Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha kuweka changarawe katika barabara inayounganisha Tarafa za Umba, Mlalo, Mtae ya Hekicho, Lugurua hadi Manolo?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa mara ya kwanza naomba nikiri wazi kwamba Serikali imejibu maswali kwa ufasaha sana, swali hili limejibiwa kwa ufasaha na hali ndivyo ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna ambavyo amekuwa akiendelea kujibu kwa ufasaha maswali ya Wabunge hapa Bungeni, namuombea Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki na fahamu zake zizidi kukua kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza. Barabara hii imekuwa ni mkombozi mkubwa haswa hivi karibuni tulipata mvua ambazo zilifunga barabara kubwa ya TANROADS, barabara hii ikawa ndiyo mkombozi. Lakini zipo kona kali ambazo magari makubwa kuanzia tani nne na kuendelea yanashindwa kupita kwa ufasaha.

Je, Serikali ipo tayari kurekebisha hizi kona takribani tatu ili barabara hii iweze kuwa na ufanisi zaidi? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kupokea pongezi za Mheshimiwa Mbunge pia na mimi nimpongeze kwa utumishi wake uliotukuka kwa wananchi wake na hasa kwa sababu amekuwa akifuatilia sana masuala ya miundombinu ya barabara kwenye Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la nyongeza alilouliza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge TARURA inatambua uwepo wa hizo kona kali tano, ambazo kimsingi zinazuia magari yenye zaidi ya tani nne kuweza kupita. Katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga milioni 328 kwa ajili ya kuanza kurekebisha kona mbili kati ya hizo kona tano ambazo zimebainika ni kali sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Serikali itatumia hizi fedha milioni 328 kupasua miamba na kuweka tabaka la zege ili magari yaweze yenye ukubwa wa kuanzia tani nne hadi 10 yaweze kupita. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itahakikisha inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu na hasa katika barabara uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.(Makofi)

Name

Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha kuweka changarawe katika barabara inayounganisha Tarafa za Umba, Mlalo, Mtae ya Hekicho, Lugurua hadi Manolo?

Supplementary Question 2

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2022/2023 tulipokea milioni 500 kwa ajili ya kujenga barabara ya kiwango cha lami kutoka Manyinga kwenda Madizini yenye urefu wa kilomita moja, lakini jambo la kushangaza barabara hii imejengwa mita 500. Kipindi kifupi cha miezi sita barabara hii ikawa imeharibika.

Je, Serikali ipo tayari kufanya ukaguzi maalum wa kujiridhisha na matumizi ya hizi fedha milioni 500? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba inajenga na inakarabati barabara kwa viwango vinavyokubalika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala alilolitaja kuhusuana na hii barabara yake ya Manyinga, tumelichukua na tutaliweka katika vipaumbele kuhakikisha fedha zinatengwa na barabara zinarekebishwa na kujengwa kwa viwango vinavyokubalika, kwa sababu hiyo ndiyo dhamira ya Serikali.