Kuhusiana na swali lake la kwanza, ninaomba niendelee kumwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba tuendelee kuwafahamisha na wananchi kwamba kufungwa kwa barabara hii ambayo ipo kando ya reli yaani kwa maana ya SGR ni takwa la kisheria. Ni takwa la kisheria kwa tafsiri ya kuimarisha usalama wa wananchi, watumiaji wa reli lakini pia kulinda ile miundombinu ya reli. Kwa hiyo naomba tuendelee kuwaelimisha wananchi ili waweze kufahamu kwamba hili ni suala ambalo linahusu usalama wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, naomba niendelee kumueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua hoja uliyoisema na ni ya msingi. Kwa wakati huu Serikali itafanya jitihada kuhakikisha inaimarisha miundombinu katika eneo hili la Ruvu ambalo mwisho wa siku litakuja kufanyiwa ujenzi kwa maana ya tafsiri tayari SGR inapita katika eneo hili. Tutaimarisha na tutatengeneza mazingira mazuri ili kuweza kutengeneza njia ya wananchi kupita, lakini pia magari kupita na kutengeneza suluhisho la kudumu. Kwa hiyo, hoja yako Mheshimiwa Mbunge tumeipokea na tunaifanyia kazi. (Makofi)