Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y MHE. TUNZA I. MALAPO) aliuliza:- Dhana ya elimu ni majumuisho ya mambo mengi sana ikiwemo matibabu ya huduma ya kwanza, gharama za umeme, maji, vyakula (kwa shule za bweni), posho za walimu (part time) pamoja na zana za kufundishia zisizohifadhika kwa muda mrefu; na nyingi kati ya gharama hizo zilikuwa zinatatuliwa mashuleni na Wakuu wa Shule kwa kutumia ada na michango waliyokuwa wanatoza wanafunzi. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha ufanikishwaji wa dhana hii ya elimu bure bila kuanzisha migogoro mipya kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kuhusu uboreshaji wa elimu lazima tuzingatie mafunzo kazini kwa walimu. Sasa nataka niulize, Wizara ina mpango gani wa kufufua Vituo vya Walimu ambavyo vilianzishwa huko nyuma chini ya Mpango wa Kuboresha Elimu Ngazi ya Wilaya (District Based Support to Education(DBSPE) ambavyo kwa sasa hivi havitumiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili morale kwa Walimu ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba, dhana hii ya elimu bure inafanikiwa. Kwa hiyo, sasa nataka kujua kwamba, Serikali ina mpango gani kuhakikisha madeni kwa Walimu hayajirudii pamoja na kwamba, tupo kwenye sera ya kubana matumizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu ya maswali haya ya nyongeza.
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunazo Teachers Resource Centers ambazo ni kweli zimekuwa zikisaidia sana katika harakati za kuanza kuwajengea Walimu taaluma ya kutosha katika kuhakikisha kwamba, wanafundisha masomo yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Chikota, kwamba Serikali katika mpango wake mpana wa sasa hivi; licha ya kufanya ukarabati wa maeneo mbalimbali katika shule kongwe pia itahakikisha kwamba vile vituo vinakuwa centers nzuri kama ilivyokula pale awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba, vituo vile vinasaidia kuweka mbinu bora. Kwenye hii Sera mpya ya Elimu tutaweka mbinu bora kwa Walimu. Kwa hiyo, vituo vile vitaendelea kutumika vizuri zaidi, lakini vile vile TAMISEMI na Wizara ya Elimu tuna mpango mpana katika kuhakikisha kwamba, wanafundisha vijana wetu katika mazingira mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la morale kwa wafanyakazi hasa Walimu, suala la malimbikizo ya madeni, ni kweli na tumesema hapa, hata Waziri wa Elimu siku ile alipokuwa anahitimisha hoja yake alizungumzia jinsi gani madeni yaliyokuwepo mwanzo na madeni yaliyolipwa na madeni gani ambayo yako sasa yanahakikiwa ili waweze kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nikiri wazi kwamba, madeni ya Walimu hayawezi kwisha kwa sababu kila siku ya Mungu lazima kuna Walimu wanakwenda likizo na lazima kuna Walimu ambao wakati mwingine wanahama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la dhana ya kulipa madeni mpaka ibaki sifuri kabisa, jambo hilo litakuwa gumu kwa sababu kila siku lazima kutakuwa na watu wanaendelea kudai. Jambo la msingi ni kwamba, ni lazima madai yanapojitokeza tulipe. Tukiri wazi kwamba Serikali ilijitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuhakikisha Walimu hawa wanalipwa madeni yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, si kulipa madeni tu, hali kadhalika sasa hivi tunapambana katika kuboresha mazingira ya Walimu wanaofanyia kazi hususani ujenzi wa nyumba ili Walimu hawa wajisikie wako katika mazingira rafiki ya kufanya kazi.
Name
Dr. Faustine Engelbert Ndugulile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y MHE. TUNZA I. MALAPO) aliuliza:- Dhana ya elimu ni majumuisho ya mambo mengi sana ikiwemo matibabu ya huduma ya kwanza, gharama za umeme, maji, vyakula (kwa shule za bweni), posho za walimu (part time) pamoja na zana za kufundishia zisizohifadhika kwa muda mrefu; na nyingi kati ya gharama hizo zilikuwa zinatatuliwa mashuleni na Wakuu wa Shule kwa kutumia ada na michango waliyokuwa wanatoza wanafunzi. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha ufanikishwaji wa dhana hii ya elimu bure bila kuanzisha migogoro mipya kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na suala la elimu bure na changamoto ambazo zinakabiliana na suala hili, katika Wilaya ya Kigamboni, Wilaya ya Temeke na naamini katika Wilaya nyingi Tanzania, kuna changamoto kubwa sana ya Walimu hususani upande wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu hawa walikuwa wanagharamiwa kwa michango ambayo ilikuwa inakusanywa pale shuleni ambayo ilikuwa inalipia hawa Walimu wa part time. Serikali imesema imetoa mwongozo wa jinsi ya kusimamia suala hili, je, Serikali itakuwa tayari sasa kutoa maelezo ya mwongozo huo kwa Waheshimiwa Wabunge ili na sisi twende kuwasimamia zoezi hili kwa ukamilifu?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba, dhana ya elimu bure imekumbana na changamoto nyingi, lakini changamoto hizi ni changamoto za mafanikio. Kwa sababu kama mwanzo kulikuwa na suala la ulipiaji wa Walimu, vijana waliokwenda sekondari wanashindwa kwenda kusoma kwa sababu ya ada au michango mbalimbali. Nimeshuhudia sehemu mbalimbali zilizopita miongoni mwa vijana hao wengine walikuwa madereva wa bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii na Wabunge ni mashahidi; naamini Wabunge wengi walishakopwa na kuombwa sana na wananchi wao kuwalipia watoto ambao matokeo yao hawakuweza kuyapata kwa sababu ya ada ya mitihani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baada ya kuyachukua madeni na katika mpango wake mkakati, hasa kama ulivyojielekeza kwa Walimu wa sayansi, ni kwamba mwaka huu katika suala zima la ajira; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ile ilivyozungumza, kwamba katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2015/2016 kulikuwa na tengeo kwa ajili ya Walimu ambao tulikuwa tunatakiwa tuwaajiri na kipaumbele kikiwa ni kuwaajiri Walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukaenda mbali zaidi, kwa upande wa Walimu wa sayansi kuna wengine ambao wako nje ya system, lakini wana uwezo Serikali itaangalia kwa ukaribu zaidi namna ya kufanya ili Walimu wale waweze kutumika pamoja na wale ambao wamestaafu lakini wana uwezo wa kufundisha masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunaweza kuangalia vilevile vijana wetu waliosoma Bachelor of Science in Chemistry, Bachelor of Science in Physics, Statistics, au Bachelor of Science in Mathematics. Watu hawa hawaitwi walimu, ni watu waliosomea fani nyingine lakini akienda shuleni anaweza kufundisha. Ndiyo maana tumesema kwamba watu hawa tutawabainisha vilevile. Vijana hawa wengine wametembea mpaka soli za viatu zote zimekatika, hawaitwi Walimu lakini ni wataalam wazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda katika mpango wetu mpana kabisa wa kuhakikisha jinsi tutakavyowaingiza vijana hawa katika utaratibu mzuri angalau wapewe hata short course ya teaching skills ili tuongeze idadi ya Walimu wa Sayansi na kuondoa tatizo hilo, kwa sababu tumejenga maabara nyingi hivyo lazima tupate Wataalam ambao watafundisha maeneo hayo. Nadhani hayo ndiyo maeneo ya kuweka msisitizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeipeleka katika Halmashauri zote miongozo yote ya Sera ya Elimu, kwamba kila eneo ada kiasi gani, gharama za ukarabati kiasi gani. Miongozo hii tumepeleka katika Halmashauri zote ili watu wapate ufahamu ile pesa inayopelekwa inaenda katika kipengele gani kwa sababu kila kipengele kimewekwa asilimia yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y MHE. TUNZA I. MALAPO) aliuliza:- Dhana ya elimu ni majumuisho ya mambo mengi sana ikiwemo matibabu ya huduma ya kwanza, gharama za umeme, maji, vyakula (kwa shule za bweni), posho za walimu (part time) pamoja na zana za kufundishia zisizohifadhika kwa muda mrefu; na nyingi kati ya gharama hizo zilikuwa zinatatuliwa mashuleni na Wakuu wa Shule kwa kutumia ada na michango waliyokuwa wanatoza wanafunzi. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha ufanikishwaji wa dhana hii ya elimu bure bila kuanzisha migogoro mipya kati ya wakuu wa shule, walimu, wazazi pamoja na wanafunzi?
Supplementary Question 3
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ningependa kuuliza swali dogo tu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa hapo nyuma, shule nyingi zilikuwa zinategemea sana michango ya wazazi ili iwasaidie katika kuweza kutoa mafunzo hasa katika zile fani ambazo hazikuwa na Walimu wa kutosha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fungu maalum kwa ajili ya wale Walimu ambao watakuwa wanatoa mafunzo hasa ya masaa ya ziada baada ya ule muda wa kazi kukamilika?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba tutafanyaje katika kuongeza fungu maalum kwa ajili ya Walimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunaanza, maana tumepata mahali pa kuanzia. Kama nilivyosema kwamba mgawanyiko wa fedha unapelekwa katika jinsi gani kugharamia elimu hii na naamini kama nilivyosema kwamba kila jambo lina changamoto yake. Jambo hili limekuwa na mafanikio makubwa sana na ndiyo maana kwa kadri tunavyoenda tunafanya tathmini vile vile ili kuangalia na changamoto zilizojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi tutaangalia jinsi gani tutafanya, lakini lengo kubwa ni kuweza kuwaajiri Walimu ili waweze kutatua tatizo la upungufu wa Walimu hasa Walimu wa sayansi katika maeneo yetu.