Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Pius Stephen Chaya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Nkonko ambacho nacho kilipewa fedha na Serikali kwa ajili ya kujenga jengo la kuhifadhia maiti (mortuary), mpaka sasa hivi hakitumiki kwa sababu hakuna jokofu. Je, ni lini Serikali itapeleka jokofu kwa ajili ya kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya cha Nkonko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Makanda ambayo ipo zaidi ya kilometa 25 haina kituo cha afya, lakini inahudumia kata jirani za Makutupora, Makulu, Makanda B, Bahi na vilevile Kata ya Mpendwa na ni mojawapo ya kata ambayo tuliiweka kwenye kata za kujengewa vituo vya afya vya kimkakati. Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Makanda kama kituo cha afya cha kimkakati? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika kipindi cha mwaka huu wa fedha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa zaidi ya shilingi bilioni 250 katika halmashauri zote 184 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni kuweka kipaumbele cha kununua jokofu, kwa ajili ya hicho kituo cha afya ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, Serikali tayari imeshatoa taarifa na maamuzi ambayo kupitia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, majimbo yote 214 ya Tanzania Bara yatajengewa vituo vya afya na tayari tuko hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ajili ya kujenga vituo hivyo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo hicho cha Makanda ni miongoni mwa vituo ambavyo vipo kwenye orodha hiyo na amefuatilia mara kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wawe na uhakika na hilo, lakini kuna majimbo 18 ambayo mpaka sasa hatujapata mapendekezo ya kata ambazo wanahitaji kujenga vituo vya afya. Kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge ambao hawakuleta taarifa ya kata ambazo wanapendekeza, watuletee ili tukianza kutoa fedha kata hizo ziwe sehemu ya mradi huo, ahsante. (Makofi)
Name
Zuberi Mohamedi Kuchauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 2
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, Kituo cha Afya cha Mpengele kwenye Kata ya Mkata, ni miongoni mwa vituo vya afya vya mwanzo kabisa, lakini hakina jengo la OPD mpaka leo. Je, Serikali iko tayari kutuletea fedha kwa ajili ya kujenga jengo la OPD?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Kituo hicho cha Afya cha Mpengele katika Kata hiyo ya Makata, Jimbo la Liwale, Mheshimiwa Kuchauka amefuatilia mara kadhaa na kwa bahati njema Serikali tulishaainisha vituo vya afya vyote vyenye majengo pungufu. Baada ya ukamilishaji wa vituo vya afya vya kimkakati tunakwenda kuanza na awamu ya pili ya kukamilisha majengo katika vituo vyenye majengo pungufu na vituo vya afya ambavyo ni chakavu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tutalipa kipaumbele, ahsante.
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itajenga jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mafiga?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasikia kituo cha afya?
MWENYEKITI: Rudia swali.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itajenga jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mafiga? Mheshimiwa Waziri, hili swali nimeuliza mara nyingi na tumeongea wote pamoja.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma amefuatilia na ameuliza mara kadhaa kuhusiana na jengo hilo katika Kituo cha Afya cha Mafiga katika Manispaa ya Morogoro. Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali sikivu imeshaweka mpango kwa ajili ya kwenda kujenga jengo hilo katika kituo hiko cha afya, ahsante.
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itakarabati Kituo cha Afya cha Mwika? Nimeuliza swali hili toka nije hapa Bungeni, ile Novemba mpaka leo nauliza tu, lakini hamna mtu anayejibu wala hakuna kichachofanyika.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei nilishakaa naye mara kadhaa na tulishakubaliana kwamba Kituo cha Afya cha Mwika kiko kwenye mpango wa Vituo vya Afya vya Benki ya Dunia na nilimuonesha kwamba kipo kwenye orodha hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba ni suala la taratibu tu za kifedha na kituo kile tayari kitajengwa kupitia Mfuko wa Benki ya Dunia, ahsante.
Name
Deo Kasenyenda Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 5
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali upande wa afya, Kata ya Mlowa, Kijiji cha Mkolango, wananchi wamejenga zahanati kwa nguvu zao, Diwani pamoja na mimi Mbunge. Ni lini Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi katika zahanati hiyo ya Mkolango?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wote wa Mkoa wa Njombe, lakini pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kwa Mkoa wa Njombe na Mbunge wa Jimbo la Makambako, amefutilia mara nyingi sana kuhusiana na Zahanati ya Mkolango na mimi nimeshamhakikishia kwamba tumeshaingiza kwenye mpango wa zahanati ambazo zitapelekewa shilingi milioni 50. Nimhakikishie tu kwamba mpango huo bado upo palepale na tutahakikisha kwamba tunautekeleza, ahsante.
Name
Twaha Ally Mpembenwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 6
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Kata ya Mtunda ni moja katika kata za mkakati katika Jimbo la Kibiti ukizingatia kwamba kata hii ni moja ya kata ambazo zilikuwa zimekumbwa na mafuriko katika kipindi kilichopita, je, nini kauli ya Serikali katika kuweza kujenga kituo cha afya kwa wananchi wale ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu sana?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kata zote za kimkakati ambazo halmashauri zilikubaliana na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeziwekea mpango wa utekelezaji wa aina mbili; mpango wa kwanza ni kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, lakini mpango wa pili ni kupitia fedha za Serikali Kuu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mpembenwe kwamba amefuatilia mara kadhaa kuhusiana na kituo hicho cha afya na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeweka kipaumbele kuhakikisha kwamba wananchi wa kata hiyo wanapata kituo cha afya ili waweze kupata huduma bora za afya, ahsante.
Name
Esther Lukago Midimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga OPD na wodi za wagonjwa katika Kituo cha Afya Kintinku?
Supplementary Question 7
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaipandisha hadhi Zahanati ya Buchambi, Wilaya ya Maswa, kwa vile inahudumia watu wengi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishaji wa hadhi wa zahanati kuwa kituo cha afya upo kwa mujibu wa utaratibu ambao halmashauri kwanza baada ya kufanya tathmini ya idadi ya wananchi walioko katika eneo hilo, ukubwa wa usiopungua ekari 15, lakini pia na umbali kutoka kituo cha jirani zaidi cha afya wanaweza kuwasilisha maombi ya kupandisha hadhi kituo hicho ili Serikali ianze kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga, kupanua na pia kuanza kutoa huduma ngazi ya kituo cha afya, ahsante.