Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hassan Zidadu Kungu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Primary Question
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: Je, kuna upungufu kiasi gani wa walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na upi mpango wa kuondoa upungufu huo?
Supplementary Question 1
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba katika hao walimu 12,000 watakaoajiriwa watapewa kipaumbele maeneo ya pembezoni kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambako walimu wengi wanahama sana kuliko kuhamia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inaendelea kuajiri walimu kila mwaka, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza motisha na kuboresha mazingira ya maeneo ya pembezoni ili kuvutia walimu na kubaki katika maeneo ya pembezoni na kupunguza walimu kuhama? Ahsante.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la msingi kabisa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi za walimu 12,000, walimu hawa wanatarajiwa kuajiriwa kwa kuzingatia idadi yao, lakini pia kuzingatia uwiano na uhaitaji. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwa sababu Serikali mpango wake ni kuhakikisha kila eneo, mkoa, jimbo na kila shule yenye uhitaji inapata mgao, basi nikuhakikishie na wewe Mheshimiwa Mbunge katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru shule zako zenye uhitaji na zenyewe zitapata walimu hao.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana kuhakikisha inaboresha mazingira ya kufundishia katika maeneo ya vijijini. Kupitia miradi ya BOOST, SEQUIP, GPE, TSP na EP4R, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana ya kujenga nyumba za walimu ili kuboresha mazingira hayo ya kufanyia kazi, lakini pia imekuwa ikihakikisha huduma zinapatikana kwa mfano umeme unapatikana kupitia REA (Umeme wa Vijijini); huduma za maji kupitia RUWASA na imekuwa ikihakikisha barabara za TARURA na zenyewe zinajengwa, lakini huduma za msingi kama afya zinapatikana kwenye maeneo ya vijijini. Yote hiyo ni kutengeneza mazingira mazuri ili walimu wanaopangwa kufundisha katika maeneo ya vijijini waweze kufanya kazi katika mazingira bora zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuendelea kuzisisitiza halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinafanya msawazo wa walimu ili wale walimu wanaokuwa wamejazana katika shule za mijini waweze kusawazishwa na kuweza kuhamishwa kwenye maeneo ya shule zilizopo vijijini ambazo mara nyingi zinakuwa na upungufu mkubwa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved