Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI: aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kupunguza vifo vinavyotokana na mabadiliko ya hali ya hewa?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri mimi kwanza naipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa inafanya kazi nzuri sana ya kutoa tahadhari ya hali ya hewa ya nchi yetu na tahadhari ambazo ni za ukweli kwa asilimia kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa taarifa za hali ya hewa zinatolewa mapema sana, lakini Serikali haichukui hatua za mapema matokeo yake kunatokea madhara makubwa sana kama vile inaponyesha mvua kubwa katika maeneo mbalimbali. Je, mamlaka zinazohusika zina mpango gani sasa wa kuhakikisha wanafanyia kazi taarifa za hali ya hewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tumeshuhudia kunyesha kwa mvua kubwa katika maeneo na kusababisha mafuriko kama vile ya Rufiji, Kibiti, Kilwa, Lindi na Arusha - King’ori kulitokea mvua kubwa, madaraja yakavunjika mpaka gari la wanafunzi likaingia kwenye daraja.
Je, Serikali imejipanga vipi sasa kutoa taarifa pale inapotokea mvua inanyesha angalau kusimamisha masomo kwa wanafunzi wa shule za msingi na nursery school? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa pongezi kwa Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa kwa kazi kubwa ambayo wanafanya na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa sana ambao Serikali imefanya katika kuiwezesha mamlaka hii itoe taarifa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumza kuhusu kufanyia kazi, Mamlaka ya Hali ya Hewa ina jukumu kubwa la kuangaza, kukusanya, kuchakata pamoja na kuhifadhi na kusambaza taarifa za hali ya hewa na mara baada ya kukamilisha jukumu hilo la kwanza, jukumu la pili ambalo linafanyika sasa ni namna gani taarifa hizo zinakwenda kuwafikia wananchi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tunayo sheria ya mwaka 2006 ambayo ni Sheria yetu ya TMA inaipa mamlaka kufanya kazi hiyo, lakini pia tuna Sheria ya Maafa Namba 6 ya mwaka 2022 ambayo kimsingi inatoa nafasi kwa Kamati zetu za Maafa mbalimbali nchi nzima. Mara baada ya kupokea taarifa za TMA, kuhakikisha kwamba zinasambazwa na kufikishwa katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Serikali kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali imeendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, kuimarisha mifumo yetu ya tahadhari pamoja na kujenga uwezo wa watendaji ili kuhakikisha kwamba taarifa zinakuwa sahihi, lakini pia zinafika kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru pia kwa swali lake la pili juu ya ushauri alioutoa kwamba pengine inapotolewa taarifa hizo za hali ya hewa pengine kutakuwa labda na kimbunga na kadhalika, ni vyema shule zikafungwa. Ushauri huu ni mzuri na sisi kama Serikali tumeupokea, tutaenda kuuchakata na kuufanyia kazi hatua kwa hatua. (Makofi)
Name
Bakar Hamad Bakar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI: aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kupunguza vifo vinavyotokana na mabadiliko ya hali ya hewa?
Supplementary Question 2
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru, ni kweli kwamba Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa inafanya kazi nzuri hivi sasa kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Mheshimiwa Rais ameuwekeza, lakini kumekuwa na changamoto kwa wadau na taasisi mbalimbali zinazotumia taarifa hizi, kuchelewesha malipo kwa mamlaka yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni ipi kauli ya Serikali kuhusiana na taasisi hizi ambazo zinachelewesha malipo baada ya kutumia taarifa za hali ya hewa ili taarifa zetu za hali ya hewa ziendelee kuwa endelevu na bora zaidi? Ahsante. (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Bakar kwa swali lake la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatumia nafasi hii kuomba taasisi mbalimbali ambazo kimsingi ni wanufaika wa taasisi hii au taarifa za taasisi hii ili waweze kulipa ndani ya muda kwa ajili ya kusaidia mamlaka yetu ipate fedha na kuongeza uwezo zaidi, iweze kutengeneza au kuandaa taarifa zingine sahihi zaidi kuliko pengine livyokuwa hapo mwanzoni. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved