Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Venant Daud Protas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: - Je, lini Serikali itazipandisha hadhi shule za Sekondari Manonga, Seif Gulamali, Simbo na Nkinga kuwa za kidato cha tano na sita?
Supplementary Question 1
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu ya Serikali Wananchi wa Jimbo la Manonga wamekuwa wakijitolea miradi mbalimbali na wanafunzi wanaokwenda kusoma katika shule za kidato cha tano na sita katika Jimbo la Manonga wanatoka Tanzania nzima.
Je, Serikali hamuoni haja sasa kwa kuwa mna upungufu wa shule za kidato cha tano na sita mkaziongezea miundombinu shule hizo za Manonga ili wanafunzi waweze kupata elimu nzuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; matatizo yaliyoko katika Jimbo la Manonga ndivyo ilivyo Jimbo la Igalula katika Shule ya Sekondari Tura. Miundombinu ya mabweni iko safi watoto wanasoma vizuri tunapokea wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali, lakini kuna chgangamoto ya bwalo la chakula. Ikifika mwezi wa 11 wakati wa masika watoto wanakosa sehemu ya kupatia chakula. Je, lini Serikali mtapeleka bwalo la chakula kwenye Sekondari ya Tura ambayo ina kidato cha tano na sita sasa hivi? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Kuhusiana na swali lake la kwanza naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba jukumu kimsingi la kujenga miundombinu ya shule za primary na za sekondari ni jukumu la Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi ya Serikali Kuu ni kuongeza nguvu tu ili kuziunga mkono Halmashauri pale zinapokuwa zimeonyesha jitihada ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue fursa hii kuendelea kusisitiza na kumkumbusha Mkurugenzi lakini na Mbunge wote washirikiane ili Halmashauri iweze kutenga fedha katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu hii inayohitajika inajengwa na shule hizi zinaweza kuombewa kupanda hadhi kuwa shule za kidato cha tano na cha sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi Serikali imeelekeza nguvu kubwa sana katika kuimarisha miundombinu ya shule ambazo zimeshapangiwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita ambacho katika Jimbo la Manonga Shule ya Ziba na Shule ya Choma zimetengewa na zinapelekewa shilingi milioni 692 kwa ajili ya kujenga mabweni madarasa na vyoo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na bwalo la chakula, naomba niendelee kusisitiza kwamba Halmashauri ziweze kufanya jitihada za kutenga bajeti kutoka kwenye mapato ya ndani ili kuweza kukamilisha miundombinu hii. Pia Serikali Kuu pale kunapokuwa na uhitaji mkubwa na yenyewe itaendelea kuunga mkono jitihada hizi zinazokuwa tayari zimeanza kufanywa na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia utaratibu huo huo, jitihada za Serikali Kuu na jitihada pia za Mamlaka za Serikali za Mitaa tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba bwalo hili la chakula katika shule uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge linajengwa ili wanafunzi wetu waweze kupata miundombinu mizuri katika shule hiyo.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: - Je, lini Serikali itazipandisha hadhi shule za Sekondari Manonga, Seif Gulamali, Simbo na Nkinga kuwa za kidato cha tano na sita?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mlalo tunazo sekondari 31 na sekondari za Mkundi, Mtumbi pamoja na Mtaya zote hizi miundombinu yake inaruhusu uanzishwaji wa madarasa ya kidato cha tano na sita. Je, Serikali iko tyari kuzifanyia kazi shule hizi ili ziweze kuwa na kidato cha tano na sita? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mbunge amekuwa ni mahiri sana katika kuhakikisha anapambania changamoto za wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali hili. Kama shule hizi alizozitaja za Mkundi, Mtumbi na Mtale zina miundombinu hitajika basi hatua inayofuata ni Mkurugenzi kuweza kupeleka maombi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuomba kupandishwa hadhi kwa shule hizi kwa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo naomba nichukue fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi aweze kufanya tathmini katika shule hizi ili kuona kama zina miundombinu hitajika aweze kupeleka maombi ya kupandisha hadhi shule hizi ili ziweze kuwa shule za kidato cha tano na cha sita.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: - Je, lini Serikali itazipandisha hadhi shule za Sekondari Manonga, Seif Gulamali, Simbo na Nkinga kuwa za kidato cha tano na sita?
Supplementary Question 3
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuwapa wananchi wa Kilimanjaro pole kwa kuondokewa na Katibu Tawala wetu. Nilikuwa nauliza swali, Shule ya Sekondari Ng’uni imekuwa na majengo chakavu sana na wananchi wamejitahidi kuanza ujenzi wa maabara pale shuleni. Je ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya kumalizia majengo haya lakini pia na mabweni ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Ng’uni?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yenye tija kabisa kwa ajili ya wananchi wake. Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia miundombinu chakavu na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea na utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la ujenzi wa mabweni. Kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu ya awali nimesema kwamba Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza kujenga miundombinu muhimu katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa utaratibu huohuo naomba nichukue nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba Mkurugenzi mshirikiane pamoja ili kuhakikisha kwamba mnatenga fedha katika mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hii muhimu. Pia, kama nilivyotangulia kusema, Serikali Kuu itaongeza nguvu kwa ajili ya kuhakikisha pale jitihada zinapokuwa tayari zimeanzishwa Serikali iweze kuunga mkono ili kuhakikisha miundombinu hii muhimu inakamilishwa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge toa shaka Serikali itahakikisha ushirikiano na utaratibu huo mabweni haya yanajengwa. (Makofi)