Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:- Miradi ya umeme ya REA Awamu ya Kwanza na ya Pili inaendelea vizuri. Je, ni lini miradi ambayo haijakamilika itakamilika hasa ikizingatiwa kuwa Serikali iliahidi kukamilika kwa miradi hiyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2015?

Supplementary Question 1

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ahadi ya Serikali na Waziri mwenyewe humu Bungeni aliwaahidi Watanzania kwamba Miradi ya REA II itakamilika yote Juni, 2015; siyo mara moja wala mara mbili; ni sababu ipi iliyopelekea miradi hii kutokukamilika kama Mheshimiwa Waziri alivyosema? (Makofi)
La pili, kwa sababu huyu Mkandarasi mara kwa mara amekuwa akiwachangisha Watanzania shilingi 200,000/= au shilingi 300,000/= kwa kila nguzo ya umeme wale wanaohitaji; Serikali inatoa tamko gani ili kusudi wananchi hao wapate huduma hii kama ilivyotarajiwa? (Makofi)

Name

Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Answer

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tulikusudia kwamba ikifika Juni, 2015 miradi iwe imekamilika, lakini tuwe na ukweli wa kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pato letu la Taifa ni karibu dola bilioni 53 na mwaka jana tulikuwa na uchaguzi, tulikuwa na Katiba, uchumi wetu hauna uzito wa kukabili vitu vikubwa kwa wakati mmoja. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni ukweli wa kifedha na kiuchumi. Kwa hiyo, ndiyo maana sasa Serikali imemaliza majukumu makubwa fedha zinaenda REA, kwa hiyo, miradi itakamilika kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuongezea kwamba miradi ya REA na Miradi yote ya umeme, ndugu zangu Watanzania inahitaji fedha nyingine za kutoka nje. Kwa hiyo, sisi Wizara tumeanza kutafuta fedha kutoka nje. Kwa mfano, Tanzania ndiyo iliwakilisha Afrika kuweka hizi taratibu za umeme kwa kila raia wa sayari hii (Sustainable Energy for All 2030). Ni sisi ndiyo tuliwakilisha Bara la Afrika na tutahakikisha sisi ndiyo tutapata fedha nyingi kutoka huko na tumeishaanza kuzipokea. Kwa hiyo, miradi itaenda kwa kasi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Chico, tumewaambia Wakandarasi kwamba endapo pataonekana kuna rushwa, adhabu kubwa kabisa ni kwamba huyo mkandarasi hatapata miradi mingine ya REA. Kwa hiyo, kama huyu mkandarasi anachangisha, ni kwamba na wiki ijayo tunafanya tathmini adhabu yake nyepesi sana ni kutopata mradi wowote wa REA kuanzia mwaka huu.

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:- Miradi ya umeme ya REA Awamu ya Kwanza na ya Pili inaendelea vizuri. Je, ni lini miradi ambayo haijakamilika itakamilika hasa ikizingatiwa kuwa Serikali iliahidi kukamilika kwa miradi hiyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2015?

Supplementary Question 2

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa huu Mradi wa REA umesambazwa sana vijijini na nguzo zimewekwa sana vijijini, lakini nguzo hizi zimeanza kuoza. Je, ni lini Serikali itahakikisha nguzo hizi zinawekwa na wananchi wa vijijini wanapata umeme? Ahsante sana.

Name

Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Answer

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza labda iwe ni miujiza, hizi nguzo kuharibika siyo chini ya miaka kumi. Kwa hiyo, kuoza kisayansi hatukubaliani na hilo, la kwanza hilo. (Makofi)
La pili, Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba jumla Tanzania tuna vijiji 15,029. Vijiji ambavyo vimepata umeme hadi sasa ni 5,900, sawa na asilimia 33. Kwa hiyo, tukiingia REA Awamu ya Tatu, ya Nne na ya Tano, nadhani Tanzania itakuwa katika nchi pekee Barani Afrika kwamba umeme umetapakaa vijijini kote.
Mheshimiwa Mbunge, ndiyo maana ni wiki moja kutoka sasa tunafanya tathimini ya REA Awamu ya Pili, ili tuingie REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, nguzo haziozi na hazitaoza, umeme utapatikana. Ahsante.