Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuleta Muswada wa Sheria utakaotoa adhabu ya Kifo kwa wabakaji wa watoto walio chini ya miaka tisa?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, sasa hivi ubakaji umeshika kasi sana na hasa katika Mkoa wetu wa Iringa, imetokea hata vijana kwa vijana wanabakana wenyewe kwa wenyewe ambao wapo chini ya umri wa miaka 18. Je, sheria inasemaje kwa watoto wanaobakana wao kwa wao shuleni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tatizo hili limekuwa kubwa sana hapa nchini na tumeona mpaka muuliza swali anasema kwamba wauawe, lakini naona je, kuna uwezekano labda wahasiwe, maana yake imekuwa ndiyo tatizo kubwa sana? (Kicheko)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, kufuatia kumomonyoka kwa maadili, baadhi ya matendo ambayo huko nyuma hatukuzoea kuyasikia Watanzania yameongezeka kwa kasi ikiwemo matukio ya ubakaji na sasa amesema kwa watoto pia shuleni yanafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kosa hata kama limefanywa na mtoto ni kosa, lakini kwa maana ya sheria zetu mtoto atahukumiwa chini ya Sheria ya Watoto na hivyo ikitokea mmoja kamfanyia vitendo visivyo vya maadili kama hilo, taarifa zikipelekwa kwenye vyombo vya dola na ikapelekwa Mahakamani, mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja kama ni kifungo atafungwa kwenye Mahakama ya watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la pili, Mheshimiwa naona analiongea kwa hisia, ni kweli kwamba jambo hili linaudhi lakini sasa hicho anachokisema hakipo kwenye sheria zetu, kama tutafika hatua hiyo ni pale ambapo Bunge lako litakuwa limerekebisha sheria na kuruhusu hicho anachokisema Mheshimiwa Mbunge. Nashukuru. (Makofi)