Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Michael Mwita Kembaki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Primary Question

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, upi mpango wa kuondoa tatizo la ucheleweshaji wa Vibali kwa Wachimbaji Wadogo na kutozwa mapato kwenye mchanga Mgodi wa Kebaga?

Supplementary Question 1

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze Serikali kwa majibu mazuri na namna ambavyo wameweza kutatua changamoto za wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Kebaga. Pamoja na majibu hayo mazuri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kumekuwepo na Mgodi wa Barrick ambao unafanya utafiti katika Kata za Ketare, Turwa pamoja na Kenyamanyori, lakini wamekuwa wakiwapa wenyeji wenye maeneo shilingi 20,000. Je, nini mwongozo wa Serikali kuhusiana na malipo hayo madogo yanayofanywa na Mgodi wa Barrick? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; upo wasiwasi mkubwa ambao wanao wale wachimbaji wadogo katika eneo la Tarime Mjini kutokana na ujio wa Barrick katika maeneo yao. Je, Serikali inawahakikishia nini hawa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kwamba wanakuwa salama wasiingiliwe au wasipate hasara kutokana na ujio wa Barrick? (Makofi)

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kembaki kwa jinsi anavyowatetea wananchi wake wa Jimbo la Tarime Mjini. Pia, nitumie nafasi hii kumjulisha kwamba Barrick wanapofanya utafiti katika maeneo yao ya leseni na tafiti zile zinapopita katika maeneo yenye mazao au bidhaa za wananchi katika yale maeneo ambayo bado wananchi wanaishi huwa wanapita wakiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ambaye wataalam wake wa Sekta ya Ardhi hufanya tathmini ili kujua kwamba mazao yaliyoharibiwa yana thamani kiasi gani na hufidiwa kwa mujibu wa kiwango cha uharibifu uliofanyika katika sehemu walizopita katika tafiti zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Barrick inapoendelea na tafiti zake na wanapofanya tafiti mpaka nje ya maeneo ya leseni yao kwa maana ya maeneo ya wachimbaji wadogo, hawawezi kufanya kitu chochote kinyume na taratibu zilizowekwa na sheria za nchi, ikiwemo Sheria ya Madini, Sura ya 123, Kanuni na miongozo mbalimbali ya Serikali. Kama atahitaji eneo la mtu atalifidia, kama analifanya ili aweze kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo, maana yake kumekuwa na hiyo dhana ya kuwasaidia utafiti na mitaji, basi hiyo ndiyo dhana, lakini wananchi wa maeneo hayo niwape faraja kwamba, hakuna kipande chao kitakachochukuliwa na mwekezaji kinyume na sheria au sehemu ambayo amepewa kihalali.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, upi mpango wa kuondoa tatizo la ucheleweshaji wa Vibali kwa Wachimbaji Wadogo na kutozwa mapato kwenye mchanga Mgodi wa Kebaga?

Supplementary Question 2

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la wachimbaji wadogo Nywarwana, Kata ya Kibasuka, Serikali inachukua kodi katika maeneo yale, lakini hakuna choo wala barabara ya kupita. Nini mwongozo wa Mheshimiwa Naibu Waziri katika eneo lile ili wachukue kodi halali, lakini pia watoe huduma za kijamii katika eneo lile kwani lina watu wengi sana na wanachafua mazingira? (Makofi)

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Waitara kwamba nikitoka kujibu maswali hapa tukutane ili niweze kujua changamoto hiyo imesababishwa na nini, kwa sababu haiwezekani tozo zichukuliwe halafu huduma muhimu kwa wananchi zisitolewe, kwa hiyo, hilo nitalifuatilia baada ya hapa. Ahsante. (Makofi)