Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hassan Zidadu Kungu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Primary Question
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:- Je, kwa nini Kiwanda cha Kubangua Korosho Wilayani Tunduru kimeshindwa kufanya kazi kwa miaka saba mfululizo?
Supplementary Question 1
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; moja ya sababu ya kubinafsishwa viwanda vile ama kiwanda kile ni kumpata Mwekezaji mwenye uwezo wa kukiendeleza kiwanda kile. Je, Serikali haioni kuwa mwekezaji yule amekosa sifa zilizomfanya kubinafsishiwa kiwanda kile na kushindwa kukiendeleza kiwanda hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kiwanda kile kilikuwa kinatoa ajira kwa akina mama ama wanawake zaidi ya 600 na vijana zaidi ya 200. Je, ni kwa nini Serikali isimlazimishe Mwekezaji kukirejesha kiwanda kile Serikalini ili kumtafuta Mwekezaji mwingine mwenye uwezo mkubwa wa kukiendeleza na hatimaye akinamama wale waendelee kupata ajira za muda mfupi?
Name
Hussein Mohamed Bashe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Answer
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zidadu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mimi mwenyewe nimetembelea kiwanda kile na nimefika kukiona na infrastructure iliyoko pale nimeiona kwa macho yangu. Ndiyo maana kwenye jibu la msingi tumesema kwamba tunaanza majadiliano na wenzetu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao walikasimiwa madaraka yaliyokuwa yanatekelezwa na PSRC ili tuweze kuona masharti ya ubinafsishaji ya viwanda vile yalikuwa namna gani. Tatizo hili la watu waliobinafsishiwa viwanda ambao at the same time ni exporter wa raw material, wengi walichukua viwanda vya korosho na wakavifunga, halafu wakawa ni wasafirishaji wa korosho ghafi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wote, tatizo hili tunalo kwenye korosho na kwenye chai. Watu wamechukua mashamba, wamechukua viwanda hawajamua kuendeleza toka walivyobinafsishiwa. Serikali tumeanza mchakato wa kuanza kuipitia mikataba ya ubinafsishaji na kuangalia kama wanakidhi masharti waliyopewa na Serikali wakati wanauziwa viwanda hivi na Serikali itachukua hatua.
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:- Je, kwa nini Kiwanda cha Kubangua Korosho Wilayani Tunduru kimeshindwa kufanya kazi kwa miaka saba mfululizo?
Supplementary Question 2
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Kama ilivyo katika kiwanda cha korosho ninajua katika jibu la msingi amezungumzia chai; Kiwanda cha Chai MO kilichopo Rungwe kimefunga na kuwaacha wafanyakazi ambao wengi hawajalipwa na chai inakaa hainunuliwi. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, atoe tamko leo tunafanyaje kwa sababu chai ni zao ambalo linaharibika sasa wanaanza kung’oa mazao ya chai na kupanda parachichi. Tunaomba msaada wa Waziri ili tuweze kujua.
Name
Hussein Mohamed Bashe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Answer
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema wakati najibu swali la Mheshimiwa Zidadu, changamoto ya aina hii tunayo kwenye korosho, changamoto ya aina hii tunayo kwenye chai. Kwenye chai kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba mwekezaji huyu amenunua mashamba na viwanda Rungwe na baadhi ya maeneo katika nchi yetu na vyote amevifunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nimhakikishie kwamba Wizara ya Kilimo tayari ilishamwandikia barua na ametujibu, lakini hatujakubaliana na majibu aliyotupatia. Wizara na Serikali tunaendelea kufuatilia kuhakikisha yeyote aliyeuziwa shamba, aliyeuziwa kiwanda ambacho hakiendelezi atupe sababu za kutotimiza wajibu wake wa kimkataba wakati anabinafsishiwa maeneo haya na Serikali itachukua hatua. Ni jambo litakalotuchukua muda, lakini niwahakikishie tu kwamba tumeanza ku-pursue huu mwelekeo na tutafika nao mwisho. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved