Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Vita Rashid Kawawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. HUSSEIN N. AMAR K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: - Je, ni sababu gani zinazozuia kuanza utekelezaji wa Mradi wa Urani Mkuju - Namtumbo wakati ulishapata leseni ya uchimbaji na ujenzi?
Supplementary Question 1
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa mradi huu ni wa siku nyingi sana na sasa hivi gharama ya ujenzi ambayo ilishatumika ni karibu dola milioni 300 kutekeleza mradi ule, je, Serikali inaweza ikairuhusu Kampuni ile ya Mantra kuendelea wakati utaratibu wa SEA unaendelea? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mradi huu hapa sasa hivi bei yake imekuwa juu, wakati tuliposimamishwa ilikuwa dola ishirini kwa paundi ya urani, sasa hivi imefika dola mia kwa paundi ya urani, je, Serikali haioni umuhimu wa sasa hivi kutumia fursa hii kwa kuwa bei yake imekuwa kubwa ili tuweze kupata manufaa ya mradi huu? (Makofi)
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mbunge wa Namtumbo ndugu yangu Mheshimiwa Kawawa kwa jinsi ambavyo amekuwa akiufuatilia mradi huu wa kimkakati na wa manufaa makubwa kwa Taifa letu. Kwa swali lake la kwanza, Serikali kuruhusu mradi kuendelea wakati imeshaitisha zoezi la kufanya tathmini ya kimazingira ni jambo ambalo nadhani itabidi lisubiri, kwanza, kwa matumaini makubwa hilo zoezi la SEA ambalo limeanza wiki iliyopita halitochukua muda mrefu, ni miezi sita tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa sababu nilitembelea site mwezi uliopita nikaona mtambo wa majaribio waliouweka pale na mwekezaji aliniomba kwamba ingewezekana Serikali iruhusu aendelee na mradi huo wa majaribio (pilot project) ambayo ameanza mtambo mdogo, nilimhakikishia kwamba Serikali itafikiria na bado inaendelea kulifanyia kazi ombi hilo. Kama litajibiwa kabla ya SEA kukamilika basi atapata majibu yake maana Serikali haina kipingamizi na kuhakikisha kwamba mradi huu wenye tija unatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, ni kweli bei ya urani sasa hivi imepanda duniani na ni madini yenye thamani kubwa kwa sasa. Sisi kama Serikali hatuna sababu ya kuuchelewesha huu mradi zaidi ya kuhakikisha usalama wa mazingira yetu ukizingatia kwamba eneo husika lipo pembezoni au ndani ya eneo la hifadhi ambalo ni Selous pamoja na Mwalimu Nyerere National Park. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hicho ndicho kikwazo, lakini tuna hamu kubwa ya kuona mradi huu utaendelea. Hii SEA itakapojibu ndani ya miezi sita ijayo, tutauona mradi huu ukianza kutekelezwa. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved