Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tamima Haji Abass

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini ukoje?

Supplementary Question 1

MHE. TAMINA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wataalamu wa elimu ya lishe wanaotoa elimu ndani ya maeneo yetu wanakidhi mahitaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kuna mikoa 12 yenye lishe duni nchini, je, Serikali ina mikakati gani ya ziada ambayo itapeleka elimu zaidi ili kuondokana na hali hiyo? Ahsante. (Makofi)

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Tamina Haji Abass kwa maswali yake mawili mazuri kwamba je, wataalamu wanaotoa elimu ya lishe wanakidhi mahitaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukiri bado hatuna wataalamu wa kutosha wa masuala ya lishe, lakini kwa sababu tume-integrate, tumejumuisha masuala ya lishe katika mitaala ya wanafunzi wetu, kwa hiyo, walimu wetu ambao wanasomea ualimu pia, kwa hiyo wanapata mada katika masuala ya lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu katika bajeti yetu tunaanza kutoa diploma ya masuala ya lishe maana zamani ilikuwa ni degree, lakini sasa hivi tunaanza kutoa diploma ya lishe, tunaamini tutapata Maafisa Lishe wengi ambao wataweza kufanya kazi katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu pia kwamba mikoa 12 yenye lishe duni mnafanya nini, tuna mambo makubwa mawili, la kwanza kupitia utekelezaji wa Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKE) ambapo tumeelekeza kila kijiji, kila mtaa katika kila baada ya miezi mitatu kukutana, kuhamasishana na kuelemishana masuala ya lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaamini kupitia utekelezaji wa Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji tutaweza pia kusambaza elimu ya lishe kwa makundi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumezindua mpango wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao tutakuwa na vijana wawili, mmoja wa kike mmoja wa kiume katika kila kitongoji cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika kila mtaa kwa maeneo ya mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa pia ndiyo watakuwa askari wa mwanzo (front liners) katika kuelimisha masuala ya lishe na masuala mengine ya afya kwa ujumla.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini ukoje?

Supplementary Question 2

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nianze kwa kumpongeza sana Profesa Janabi kwa kuendelea kutoa mafunzo ya lishe bila kuchoka. (Makofi)

Je, Serikali ipo tayari sasa kushusha mafunza hayo ya lishe kwenye kata kwa wanawake hususani wanawake wa Kilimanjaro ambapo utayarishaji ndiyo muhimu kuliko hata kuwa na hivyo vitu?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Mama Shally Raymond kwa kweli amekuwa ni balozi mzuri wa kuhamasisha masuala ya lishe kwa wanawake wa Kilimanjaro na ninaamini wanawake wa Kilimanjaro wataendelea kumuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Profesa Janabi kwa kweli tunamshukuru na lakini pia tumepokea maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kupitia Mheshimiwa Festo Sanga na Mheshimiwa Musukuma kwamba elimu pia iwe customized, iwe inalenga makundi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kumtumia Profesa Janabi, lakini pia tutawatumia au tunaendelea kutumia wataalamu wengine wa lishe kutoka Taasisi yetu ya Chakula na Lishe, lakini pia wataalamu wa lishe ambao wapo katika halmashauri mbalimbali ili kuelimisha masuala ya lishe.

Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mnapokaa katika bajeti za halmashauri zetu tuhoji ni mikakati gani au ni intervention gani zinatekelezwa katika masuala ya lishe zaidi ya semina za wataalamu wa afya. Tunataka kuona wataalamu wakienda katika vijiji, katika mitaa, katika kliniki kutoa lishe na siyo ile bajeti ya lishe shilingi 1,000 ikatumika kwa ajili ya safari na semina za watumishi.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini ukoje?

Supplementary Question 3

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri unajua mikoa inayoongoza kwa uzalishaji ndiyo mikoa inayoongoza kwa udumavu, ni upi mkakati wa Wizara kwa sababu halmashauri mpaka sasa zimeshindwa wa kuweza kutoa elimu ili kuleta matokeo chanya?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Aida Khenani kwa kweli amezungumza ukweli mikoa ambayo ndiyo wazalishaji wakuu wa chakula ikiwemo Njombe, Rukwa, Katavi, Iringa na Kagera ndiyo pia wana kiwango kikubwa cha utapiamlo hususani kwa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati kama nilivyoisema changamoto siyo upatikanaji wa chakula, changamoto ni wananchi kuandaa chakula lakini pia na kula chakula mchanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba, 2023 kwa mara ya kwanza tumezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Chakula na Ulaji, mwongozo huu unahimiza katika vyakula tunavyokula kuzingatia makundi sita ya vyakula. Kundi la kwanza ni nafaka, lakini pia kundi la pili ni masuala ya vyakula vya asili ya wanyama, kundi la tatu vyakula vya asili ya kunde na mbegu za mafuta, kundi la nne ni mboga mboga, kundi la tano ni matunda, kundi la sita ni mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aida Khenani niseme tumepata fedha kutoka kwa wadau, tumeamua kidogo tusimame tuangalie zinakwenda kufanya kazi gani kwa sababu siyo tu fedha nyingi zinapelekwa, lakini tunataka kuona interventions ambazo zitagusa wananchi. Kwa upande wa Njombe tumeona wanawake pia hawana muda wa kulisha watoto kwa sababu ni wachapakazi wakubwa sana. Kwa hiyo ndiyo maana pia tunataka kuanzisha vituo vya malezi ya awali ya watoto ambapo pia masuala ya lishe yataweza kufanyiwa kazi na kuhimizwa. (Makofi)

Name

Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini ukoje?

Supplementary Question 4

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Mheshimiwa Waziri Serikali huwa inatenga shilingi 1,000 kwa ajili ya masuala ya lishe kwa watoto wetu chini ya miaka mitano, lakini mimi kama mwakilishi wa wananchi sijawahi kuona matumizi ya zile fedha hata siku moja kwenye halmashauri zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo kwa walengwa wetu ambao ni watoto wa chini ya miaka mitano?

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rehema Migilla amesema jambo zuri na nimelisema, kwanza tunaona ongezeko la shilingi 1,000 zinazotengwa kwa ajili ya lishe katika halmashauri mbalimbali, kwa hiyo na mimi naomba nirudishe jukumu kwenu Waheshimiwa Wabunge kuangalia pia au kufuatilia matumizi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kutekeleza hafua za lishe katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia fursa hii kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, lakini na Wakurugenzi wetu wa Halmashauri kuhakikisha fedha zile shilingi 1,000 zinazotengwa kwa ajili ya kutatua changamoto za lishe zitumike kwenye masuala yenye tija yanayogusa moja kwa moja wananchi na siyo mambo ambayo hayana tija.

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: - Je, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini ukoje?

Supplementary Question 5

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, wataalamu ambao wamehitimu degree ya lishe katika nchi yetu ni wengi na wapo mitaani. Je, Mheshimiwa Waziri atakubali sasa kwamba wawaajiri wale ambao wamemaliza waliohitimu degree ya lishe? Ahsante.

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Anastazia Wambura kwa swali lake zuri kuhusu wataalamu. Kama nilivyosema ni kweli tunao wataalamu katika ngazi ya degree ambapo tumejitahidi katika halmashauri nyingi sasa hivi angalau tuna Afisa Lishe, lakini tumeona ili tufanye vizuri zaidi tunahitaji Maafisa Lishe katika ngazi ya chini na tunaamini tukiwapata pia wa ngazi ya diploma wataweza pia kufika rahisi zaidi kwa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka kukuhaidi katika nafasi za ajira tutaongeza ajira kwa maafisa lishe lakini nitawaomba sana basi wasitake kubaki mjini wawe tayari kufanya kazi katika halmashauri zote ikiwemo halmashauri za pembezoni ambazo ndizo zina changamoto kubwa ya lishe. (Makofi)