Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kukomesha kabisa ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu wengi?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, nimeona wameainisha wanatoa mafunzo kupitia luninga na redio, lakini ajali nyingi zina-base kwenye bodaboda na hawa hawana muda kabisa wa kusikiliza redio wala kuangalia luninga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha bodaboda wanapata elimu ya usalama barabarani ili kuepuka athari hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa na ucheleweshwaji wa ulipwaji wa bima ya ajali kwa watembea kwa miguu na bodaboda, lakini inaonekana kuna kucheleweshwa kwa nyaraka kutoka Polisi. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha nyaraka hizi zinapelekwa kwa wakati ili kunusuru afya za wananchi? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ipo tabia hii ambayo vijana wa bodaboda wanajifunza uendeshaji wa pikipiki bila kulazimika kuingia vyuoni na ndiyo maana kwa kutambua changamoto hiyo imeelekezwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Maafisa wa Usalama Barabarani wa Wilaya (DTOs na RTOs) wameandaa mikakati maalumu ya kuwatembelea kwenye vituo vyao na kuwapa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafarijika baadhi ya maeneo Waheshimiwa Wabunge wameshiriki kutoa motisha kwa hawa Maafisa wa Usalama Barabarani kuwafundisha vijana hawa ikiwa ni pamoja na kuwakatia leseni za udereva wa vyombo hivi vya moto. Kwa hiyo, nina imani hali hiyo ikiendelea walio wengi watafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili, juu ya bima za ajali na nyaraka kuchelewa Polisi ni maelekezo yetu ya Serikali kwa Makamanda wote wa Mikoa kuwasimamia RTOs na DTOs wasiwe vikwazo vya kuchelewesha nyaraka ambazo ni msingi wa waliopata ajali hizi kulipwa bima kwa mujibu wa sheria, nashukuru.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kukomesha kabisa ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu wengi?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ajali nyingine za bodaboda zinatokana pengine na kutokuwa na maeneo rasmi ya maegesho hususani katika maeneo mengine ya viwanja vya ndege wanapokuwa wanagombea abiria.

Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa kutenga maeneo maalumu ya maegesho kwa bodaboda na bajaji jirani na maegesho ya magari ili wasigombanie abiria na kusababisha ajali? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Mbunge Mabula ni ya msingi na kwa sababu maeneo menhi haya yako kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa iliwahi kuelekezwa na wao ni Wajumbe wa Kamati za Usalama Barabarani ngazi za Wilaya na Mikoa na hata makao makuu, wafikirie kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya vijana wanaoendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ku-park, kufanya maegesho na hivyo kuwa na utaratibu mahususi wa kuwachukua abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, vijana hawa katika maeneo mengine wameshapiga hatua ya ustaarabu kwa sababu wana vikundi vinavyotambulika, wana mfumo wa uongozi na vilevile hujipangia huyu wa kwanza, akimaliza anafuata wa pili, hiyo inaondoa uwezekano wa kunyang’anyana abiria, ambapo inakuwa sehemu ya chanzo cha ajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa makundi yote ya bodaboda katika mikoa na wilaya zote kutumia utaratibu kama huo ili kwanza kuboresha mfumo wa usafirishaji na la pili ni kuepuka ajali za barabarani, ahsante.