Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacquline Andrew Kainja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari ya Igunga?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kutokana na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa Shule ya Sekondari ya Igunga, ipo mjini na bajeti ya uzio huo ni shilingi milioni 276. Halmashauri imetenga shilingi milioni 55.
Je, Serikali sasa haioni kuna haja kutoa fedha Serikali Kuu na ku-support uzio huu ili uweze kukamilika kwa ajili ya usalama wa watoto hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, ni lini Serikali sasa itaweza kutenga fedha kwa pamoja za majengo ya madarasa pamoja na uzio ili viende sambamba? Ahsante. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana masuala ya elimu na hasa kwa watoto wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, sisi sote ni mashahidi kwamba kutokana na utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi wa shule za msingi, lakini sekondari. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata udahili kuingia katika shule za msingi na sekondari, Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi kwa maana ya madarasa, lakini pia maabara za sayansi na mabweni. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa ujenzi wa uzio katika shule zetu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha kuna kuwa na miundombinu ya kutosha ya madarasa ili wanafunzi wote waweze kupata udahili kuingia katika shule zetu hizi za msingi, lakini shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, la Mheshimiwa Mbunge ambalo anataka Serikali Kuu iweze kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio, lakini kwa misingi ile ile ya ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Serikali za Mitaa zina jukumu la msingi la kutafuta bajeti, kupata mapato, lakini kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi ikiwepo miundombinu katika sekta ya elimu kwa maana ya madarasa mabweni na uzio.
Kwa hiyo, nichukue nafasi hii, kwanza kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga kwa kutenga fedha hii shilingi milioni 55 kwa ajili ya kuanza kujenga uzio huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa wito kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa, kuendelea kutenga fedha katika mipango na bajeti zao kwa ajili ya kujenga miundombinu muhimu kama hii ya uzio kutegemeana na hali ya eneo husika.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imeanza kujenga uzio kupitia fedha zilizotengwa katika mapato ya ndani na Mkurugenzi huyu na Serikali itahakikisha inaendelea kutenga fedha kwa utaratibu huo ili uzio uweze kujengwa kwa maslahi mapana ya wanafunzi wetu. (Makofi)
Name
Issaay Zacharia Paulo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari ya Igunga?
Supplementary Question 2
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa hatua inazochukua na majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hatuwezi kuweka uzio kwenye shule zote nchini kwa wakati mmoja shule za A level na shule nyingine zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wakiwepo wale walinzi na walezi katika shule zetu. Kwa kuwa gharama ya uwekaji wa huu uzio ni mkubwa Serikali haitakiwi kufanya tathmini ya kina ili kuja na mpango mkakati wa ulinzi thabiti kwa wanafunzi wetu katika shule zetu hizi? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kwanza, Mheshimiwa Mbunge, kwa kuendelea kufuatilia na kufuatilia hasa masuala ya ulinzi wa wanafunzi wetu na maeneo ya shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya halmashauri zetu hizi kupitia mapato ya ndani zina nafasi ya kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha zinasimamia masuala ya msingi ikiwemo haya unayoyazungumza Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie kwa sababu yote ni Serikali, tutaendelea na sisi kufanya tathmini na kutengeneza msukumo na kutengeneza mwongozo mzuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kwenye shule zetu kuna kuwa na ulinzi na wanafunzi wanaweza kusoma katika mazingira yenye amani na utulivu. (Makofi)
Name
Amandus Julius Chinguile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari ya Igunga?
Supplementary Question 3
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Amandus Chinguile ipo Nachingwea Mjini na imezungukwa na makazi ya watu, je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga uzio katika shule hiyo? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa msingi wa kutafuta fedha, kutafuta mapato na kutenga kwenye bajeti zake fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya muhimu ikiwemo ujenzi wa uzio katika shule zetu. Kwa hiyo, niendelee kumkumbusha Mkurugenzi aweze kuweka katika mipango ya kibajeti katika halmashauri yake ili aweze kutenga fedha kwa kadiri ya vipaumbele na kwa kadiri ya mahitaji kwa ajili ya ujenzi wa fence katika shule hii ya Amandus Chinguile. (Makofi)
Name
Florent Laurent Kyombo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari ya Igunga?
Supplementary Question 4
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Missenyi, Serikali imejenga hosteli katika shule za sekondari na shule hizo zimejengwa pembezoni mwa makazi ya watu ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya vijana wetu kusoma.
Je, ni lini sasa Serikali itatujengea uzio katika Shule za Sekondari za Ruzinga, Bwabuki, Bunazi na Minziro ili wanafunzi wawe katika hali ya usalama?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza kwanza jukumu lake la msingi la kutenga bajeti kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya msingi katika sekta elimu. Kwa hiyo, niendelee kumkumbusha Mkurugenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi aweze kutathmini, lakini aweze kutengeneza mipango na kutenga bajeti kwa kadiri ya vipaumbele kwa ajili ya kuendeleza miundombinu muhimu hii katika sekta ya elimu. (Makofi)
Name
Samweli Xaday Hhayuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari ya Igunga?
Supplementary Question 5
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari ya Endasak, Nangwa, Mulbadaw na Balangdalalu ni za kidato cha tano na sita na zote hazina uzio.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka msukumo kwenye ujenzi wa uzio kwa sababu ya usalama wa watoto wanaosoma kwenye shule hizo?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwemo umuhimu wa ujenzi wa uzio. Niendelee kumhakikishia Serikali inatambua umuhimu mkubwa na itaendelea kutenga fedha kupita Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini kupitia miradi ya Serikali Kuu kwa ajili ya kuhakiksiha inaboresha miundombinu katika shule zetu hizi za kidato cha tano na cha sita kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge.