Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Biharamulo kwa kukamilisha sub-station ya Nyakanazi?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nipongeze kwa hatua hizo kubwa ambazo zimefanyika za uwekezaji huo mkubwa wa Kituo cha Nyakanazi na hatimaye kuweza kutuondolea tatizo la kukatika katika kwa umeme, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Nyakanazi tulikuwa tunapata mradi wa umeme unaotoka Biharamulo kwenda Mkoa wa Kigoma au tunauita Kigoma – Nyakanazi ambao ulikuwa na vijiji 32, vijiji saba vikiwa Wilaya ya Biharamulo katika Kata za Kalenge na Nyanza na vijiji 25 Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua sasa katika Wilaya ya Biharamulo, hivyo vijiji saba vya Kata za Kalenge na Nyanza mpaka sasa baada ya kumalizika mradi ule ni wateja wangapi wameunganishiwa umeme kutokana na vijiji hivi saba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mradi huu mkubwa wa kutoka Geita kuja Nyakanazi na kutoka Rusumo kuja Nyakanazi ulipitia maeneo ya watu na walistahili fidia. Nadhani mwaka jana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati akiwa Biharamulo tuliomba wale watu ambao hawajalipwa pesa zao waweze kupatiwa pesa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kusikia kauli ya Serikali, mmefikia wapi na maandalizi ya kuwalipa pesa wale waliokuwa wamepitiwa na ule mradi ili sasa kwa sababu umeme unawaka na walipisha maeneo yao wao waweze kupata haki yao ya kulipwa fidia ambayo imechukua muda mrefu sana, wale waliokuwa wamebaki wachache kama 32? Ahsante sana.

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, Engineer Ezra Chiwelesa kwa kazi nzuri anayoifanya kuwatetea wananchi wa Biharamulo na ninaomba kujibu maswali yake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji saba vilivyopo katika Kata za Kalenge pamoja na Nyanza mpaka sasa tumeshaunganisha wateja 615 na kwa sababu kazi hii ni endelevu, tunaendelea hivyo kadiri wananchi wanavyofanya wiring tunaendelea kuwaunganisha na umeme. kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kazi hii inafanyika vizuri sana na REA kwa kushirikiana na TANESCO.

Kuhusu swali la pili la fidia, ipo katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni Geita – Nyakanazi. Kwa Geita – Nyakanazi malipo ya Serikali yaani statutory compensation tayari imeshafanyika kwa wananchi wote, ambacho kimebaki ni top up compensation ambapo mkandarasi anatakiwa kuongeza ili waweze kulipwa kwa viwango vya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaambiwa mshauri elekezi anatarajiwa kuja hivi karibuni ili kuweza kufanya survey pamoja na masuala mengine ya kiutendaji ili wananchi hawa waweze kumaliziwa ile top up compensation ya mfadhili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipande cha Rusumo – Nyakanazi kulikuwa na wananchi 1,024 na wananchi takribani 986 wameshalipwa fedha shilingi bilioni 3.7 na wannchi waliobaki ni 38 tu ambapo wanadai shilingi milioni 81.02. Wananchi hawa hawajalipwa kwa sababu ya changamoto za mirathi na migogoro mingine, lakini fedha zao zipo na kadiri ambavyo wataweza kukamilisha taarifa zao na kuweza kumaliza migogoro na kukamilisha taratibu za mirathi watapatiwa fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, fedha za wananchi hawa zipo, taratibu zikikamilika hawa 38 waliobaki katika kipande cha Rusumo – Nyakanazi na wenyewe watalipwa fedha zao, ahsante.

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Biharamulo kwa kukamilisha sub-station ya Nyakanazi?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kahama ina mkandarasi mmoja tu wa kupeleka umeme wa REA vijijini pamoja na halmashauri zake tatu. Sasa ilhali amezidiwa na malalamiko ni makubwa sana kwa wananchi wetu, ni nini mkakati wa Serikali wa kupeleka kila halmashauri mkandarasi wake ili kuondoa malalamiko haya kwa wananchi?

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpa pole Mheshimiwa Cherehani kwa changamoto hii ya mkandarasi. Nataka nimhakikishie kuwa tunafahamu changamoto ya mkandarasi huyu wa Kahama na tayari tumeshachukua hatua ikiwemo kukaa naye na kuweza kujua ni namna gani tunamwongezea nguvu ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, ndani ya hizi wiki mbili, tatu mimi na yeye tuongozane twende Kahama ili tuweze kuangalia utekelezaji wa miradi hii katika eneo hili kwa sababu ni kweli kuna changamoto, lakini sisi dhamira yetu ni kutatua changamoto hizi ili wananchi wapate umeme kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunafahamu changamoto za mkandarasi na tutaendelea kumsimamia kwa weledi mkubwa sana kuhakikisha anamaliza kazi ambayo alitakiwa kuimaliza kwa wakati, ahsante.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Biharamulo kwa kukamilisha sub-station ya Nyakanazi?

Supplementary Question 3

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa kazi ya kusambaza umeme vijijini. Mara ya mwisho nilikuwa nimekuomba kuhusiana na unyeti wa kupeleka umeme katika Vitongoji vya Songea Pori pamoja na Nindi ambavyo viko mpakani na Msumbiji. Nilikuwa napenda kukumbusha na kujua labda pengine kama kuna hatua ambazo tayari zimeshaanza kuchukuliwa, ahsante.

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nianze kwa kumpongeza mama yangu Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Nyasa. Serikali kwa mwaka huu wa fedha unaokuja 2024/2025 tayari tumetenga fedha ya kupeleka umeme kaika vitongoji 4,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwamba hivi vitongoji viwili ambavyo amevitaja hapa kwa unyeti wa maeneo haya kwa sababu yako mpakani, tutazingatia ili na yenyewe yaingie katika mpango wa mwaka wa fedha unaokuja ili wananchi wa vitongoji hivyo waweze kupata umeme, ahsante.

Name

Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Biharamulo kwa kukamilisha sub-station ya Nyakanazi?

Supplementary Question 4

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa katika Jimbo la Tunduru Kaskazini? Ahsante.

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia kaka yangu Mheshimiwa Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini kwa kazi kubwa anayoifanya katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki ni muhimu sana kwetu sisi kwa sababu ni sehemu ya mradi wa kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, fidia katika eneo hili ni kipaumbele kwenye Serikali ya Awamu ya Sita na tunaendelea kufanyia kazi ili hivi karibuni wananchi hawa waanze kulipwa fidia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kaka yangu Mheshimiwa Zidadu na wananchi wa Tunduru kuwa fidia hii Serikali tunaenda kuilipa, watulie na watupe muda kidogo tumalizie taratibu ili tuanze kuwalipa, ahsante.