Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Edwin Maleko
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:- Je, kuna mkakati gani wa kuwaongezea bajeti TANAPA na TAWA kwani majukumu yao ni makubwa ikilinganishwa na bajeti inayotengwa?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa sasa, sekta ya utalii imekua sana hasa baada ya Mheshimiwa Rais Kutangaza utalii wetu na kutengeneza Filamu ya Royal Tour, je, Serikali haioni umuhimu wa kurejesha utaratibu wa zamani ili fedha hizo ziende kusaidia kwenye miundombinu pamoja na huduma nyingine zinazotolewa? (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kazi kubwa imefanyika ya kutangaza sekta ya utalii. Hapa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amechukua jukumu hili yeye mwenyewe na kushiriki kwenye filamu ile ya Royal Tour ambayo imekuwa na matokeo mazuri sana kwa nchi yetu. Vilevile, ameshiriki kwenye filamu ya Amazing Tanzania ambayo kesho tunaenda kufanya uzinduzi wake kwa upande wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeona ukuaji wa kasi wa sekta hii na imekuwa ikifanya tathmini ya kina kuhusu mwenendo wa ukuaji wa sekta hii na mahitaji yake. Ndiyo maana nilipojibu swali la msingi nimeonesha kwenye ule upande wa OC jinsi ambavyo Serikali imeongeza fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka katika bajeti ya mwaka huu tuliidhinisha hapa, asilimia sita kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Sekta ya Utalii. Vilevile asilimia tatu kwenye eneo la sekta ya wanyamapori. Hizi ni fedha ambazo mwanzoni zilikuwa hazitolewi, lakini ni fedha ambazo sasa zinatoka ili kuimarisha sekta yetu kama nilivyosema kwenye upande wa OC na kwenye upande wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ongezeko kubwa la karibu dola bilioni tano kwa TANAPA dola karibu bilioni nne kwa ajili ya TAWA. Kwa hiyo, tathmini hii inayofanyika ya ukuaji wa sekta, ninaamini kabisa kwamba, tutaweza kukidhi mahitaji ya sekta hii na kuweza kuhakikisha kwamba, fedha zinatoka kwa kutosheleza ili tuweze kuiboresha sekta yetu ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia sana kwenye pato la Taifa na ajira katika nchi yetu.
Name
Josephat Sinkamba Kandege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Primary Question
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:- Je, kuna mkakati gani wa kuwaongezea bajeti TANAPA na TAWA kwani majukumu yao ni makubwa ikilinganishwa na bajeti inayotengwa?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba utalii unatuongezea fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa sana. Pia, upatikanaji wa OC kila mtu anajua jinsi ambavyo inapatikana kwa kusuasua. Je, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba kunakuwepo na utaratibu wa kuwepo retention kwa ajili ya taasisi hizi ili yale matengenezo yanayotakiwa kufanywa kwa muda, yafanywe kwa wakati?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama nilivyosema kwenye majibu ya awali, retention imeanza ndiyo maana nimesema tuna asilimia sita inayokwenda kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Utalii; pia, tunayo asilimia tatu ambayo inaenda kwenye World Life Protection Fund.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi ambavyo tathmini zinafanyika kuhusiana na ukuaji wa sekta hii, tathmini hiyo itatuelekeza juu ya umuhimu wa kuwa na 100% retention au twende hatua kwa hatua ili tusiweze ku-suffocate maeneo mengine ambayo fedha hizi za utalii zinaweza kuchangia.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved