Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Josephine Johnson Genzabuke
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:- Je, lini Serikali itafika katika Kata ya Kagerankanda kutatua mgogoro wa mpaka baina ya vijiji na TFS?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, wananchi wa Vijiji vya Mvugwe, Makere, Kitagata, Nyachenda, Nyamidaho, Mugombe na Nyakitonto na kata nyingine ambazo sikuzitaja zimezunguka Hifadhi ya Makere Kusini na kwa sasa wananchi hao wanazuiliwa kuvuna mazao yao; je, Serikali iko tayari kuiagiza TFS na watu wa Kitalu cha Kagerankanda kilichopo Kabulanzwili ili wananchi waweze kuvuna mazao yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kati ya ekari 10,000 zilizotolewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli ni vijiji viwili tu vilivyoweza kupata ambapo ekari 2,496 ziligaiwa Kijiji cha Kagerankanda na Kijiji cha Mvinza kilipata hekta 2,174, lakini ekari hizo 5,000 zilizobaki zimechukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Vijiji vyote hivyo nilivyovitaja kwa maana ya Mvugwe, Makere, Kitagata, Nyachenda, Mugombe, Nyakitonto, Nyamyusi na Kulugongo vyote vinategemea hifadhi hiyo ya Makere.
Je, Serikali iko tayari kukaa na Wizara ya TAMISEMI ili hizo hekta 5,000 zilizochukuliwa na Halmashauri ya Kasulu DC zirudishwe kwa wananchi wa vijiji hivyo niulivyovitaja?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Genzabuke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili la wananchi kulima kwenye hifadhi limekuwa likiendelea kwa muda mrefu, lakini vilevile tulipata maombi ya Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma na Kagera tulipokaa nao kwamba yale maeneo ambayo wananchi wamelima kwenye hifadhi waruhusiwe kuvuna mazao yao, lakini wasiruhusiwe kulima tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekwishatoa maelekezo kwa wahifadhi wetu wa maeneo haya kwamba wananchi waliolima kwenye hifadhi waruhusiwe kuvuna mazao yao, lakini wasiruhusiwe kuendelea kupanda kwenye hifadhi hizi. Ninawakumbusha wahifadhi wetu agizo hili bado linasimama na sasa Serikali au Wizara tutafuatilia wahifadhi wetu wote ambao hawajatekeleza agizo hili na hatutasita kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, wakati tulipopata maelekezo ya kumega ardhi kwa vijiji hivi, vilevile tulipewa maelekezo ya kutenga eneo kwa ajili ya halmashauri kwa shughuli za uwekezaji, lakini vilevile kuwa akiba endapo yatatokea mahitaji ya ziada, wananchi waweze kupewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu eneo hili sasa hizi hekta 5,000, zinamilikiwa kisheria na halmashauri, tutaendelea kuwasiliana na wenzetu wa halmashauri kuona namna bora ya ardhi hii kutumika kwa mujibu wa sheria kwa sababu halmashauri hii wananchi hawa ni wananchi wake. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved