Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege uliopo Wilaya ya Kahama ili uwe na hadhi ya kutua ndege kubwa?

Supplementary Question 1

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Kahama imekuwa ndiyo kitovu cha kibiashara kwa Mkoa wa Shinyanga, lakini pia na Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nchi hizi za Maziwa Makuu. Kwa nini Serikali isitenge japo fedha kidogo ili kuukarabati uwanja huu ambao ni wa kiwango cha moramu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Manispaa ya Kahama imekuwa ikikusanya fedha nyingi zaidi ya shilingi bilioni 13 mpaka shilingi bilioni 15 kwa mwaka. Kwa nini Serikali isitoe kibali sasa kwa Manispaa hii ya Kahama angalau uwanja huu uwekwe kwa kiwango cha lami pamoja na miundombinu yetu ili kuondoa adha wanayoipata wasafirishaji?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Cherehani kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa Uwanja wa Ndege wa Kahama lakini hata ule wa Shinyanga. Pili, napenda kumwarifu Mheshimiwa Cherehani pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba katika kipindi ambacho Serikali imewahi kutenga fedha nyingi kuliko wakati mwingine wowote, ni sasa. Hivi ninavyozungumza, takribani Shilingi trilioni moja zinajenga viwanja vya ndege karibu vyote kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, moja, tumepokea ushauri wake mzuri kwa ajili ya kuweka moramu ili uwanja huu uendelee kutumika zaidi na ikizingatiwa ni jengo la ubia ambalo limejengwa na wenzetu wa Madini. Pili, namwomba pia awe na subira kidogo, tutakapokamilisha Uwanja wa Ndege wa Shinyanga, tutapima mahitaji makubwa yaliyopo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kahama halafu tuone ni hatua ipi ambayo inahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, izingatiwe kwamba, tunapozungumza hapa hata maeneo mengine kwenye viwanja vya mikoa, kuna mahitaji makubwa ya fidia pamoja na viwanja hivyo vifanyiwe maboresho. Kwa hiyo, watupe muda kidogo, baada ya hapo tutaona cha kufanya kama Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nampongeza kwa sababu amekuja na mawazo ya kimapinduzi. Anazungumza juu ya Halmashauri ya Kahama kwamba ni halmashauri kubwa ambayo inakusanya mabilioni ya pesa na anaomba kibali kwamba pengine waruhusiwe kufanya ukarabati. Kimsingi Serikali hii ya Awamu ya Sita inaunga mkono jitihada za halmashauri na Waheshimiwa Madiwani wa aina yake katika kuiunga mkono Serikali kusaidia maboresho mbalimbali ya viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu chini ya Mheshimiwa Waziri Mbarawa pamoja na Mamlaka yetu ya Viwanja vya Ndege haitakuwa kikwazo, bali itakuwa msaada katika kurahisisha azma yenu hiyo kutokana na umuhimu mkubwa ambao mmeuona endapo mtatenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho.

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege uliopo Wilaya ya Kahama ili uwe na hadhi ya kutua ndege kubwa?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ni mkoa wenye historia katika nchi hii, kwani anatoka Muasisi wa Taifa letu Baba Julius Kambarage Nyerere. Tumeona mkiwa mnamuenzi kwa matembezi na kwa vitu mbalimbali. Sisi watu wa Mkoa wa Mara, moja ya kumuenzi Baba wa Taifa ni kuhakikisha mnakamilisha Uwanja wa Ndege wa Musoma kwa kiwango cha lami. Ni lini mtatenga fedha za kutosha kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Musoma unakamilika? Wabunge tumechoka kushukia Mwanza.

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Ester Bulaya kwa swali lake ambalo ameuliza kwa umakini mkubwa. Serikali hii ya Awamu ya Sita inatambua, inazingatia na inafahamu umuhimu wa Baba wa Taifa. Pia inatumbua umuhimu wa viwanja vya ndege nchi hii, ndiyo maana pamoja na viwanja vyote nilivyosema vinaendelea kujengwa na kukarabatiwa, Uwanja wa Ndege wa Musoma upo, umeshatengewa fedha na unajengwa. Hivi ninavyozungumza, upo 60%. Labda ninachoweza kumhakikishia, ni kuiagiza mamlaka inayosimamia iharakishe ujenzi huo ukamilike ili uweze kuanza kutumika.