Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha maporomoko ya Kalambo yanatangazwa kitalii?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutangaza utalii inahitaji uwezeshaji wa kibajeti, je, Serikali itakuwa tayari kuhakikisha kwamba inaiwezesha TTB ili iwe na uwezo mkubwa wa kutangaza vivutio vilivyoko Nyanda za Juu Kusini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tuliwahi kupata ushauri kutoka Serikalini kwamba ili maporomoko ya Kalambo yaweze kufahamika maeneo mengi ni pale ambapo tutakuwa na uwanja mdogo, kwa maana ya airstrip na sisi Kalambo tayari tulishatenga eneo hilo. Je, mchakato huo umekwamia wapi ili tuwe na huo uwanja mdogo?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kuiwezesha TTB kuweza kufanya jukumu lake kubwa la kutangaza vivutio vyetu vya utalii. Kama mtakavyokumbuka katika Bunge la mwaka huu Serikali iliridhia kutenga asilimia sita ya mapato ya utalii yaweze kutumika kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utalii, hususani kuitangaza sekta hii. Kwa hiyo, nimhakikishie kuwa tupo vizuri kwenye eneo hili na kazi itafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la pili la uwanja wa ndege, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anafahamu, wataalamu wetu wa TANAPA walishafanya ziara kwenye eneo hili ambalo wenzetu wa Kalambo walitupa maeneo matatu yanayoweza kujengwa uwanja wa ndege. Tulituma wataalamu wetu na vilevile Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilifika kule, kuna tathmini inafanyika ndani ya Serikali. Naomba wawe na subira wakati Serikali inajipanga kutekeleza jambo hili. (Makofi)