Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Gibson Blasius Meiseyeki
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Arumeru-Magharibi
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, hatua gani zinachukuliwa ili kupunguza changamoto ya walimu katika shule za msingi na sekondari mkoani Mara?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ni dhahiri kwamba Serikali kwa sasa imewekeza sana kwenye kujenga miundombinu ya shule kwa maana ya kuongeza madarasa kwa shule za msingi na sekondari. Vilevile kupitia elimu bila ada imehamasisha wananchi wengi kuweza kupeleka watoto wao shule. Sasa hii kasi ya kuajiri walimu 12,000 kwa mwaka ni kasi ndogo sana ukilinganisha na upungufu wa walimu uliopo Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani Mkoa wa Mara kwa shule za msingi tuna uhitaji wa walimu 14,000 lakini waliopo ni 8,000 tu. Tuna upungufu wa walimu 6,000 na kitu, walimu wanaojitolea ni 785 kwa shule za msingi na sekondari ni 284. Serikali inapokuwa inaajiri walimu haitoi kipaumbele kwa hawa wanaojitolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, ni kwa nini msishushe waraka kwenda halmashauri kutoka kwenye own source zao walau waweze kutenga kati ya shilingi 100,000 mpaka 200,000 kuwapa kama token hawa wanaojitolea ku-supplement ile ambayo wazazi wanachanga ili watoto wetu waendelee kupata masomo na haki ya kufundishwa kama wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hata Dira yetu ya Maendeleo inasema uchumi shindanishi na viwanda kwa maendeleo ya watu. Sasa ukiangalia takwimu za walimu wanaofundisha masomo ya sayansi Mkoa wa Mara tunauhitaji wa walimu 1,900 wakati tunao walimu 1,000 tu. Sasa hivi Serikali inajenga shule za sayansi kwa wasichana kwenye mikoa yetu hii. Serikali inachukua jitihada gani kuhakikisha kwamba inaajiri walimu wengi wa sayansi ili kwenda kuziba haya mapengo? Kwa sababu usipokuwa na walimu wa sayansi, watoto wanamaliza bila kupata elimu na viwanda vyenyewe tunavyovileta hapa Tanzania havitapata wajuzi.
Name
Gibson Blasius Meiseyeki
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Arumeru-Magharibi
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana. Kama alivyosema yeye mwenyewe ametambua jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata elimu iliyo bora na ndiyo maana kwa sasa hivi tunatekeleza Mpango wa Elimu Bila Ada na matokeo yake udahili umeongezeka na mahitaji ya miundombinu ya elimu yameongezeka na uhitaji wa walimu umeongezeka na Serikali imekuwa na mikakati tofauti tofauti kuhakikisha inaboresha miundombuinu, lakini pia kwenye eneo la walimu Serikali inachukua hatua, mfano ajira, kwa hiyo, Serikali tayari kila mwaka inahakikisha kwamba inaajiri walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili Serikali inatumia mpango wa walimu wa kujitolea na Mheshimiwa Mbunge hapa amefanya rejea. Kwa hiyo, Serikali kwa kutumia utaratibu huo inakuwa inahakikisha kwamba inaongeza pia idadi ya walimu wanaohitajika. Nitatoa tu mfano, katika Mkoa wa Mara kuna walimu wa kujitolea 625 katika shule za primary na walimu 185 wa kujitolea katika shule za sekondari. Serikali pia inatumia mbinu ya kutumia TEHAMA na hivi sasa Serikali imeanzisha ujenzi wa madarasa janja (smart classes) ambayo yanatumia TEHAMA na mwalimu mmoja anaweza kufundisha shule tofauti tofauti au shule zaidi ya moja na nje ya mkoa mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatumia na imeanzisha utaratibu wa kuanza kuwatumia wanafunzi wa ualimu na kuwapa ule mwaka mmoja wanakuwa wanafanya mafunzo kwa vitendo (internship). Hii yote ni mikakati ya kuhakikisha kwamba Serikali inapunguza ukali wa upungufu wa walimu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge katika swali lako hili la kwanza Serikali itaendelea na utaratibu wa kutoa miongozo mbalimbali na kutumia hii mikakati ili kuhakikisha kwamba inabuni namna nzuri zaidi ya kuweza kuongeza walimu. Kama vile Serikali inavyohakikisha kwamba inajenga miundombinu mizuri ya kutosheleza ongezeko la udahili wa wanafunzi, basi hivyo hivyo itahakikisha kwamba inaongeza walimu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka za Serikali za Mitaa tumeshawaelekeza kwamba wanaweza wakatumia mapato ya ndani kwa ajili ya kulipa walimu wanaojitolea ili na wenyewe kuchangia katika kupunguza upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili ameuliza kuhusiana na walimu wa sayansi; Serikali itazingatia katika ajira hizi lakini katika upatikanaji wa walimu kwa njia nilizozitaja hapo awali, kwamba wanapatikana walimu wa sayansi na hasa huko vijijini kwa sababu huo ndiyo mpango wa Serikali na ndiyo mpango wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu iliyobora. Pia amejielekeza katika kuhakikisha tunajiimarisha katika masomo ya kisayansi. Kwa hiyo, kuna kila sababu ya kuhakikisha tunapata walimu walio bora wa kutosheleza kufundisha masomo ya kisayansi.
Name
Selemani Moshi Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, hatua gani zinachukuliwa ili kupunguza changamoto ya walimu katika shule za msingi na sekondari mkoani Mara?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa halmashauri zilizo na uhaba mkubwa sana wa walimu hasa katika Kata ya Ilangu, Ipwaga, Mnyagala na Isengule kwenye shule za sekondari.
Je, ni lini wataleta walimu ili waweze kufanya kazi kwenye maeneo ya kata hizo?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mbunge, swali lake ni la msingi na kama nilivyotangulia kujibu hapo awali, Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 mwaka huu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na yeye kwenye jimbo lake atapata mgao wa walimu hawa 12,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza mbinu na mikakati mbalimbali ambayo pia inatumiwa na Serikali kupunguza ukali wa upungufu wa walimu. Mkakati mmojawapo ni kuhakikisha kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa na zenyewe zinajipanga kutenga bajeti kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuweza kuajiri walimu kwa mikataba ili waweze kupunguza ukali wa uhitaji wa walimu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwa njia hizi Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inaleta walimu shuleni katika jimbo lako lakini pia inatumia mbinu tofauti tofauti za kupunguza ukali wa upungufu wa walimu.
Name
Nicodemas Henry Maganga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, hatua gani zinachukuliwa ili kupunguza changamoto ya walimu katika shule za msingi na sekondari mkoani Mara?
Supplementary Question 3
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbogwe ina changamoto ya upungufu wa walimu, je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri walimu wanaojitolea kwenye Halmashauri ya Mbogwe?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu awali kwamba Serikali itaendelea kuajiri walimu na katika mgao wa walimu hawa 12,000 wanaotarajiwa kuajiriwa, Mheshimiwa Mbunge na wewe utapata mgao wa walimu kwenye shule zilizopo katika jimbo lako, lakini kupitia mapato ya ndani ya halmashauri pia mnaweza mkatenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuhakikisha mnaweza kuajiri kwa mikataba pia kuwalipa posho walimu wanaojitolea.