Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kudhibiti ukuaji wa makazi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangwa kuwa makazi ya wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mpango huu ambao Serikali inauita KKK, ilikuwa ni programu ambayo Serikali imetoa pesa nyingi, lakini inavyoonekana hakuna ufuatiliaji mkubwa wa pesa hizi kiasi kwamba kwenye halmashauri zetu miradi hii haifanyiki kwa ufanisi. Je, Serikali ina mpango gani mahsusi kuhakikisha kwamba miradi hii inakwenda kutekelezwa kwa wakati? Ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wananchi wa Kata ya Pugu Jimbo la Ukonga wako katika mpango huu na wengi wameshalipa pesa takribani shilingi 250,000/= kwa kila kaya, lakini mpaka sasa mpango ule umesimama. Ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wale wanarasimishiwa ardhi yao?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwanza la KKK, ni kweli Serikali hasa hii Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka fedha nyingi sana katika mradi huu wa KKK. Tulishirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI na fedha hii ikaenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilichagua wao maeneo ambayo walitaka kuyapanga, kuyapima na kumilikisha. Sasa, fedha hii kuna maeneo ninakiri kwamba ilienda na badala ya kutumia fedha hii kwa ajili ya kupima, kupanga na kumilikisha, walipeleka fedha hii kwenye shughuli nyingine. Hata hivyo, kwa sasa ninawasifu na kuwapongeza wenzetu wa TAMISEMI, wamekuwa wakishirikiana nasi kwa karibu sana, vilevile kupitia Kamati ya Bunge ya TAMISEMI katika kuhakikisha halmashauri zinarejesha fedha hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali la pili la Pugu – Ukonga, Manispaa au Jiji la Dar es Salaam ambayo ni Ilala iliingia mkataba na kampuni za urasimishaji ambapo kampuni hiyo ilienda, ilichukua fedha kwa wananchi lakini hawakukamilisha kazi ile. Ninampa taarifa tu Mheshimiwa Shangazi kwamba Wizara sasa imeona tuingilie hili kuhakikisha kwamba wananchi wale waliotoa fedha yao, wanapata ule urasimishaji walioutarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunafanya kazi kwa karibu sana na Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha kwamba tunawapa wananchi hawa urasimishaji waliokuwa wanautarajia. Niseme tu mwishoni, kwamba vilevile tumeanza kufanya audit ya hizi kampuni zote za urasimishaji ili tuweze kuona uwezo wao wa kutekeleza majukumu ambayo wanaenda kuyaomba kule kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini.

Name

Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kudhibiti ukuaji wa makazi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangwa kuwa makazi ya wananchi?

Supplementary Question 2

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kule Musoma kwenye hili zoezi la urasimishaji unakuta watu waliotarajiwa kupimiwa kwenye hilo eneo labda walipaswa kuchanga watu 100 na kila mmoja akachanga labda shilingi 150,000/=, lakini kati ya hao, wamechanga nusu na nusu wengine hawakuchanga na kutokana na hali hiyo yale maeneo yameshindwa kupimwa, lakini na wale waliokwishachanga fedha zao zimekaa kule…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: … tunawasaidiaje watu kama hao?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishasema wakati najibu swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi na kwa Mheshimiwa Manyinyi kule kunafanana, kwamba ni zile kampuni ambazo ziliingia makubaliano na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwenye kesi ya Mheshimiwa Manyinyi ina maana na Manispaa ya Musoma ndizo ambazo zilileta changamoto hizi kwa wananchi. Kwa hiyo ndiyo maana tunaangalia upya utaratibu wa kampuni hizo kufanya kazi katika urasimishaji kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini na baada ya hapo ninaamini changamoto hizi zitaisha.

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kudhibiti ukuaji wa makazi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangwa kuwa makazi ya wananchi?

Supplementary Question 3

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Hivi ni kwa nini Makao Makuu kwa mfano hapa Dodoma wananchi bado wanafanya ujenzi holela wakati hapa ndiyo uso wa nchi na ni makao ya nchi?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, narejea kwenye majibu yangu ya msingi nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tendega kwamba sasa Wizara tunahakikisha tunafanya kazi kwa karibu sana na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuhakikisha tunapanga, tunapima na kumilikisha. Tunawasisitiza sana wenzetu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha watu wanaojenga wawe na vibali vya ujenzi. Vibali vile vinatokana na maeneo ambayo yameshapimwa na kurasimishwa kwa hiyo tunaendelea kufanya kazi kwa karibu sana na wenzetu wa Mkoa wa Dodoma na Jiji la Dodoma kuhakikisha kwamba changamoto hizi sasa zinaendakwisha kabisa.