Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuanza kutoa ruzuku vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro kutoka kwenye mapato ya mlima?
Supplementary Question 1
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, niombe watekeleze ambayo wamekuwa wakiahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiuliza Serikali, kama ambavyo kwenye mashirika na taasisi nyingine wamekuwa wakilipa CSR, je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kubadilisha sheria na kanuni ili wananchi wanaozunguka Mlima Kilimanjaro waweze kupata CSR kama yalivyo maeneo mengine ya migodi na kwingineko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tayari tumeshaunda vikundi mbalimbali katika Jimbo la Hai kwa ajili ya kusaidia vijana wetu wanaopandisha wageni kwenye Mlima Kilimanjaro, lakini kumekuwa na tatizo, zile kampuni za watalii nyingi zinakuja na vijana wao kutoka maeneo mengine.
Je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kuzielekeza kampuni hizi zichukue vijana waliopo pale Machame Gate na mageti mengine yaliyopo Mkoa wa Kilimanjaro ili vijana wanufaike na mlima wao? (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya kijamii imekuwa ikifanya vizuri isipokuwa tu baada ya tatizo la Covid ambalo mapato ya hifadhi zetu yalishuka ndipo miradi hii ilianza kupata changamoto. Baada ya mafanikio makubwa ya kudhibiti ugonjwa huu na kazi kubwa ya kutangaza vivutio vyetu vya utalii, tumeona mapato yameendelea kukua siku hadi siku na tumeweka mfumo mahsusi kwa sasa unaotuelekeza kwenye kutekeleza miradi hii ya kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge katika bajeti ya mwaka huu tumetenga takribani shilingi 3,000,000,000 kwa ajili ya miradi hii ya kijamii. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge mtupe muda tuendelee na utaratibu huu wakati tunafanya tathmini ya mwenendo wa ukuaji wa sekta ya utalii ili tukiona imetengemaa basi tunaweza kuja na huo mpango ambao utapendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la ajira; suala la ajira kisheria ni fursa kwa Watanzania wote kuweza kufanya kazi mahali popote katika nchi yetu mradi hawavunji sheria. Sasa nimesikia changamoto hii ambayo Mheshimiwaa Mbunge ameisema, lakini tukumbuke vilevile kwamba ajira hizi zinatolewa na sekta binafsi na wao katika kutoa ajira hizi vipo vigezo, sifa ambazo wanaziangalia na kubwa zaidi kwao ni uaminifu kwa hawa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Hai kuona uwezo wa vijana wale, kama kuna mapungufu tupo tayari kushirikiana nao kuwajengea uwezo, lakini vilevile kuwahamasisha katika suala zima la uaminifu, ili tuhakikishe kwamba vijana hawa nao wanapata fursa ya kuajiriwa katika eneo lile na kuweza kunufaika na rasilimali iliyopo kwenye eneo lao. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved