Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kujenga mitaro ili kuzuia uharibifu wa barabara unaosababishwa na mvua katika maeneo ya milimani Mkoani Kilimanjaro?

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naishukuru Serikali kwa juhudi za kutenga fedha za kujenga mitaro hiyo, lakini kwa kuwa tatizo hili ni kubwa sana na ni la siku nyingi na ni endelevu, naomba kufahamu, je, Serikali imeshafanya usanifu kwenye maeneo gani ya kuleta suluhisho la kudumu katika maeneo yote hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo hili liko Mkoa wote wa Kilimanjaro katika majimbo yote tisa, kuanzia Jimbo la Siha, Hai, Moshi Vijijini, Vunjo, Rombo, Mwanga, Jiimbo la Same Mashariki hadi Same Magharibi na hata Manispaa ya Moshi huwa inaathirika na tatizo hili. (Makofi)

Sasa swali langu, kwa kuwa maji hayo yakitoka kwenye milima yanatirirka hovyo barabarani, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabwawa ya kukinga maji hayo ili yatumike kwenye kilimo au mifugo na tatizo hili kuisha kabisa? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake haya muhimu sana na yenye tija. Naomba nimjibu maswali yake yote mawili kwa pamoja kuwa tafiti tayari zilifanyika mwaka 2014 katika Wilaya ya Siha na Serikali ilibaini kwamba ujenzi wa barabara za zege una tija sana, lakini ikabaini pia kutua paving blocks na strip concretes na ujenzi wa majaribio ulifanyika katika barabara ya Lawate – Kibong’oto na kimsingi majaribio yalionesha ufanisi mkubwa.

Kwa hiyo, kwa hivi sasa baada ya kufanya performance evaluation, majaribio na kuonesha ufanisi sasa mkoa unatekeleza ujenzi wa miundombinu hii katika maeneo mengine ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala lake ni la muhimu sana na Serikali tayari imeshakuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inajenga miundombinu iliyobora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mapendekezo, mawazo na ushauri wako wa ujenzi wa mabwawa ya kupokea maji hayo kwa ajili ya matumizi ya kilimo, ni maoni na mawazo mazuri na sisi kama Serikali tunayapokea, kuyachakata na kuona namna nzuri ya kufanya utekelezaji wake.

Name

Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kujenga mitaro ili kuzuia uharibifu wa barabara unaosababishwa na mvua katika maeneo ya milimani Mkoani Kilimanjaro?

Supplementary Question 2

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha zege barabara zilizopo kwenye miinuko katika Milima ya Matumbi inayoanzia Pungutini kupitia Mwengei kwenda Kibata hadi Kipatimu?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiboresha kufanya ujenzi na marekebisho ya miundombinu ya barabara kwa kuzingatia pia topografia ya eneo husika na kama nilivyotangulia kutolea mfano katika maeneo ya Kilimanjaro ambayo yana miinuko. Serikali imekuwa ikitumia teknolojia ya kuweka zege ambayo inakuwa na ubora zaidi na inaweza kuhimili changamoto mbalimbali za kimazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika utaratibu huo huo Serikali itaendelea kuhakikisha inatafuta fedha kuhakikisha kwamba miundombinu bora hii ya zege na hasa katika maeneo ya miinuko katika jimbo lake yanaweza kujengwa ili nao waweze kupata barabara zilizobora zitakazopitika katika mwaka mzima na zitakazoweza kuhimili misukosuko ya kimazingira.

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kujenga mitaro ili kuzuia uharibifu wa barabara unaosababishwa na mvua katika maeneo ya milimani Mkoani Kilimanjaro?

Supplementary Question 3

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ninavyoongea sasa hivi barabara ya kutoka Nkwenda kwenda Mabira, pia barabara ya kutoka Kakanja kupita Kikukuru mpaka kwenda Kitwe hazipitiki na sasa ni wakati wa kiangazi na ni maeneo makubwa ambayo sasa yanazalisha kahawa. Nini mkakati wa dharura wa kutengeneza hiyo barabara ili tuweze kupeleka kahawa yetu sokoni?

Name

Yussuf Kaiza Makame

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chake Chake

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua za dharura kufanya marekebisho katika maeneo ya barabara ambazo mawasiliano yamekatika na imekuwa ikifanya hivyo katika maeneo mbalimbali ya nchi, hasa ukizingatia athari ambazo zimetokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na barabara hii ya Nkwenda – Mabira na Barabara ya Kakanza – Kitwe, ambayo anasema ni muhimu sana hasa katika biashara ya kahawa. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, sisi Serikali tumepokea na kwa sababu kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha inarudisha mawasiliano ya barabara kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika nakuhakikishia, Mheshimiwa Mbunge, suala hili tumelipokea, kwa ajili ya kulifanyia kazi. (Makofi)