Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabani ya kisasa na ya kudumu ya kukaushia tumbaku, Ulyankulu?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kutokana na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuweza kututengea shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kujenga mabani mapya 600 ya kisasa. Ni ukweli kwamba Serikali mmekiri kuna upungufu mkubwa wa haya mabani na kutokana na ukubwa wa tatizo la athari ya mvua ya msimu uliopita mabani haya 600 ni machache sana. Je, sasa Serikali haioni kuna umuhimu wa kutoa ruzuku ili kuweza kuwajengea wakulima wetu wa tumbaku ambao kwa kiasi kikubwa walipata athari kubwa, hali ambayo imesababisha uzalishaji wao kuwa wa kusuasua?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kulingana na ukubwa wa athari ya mvua iliyonyesha msimu uliopita, wakulima wengi wa tumbaku wamelowesha mashamba yao, mabani yao yameanguka, na hata mitaji yao kuweza kupotea. Hali hii imesababisha hao wakulima waweze kushindwa kufidia au kulipa madeni kwenye vyama vya msingi. Kutokana na hali hiyo kampuni za ununuzi ziliweka madalali wa kufilisi dhamana na mali za wale wakulima wetu, hali ambayo kampuni hizi za udalali zimesababisha taharuki kubwa sana kwa hao wakulima wetu, wakulima wamenyang’anywa mashamba, nyumba na mali zao nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni sababu na haja kubwa ya kusitisha hawa madalali wa kufilisi wakulima wetu, ilhali hali halisi ya athari ya mvua wameiona? Ahsante.
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Rehema kwa kazi nzuri anayoifanya katika jimbo lake, hususani kufuatilia wakulima wa tumbaku. Nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya jitihada ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha athari zote zilizosababishwa na mvua kwa wakulima sisi tunakuwa sehemu na ndiyo maana sehemu ya kwanza tumetenga fedha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kusaidia kujenga mabani ya kisasa, lakini tutaendelea kutenga fedha hata katika mwaka unaokuja, ili kuhakikisha lengo la mabani yote yaliyopo tunaweza kulifikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu tutaendelea kutoa ruzuku katika maeneo mengine ikiwemo mbolea na dawa kwa wakulima wa tumbaku. Vilevile kwenye hili jambo tutaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wale madalali ambao wametumika kunyang’anya mali za wakulima wa tumbaku, niseme sisi kama Wizara, jambo hili tunalifahamu. Tumekuwa tukilifuatilia na tumesema baada ya hapa tutaendelea kufanya vikao zaidi ili kupunguza athari ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa wakulima kuuziwa mali zao. Kwa hiyo, tunalifahamu na tunalifanyia kazi, nimuondoe shaka Mheshimiwa Mbunge, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved