Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Agnesta Lambert Kaiza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:- Je, kwa kiwango gani Sheria zilizopo za kupambana na matukio ya ubakaji zinajitosheleza?
Supplementary Question 1
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa sheria mbalimbali ambazo amezitaja Mheshimiwa Waziri, bado vitendo vya ubakaji vimeshika kasi sana hapa nchini. Kwa kuwa, zipo nchi ambazo zimefanikiwa katika suala zima la kupambana na vitendo hivyo ya ubakaji, mfano Nigeria wao wameenda mbali sana wamepitisha sheria ya kuwahasi wale wote ambao wanapatikana na hatia ya ubakaji. Swali la kwanza kwa Serikali; je, Serikali ipo tayari sasa kujifunza kwa nchi hizi ambazo zimefanikiwa kwa kufuata mfano wao ili mwisho wa siku tuweze kukomesha vitendo hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtambua kijana wa miaka 18 kama mtu mzima na ndiyo maana anaruhusiwa kupiga kura na kupigiwa kura, kuwa kiongozi, pia ana haki hata ya kuwa Mbunge wa Jamhuri la Muungano wa Tanzania. Ukiangalia sheria ya kupambana na masuala ya ubakaji, kijana wa miaka 18 anatambulika kama mtoto mdogo na hivyo akienda kubaka yeye adhabu yake ni kupigwa viboko. Je, Serikali haioni kwamba sheria hii imepitwa na wakati na hivyo inaleta contradiction kubwa sana ya Katiba Mama?
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge umeshauliza maswali mawili sasa.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: …mpo tayari kupitia upya sheria hii ili mwisho wa siku tuweze kwenda sawasawa na kijana huyu wa miaka 18 sasa, ijulikane wazi kwamba ni mtoto. Kama ni mtoto sasa basi anakuwa hana hata hizi sifa nyingine ambazo nimezitaja, lakini kama atakuwa na hizo sifa, basi sheria hii ifanyiwe marekebisho ili mwisho wa siku tuweze kuwa na ustawi wa jamii ambao umekamilika? Ahsante. (Makofi)
Name
Geophrey Mizengo Pinda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kujibu swali hili, niende kwenye maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, katika uhalisia Serikali inapotunga sheria na watungaji wa sheria wenyewe ndiyo sisi tuliopo hapa kwenye chombo hiki, kimsingi kila sheria unapoiona inakuja, inakuja kwa wakati wake na kwa uhitaji wake. Sheria katika mwenendo wake zinachakaa au zinaharibika kabisa kutokana na mfumo wa mambo mbalimbali yanayojitokeza kwenye jamii husika, hapo ndipo tunapopata nafasi ya kuzikarabati kwa maana ya kuziimarisha zikae sawa na wakati tulionao au kuanzisha sheria mpya kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ya kuhasi ambapo nchi nyingine inatumia kwanza sipendekezi sana kuiga, ninadhani ni mfumo mzuri kutengeneza kitu ambacho kitakuwa cha kwetu badala ya kuiga kwa sababu wakati wanatunga labda walikuwa na vitu vilivyowasukuma wafanye vile. Kwa ujumla wake tupokee ushauri wako kwamba, tupitie upya hizi sheria ambazo zimepitwa na wakati au zina mwingiliano ambao hauna tafsiri sahihi ya sheria na matukio ambayo yanaendelea kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la umri wa miaka 18, ni kweli kwa sababu watunzi wa sheria wote tunaletewa draft hapa na baadaye tunaipitisha, lakini uanzishwaji wa utungaji wa sheria unategemea taasisi iliyowasilisha hoja yake hapa Bungeni. Hii vilevile, imekuwa na kasoro ndogondogo za mwingiliano bila kujali kwamba, kuna sheria nyingine ambayo imesimama upande huu ikieleza jambo ambalo linamhusu kwa mfano kijana wa miaka 18.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipengele cha 13 utakiona kinaeleza umri wa miaka 18 kama umri sahihi wa mtu kutambuliwa kuwa mtu mzima, lakini kwenye sheria ya udhibiti wa mama na mtoto, mtoto wa miaka 18 bado anaonekana kwamba hajaingia kwenye kipindi chanya cha umri wa miaka 18 kuwa mtu mzima. Haya yote haya wakati tunapokwenda kwenye utekelezaji tunakutana na hizi changamoto ndiyo maana tunarudi tena kukaa na kuangalia namna ambavyo tunaweza tukazi-level zikafanana.
Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Wabunge kwamba, kwa sababu ni sisi wenyewe tumebaini, basi ipo haja na tupokee ushauri wako kwenda kuangalia pale ambapo panaleta conflict ya kisheria ili tuweze kunyoosha mapito ya sheria hii. Ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ni sheria gani hapo umeitaja ya udhibiti wa mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwenye kumbukumbu nimetaja tu kipengele cha Katiba Namba 13.
SPIKA: Aaah! Nilifikiri kuna sheria nyingine pengine inaitwa hili jina, lakini hii ya miaka 18 kwamba ni mtoto hawezi, hii tumeiweka kwenye sheria gani? Ama tusiseme mtoto, kijana wa miaka 18 anahesabika ni mtoto akibaka? Kuna uhalisia hapo? Hebu naona Mwanasheria mwingine anataka kutusaidia hapo.
Mheshimiwa Patrobass Katambi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo ninadhani kuna mkanganyiko ambao ameufanya. Kilichofanyika, mwenye umri wa miaka 18 anatambulika ni mtu mzima kwa sheria tulizonazo, hata zile tulizobadilisha huwa tuna Young Persons Act pia kuna Age of the Majority, lakini katika msingi huo wa miaka 18 aliousema, kama angefafanua vizuri ni kwamba mwaka 1998 ilitungwa ile Sexual Offenses Special Provisions Act, ambayo iliingiza hata mtoto wa shule ya msingi au sekondari mwenye umri wa miaka 18 ili mradi kwamba ni mwanafunzi with or without consent akiwa kwenye mahusiano, kosa litatambulika kwamba ni ubakaji. Kwa hiyo, ile ndio muktadha ule wa miaka 18, lakini mpaka sasa sheria inatambua miaka 18 ni mtu mzima. Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Sawa, ile siyo hii sheria uliyoitaja ni sheria inayohusu elimu ndiyo tuliibadilishia huko. Sasa, hata kule yaani kosa analokuwa amefanya ni kosa la huku kwingine, sasa mtu ana miaka 23 yupo kule unasema kwa kuwa ni mwanafunzi hawezi kubaka. Kule hatukusema mambo ya kubaka. Ninakumbuka wakati wa kutunga ile sheria, hatukuzungumzia mambo ya amefanya kosa la jinai, ameua, amefanya nini hata kama ni mwanafunzi, lakini ana umri huo anahukumiwa kwa kosa la huku. Kosa tu linaloingia kule ni lile la kwamba, yeye kwenye ndoa na nini, yaani vitu kama hivyo, lakini haya mengine haya sikumbuki tumeweka wapi hapo mahali ambapo tunamwona mtu wa miaka 18 kwamba ni mtoto, akibaka anachapwa viboko.
Ninadhani hilo tulitazame kwa pamoja, kama hatuna hicho kifungu tukatazame vizuri kama kuna mahali kuna changamoto tuirekebishe, kwa sababu itakuwa siyo sawa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, haipo katika sheria zetu. Juzuu zote 441 haipo.
SPIKA: Sawa. Kwa sababu bado tupo kwenye kipindi chetu cha maswali na majibu na hapa Mbunge anasisitiza ipo, ngoja ajaribu kutazama atakaponiletea hapa tutatoa ufafanuzi vizuri ili wote tuwe tumeelewana vizuri. Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wewe utazame na Mheshimiwa Naibu Waziri na wewe ukatazame, Mbunge na yeye anatazama. Nitaletewa hapa mbele tutaoa ufafanuzi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Waziri tunakushukuru sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved