Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, upi mkakakati wa Serikali kujenga mifereji kudhibiti mafuriko Tabora Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, shilingi milioni 399 ambazo anasema zimekwenda mwaka 2022/2023 kujenga mifereji kwa ajili ya kupunguza mafuriko hazijaonekana kufanya kazi hiyo kikamilifu kwa sababu wananchi wetu wameendelea kupata mafuriko mwaka hadi mwaka pindi mvua zinaponyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaweza kuniambia ni mifereji ipi ambayo imetumia fedha hizo kujengwa mitaro hiyo ili tuweze kujua ni mitaro gani ambayo imejengwa kwa ajili ya kusaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri unaonaje tukimaliza Bunge hili mwezi Julai tuongozane ili tuweze kwenda kuona hali halisi jinsi ilivyo katika Manispaa ya Tabora? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kupambania wananchi kuhakikisha kwamba wanapata miundombinu bora ya mifereji hii ili kuzuia mafuriko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua shilingi milioni 399.12 katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilienda kujenga mifereji katika eneo gani? Kumjibu hilo fedha hii ilienda kujenga kilometa 2.2 katika Barabara ya Kombomasai - Kata ya Malolo, Navimajo - Kata ya Mpera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kwamba nipo tayari baaada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kutembelea na kukagua eneo hilo na ujenzi wa miundombinu hii. Nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge mimi sitasubiri mpaka mwezi Julai, mwisho wa Bunge, Jumamosi hii ninatarajia kuwa Tabora na nikuhakikishie nitaenda kukagua eneo hili kujionea hali halisi na kuona kwamba fedha hii imeenda kuwanufaisha wananchi na tutaenda pamoja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, upi mkakakati wa Serikali kujenga mifereji kudhibiti mafuriko Tabora Mjini?

Supplementary Question 2

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zilizojengwa na TARURA kwenye Wilaya ya Tanganyika zimeharibika baada ya mvua nyingi kuvunja madaraja na mifereji ikiwemo Barabara ya Ikaka - Mnyagala, Ikaka - Kamsanga. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kutokana na mvua nyingi zinazonyesha miundombinu ya barabara maeneo tofauti tofauti imekuwa ikipata changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba inaenda kufanya ujenzi wa dharura kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika ili kuhakikisha mawasiliano yanarudi, yanaunganika na yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, amenitajia barabara zake hizi, mara baada ya kutoka katika kipindi hiki cha maswali na majibu nitakaa nay echini ili aweze kuniainishia haya maeneo husika na tutayachukua sisi kama Serikali ili kuona hatua gani za dharura zinaweza kuchukuliwa ili kuhakikisha tunaunganisha mawasiliano katika maeneo aliyoyataja.

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, upi mkakakati wa Serikali kujenga mifereji kudhibiti mafuriko Tabora Mjini?

Supplementary Question 3

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Kata ya Nkwenda, Kijiji cha Nkwenda ambako kunafanyika soko linalowaleta pamoja wafanyabiashara wa Kyerwa na Karagwe kuna mtaro mkubwa sana umeelekezewa kwenye hilo soko la Nkwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua mkakati wa kujengea huo mtaro ili uweze kuwa salama kwa wafanyabiashara kuepusha mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara nyingi na kufanya soko au biashara ishindikane kufanyika kwenye eneo hilo.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu ya barabara, mifereji na hasa katika kuchochea uchumi kwa maana ya kuwezesha shughuli za uchumi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itahakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kuhakikisha inajenga mitaro katika eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge ili kuboresha mazingira na kuwawezesha wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji mali kwa utulivu na kwa urahisi zaidi.

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, upi mkakakati wa Serikali kujenga mifereji kudhibiti mafuriko Tabora Mjini?

Supplementary Question 4

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, mvua za El-Nino zimenyesha kwa kiwango kikubwa katika Halmashauri ya Itigi, Barabara ya Itigi – Damweru haipitiki kabisa, ilikuwa imejaa maji na sasa maji yameanza kukauka, lakini Barabara ya Kalangali kwenda Tulieni imeharibika kabisa haipitiki.
Je, Serikali iko tayari kutuongezea pesa za kutosha kurudisha miundombinu hii ili watu wafanye maisha yao ya kawaida?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi na hasa za wilaya na kama nilivyotangulia kusema kipaumbele cha Serikali katika kipindi hiki ni kuhakikisha inaunganisha mawasiliano ya barabara kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itatafuta fedha na itatumia taratibu za dharura kuhakikisha inaunganisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo yameathirika sana na mvua na mawasiliano yamekatika katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa uendelevu Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii ili iweze kuwa miundombinu imara ambayo inapitika kwa misimu yote na mwaka mzima.