Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Salim Alaudin Hasham

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Primary Question

MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja linalounganisha Kata ya Mwaya na Mbuga lililovunjika tangu mwaka 2023?

Supplementary Question 1

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninashukuru sana Serikali kwa kuwa tayari kujenga daraja hilo, lakini ili daraja liwe na tija zaidi ni lazima kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kutoboa ili kuunganisha kati ya barabara ya Wilaya ya Liwale pamoja na Ulanga inayopita katikati ya Mbuga ya Mwalimu Nyerere. Sasa ni lini Serikali itakuwa tayari kufungua barabara hiyo ili kuunganisha Mikoa ya Kusini pamoja na Morogoro?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni lini Serikali itaunganisha barabara ya kutoka Makanga – Mafinji ili kuunganisha Wilaya ya Ulanga na Malinyi na kurahisisha usafiri, kwa sababu sasa hivi wananchi wanazunguka kilomita 80 ili kufika Wilaya ya Malinyi? Ila barabara hiyo ikiisha itakuwa inapitika kwa kilomita 30 peke yake. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kumalizia barabara hiyo? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli amekuwa akifanya ufuatiliaji mkubwa sana katika masuala haya ya kupata barabara katika jimbo lake, lakini pia katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, ametaka kujua ni lini na mkakati wa Serikali ni upi katika kuhakikisha kwamba inajenga barabara ile ambayo itaunganisha Wilaya ya Liwale pamoja na Wilaya hii ya Ulanga ambayo kimsingi ni Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu ambazo zinahitajika hapa ni kuhakikisha kwamba barabara hii inapandishwa hadhi, ili sasa iweze kuwa barabara ya mkoa ambayo inaunganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia Road Board, waanzishe mchakato huu ili barabara hii iweze kupandishwa hadhi, lakini pia iweze kufanyiwa upembuzi yakinifu, kwa sababu barabara itapita katika eneo la Hifadhi ya Selous. Kwa hiyo, inahitajika upembuzi yakinifu kwenye upande wa mazingira. Baada ya kukamilisha taratibu hizo barabara hii itajengwa ili iweze kuwa na tija kubwa kwa ajili ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge anauliza kuhusiana na ujenzi wa Barabara ya Makanga na Mafinji ambayo kimsingi ina kilometa 35 tofauti na barabara inayotumika sasa hivi ile njia ya Lupilo ambayo ina urefu wa kilometa 80. Ninaomba kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kwa kilometa 30 tayari imeshafunguliwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2023/2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.061.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa ma-culvert makubwa mawili. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge mchakato wa manunuzi unaendelea na pindi utakapokamilika, barabara hii itajengewa ma-culvert hayo makubwa mawili.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kilometa tano zile zinazobakia katika kilometa hizi 35, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, tumeweka katika Mpango ujenzi wa ma-culvert 15, lakini pia itatengewa fedha shilingi 900,000,000 kwa ajili ya kukamilishwa. Kwa hiyo ninakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini kuhakikisha kwamba katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge, wanapata miundombinu ya barabara iliyo bora.