Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga fedha za Ujenzi wa Barabara ya Makofia - Mlandizi - Mzenga hadi Maneromango kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, ni mara ya kwanza kwa Barabara hii ya Makofia – Mlandizi – Maneromango kupata jibu la matumaini kwamba, awamu hii ya sita imeanza kutekeleza ujenzi wake kwa kipande cha kilomita 23.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ninataka niulize kwa kuwa, katika barabara hii vipo vijiji kwa mfano, Kijiji cha Matimbwa na Yombo, wananchi walifanyiwa tathmini, kwa ajili ya kulipwa fidia. Je, Serikali haioni haja sasa ya wananchi walio kando ya barabara hii, wakiwemo wa Vijiji vya Matimbwa na Yombo, kulipwa fidia wakati Serikali ikitafuta fedha za ujenzi wa kipande kilichobaki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kwa kuwa, wakati wanawasilisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi walitupa matumaini Wakazi wa Bagamoyo juu ya ujenzi wa Daraja la Mpiji Chini na kwamba, watamsimamia mkandarasi, ili aendelee na kazi. Je, Serikali ipo tayari kutimiza ile ahadi yao ya kupandisha hadhi kipande cha Barabara ya Mingoyi – Kiembeni inayounganishwa na Daraja hili la Mpiji Chini ili kuwarahisishia Wakazi wa Bagamoyo na Kinondoni, kwa ajili ya mawasiliano? Naomba kuwasilisha na ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua jitihada za Serikali. Namhakikishia kwamba, suala hili tunalifanya haraka sana kwa sababu ni barabara ambayo inaenda kuunganisha Mji wa Mlandizi pamoja na Kituo cha SGR na tayari tupo kwenye hatua za mwisho kabisa za manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, tayari tulishawasilisha jedwali ambalo limehahakikiwa na lipo Hazina likisubiri tu fedha itoke tuweze kuwalipa wananchi hawa ambao watapisha ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Daraja la Mpiji Chini; ni kweli kwamba, daraja hili lilishapata mkandarasi. Mimi binafsi nimeenda, lakini pia, Waziri ameenda pale na kutoa maelekezo ni nini mkandarasi aweze kufanya. Katika mito ambayo ilipanuka sana ni pamoja na eneo hili ambalo mkandarasi alikuwa analijenga kwa hiyo, kuna haja ya kufanya mapitio upya ya usanifu uliokuwa umefanyika kwa sababu, daraja hili limeongezeka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupandisha hadhi barabara aliyoitaja; namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, taratibu zipo, tunasubiri maombi kutoka Mkoa ambayo tathmini itafanyika na wataalam wetu mara tutakapopata maombi rasmi ya kupata Mkoa kama taratibu zilivyo. Ahsante. (Makofi)

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga fedha za Ujenzi wa Barabara ya Makofia - Mlandizi - Mzenga hadi Maneromango kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, kabisa naanza kuipongeza Serikali kwa kuanza kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa kilomita mbili kwenye Mji wetu wa Kharumwa ambapo sasa hivi kilomita moja inaenda kukamilika ndani ya wiki hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na ahadi pia, ya kufungiwa taa. Je, ni lini Serikali, baada ya kukamilisha hii kilomita moja, itaanza kufunga taa na kuanza ujenzi wa kilomita ile nyingine? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema kwenye bajeti, Kharumwa ni Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale na mpango ni kuhakikisha kwamba, miji yote na hasa kwa kuwa, tumejenga lami nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuna mpango wa kufunga taa karibu katika Wilaya zote, Makao Makuu ya Wilaya, ukiwepo na Mji wa Kharumwa, ahsante. (Makofi)

Name

Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga fedha za Ujenzi wa Barabara ya Makofia - Mlandizi - Mzenga hadi Maneromango kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 3

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia kilomita 35 Barabara ya Uchumi iliyoanzia Ziwani – Madimba – Msimbati kwa kiwango cha lami ambako kuna mitambo na visima vya gesi? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, barabara aliyoitaja ndiyo inaenda kwenye visima vyetu vya gesi kilomita 35 na kama atakuwa ameona, bajeti tumepitisha na ipo kwenye mpango kuanza kuijenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami katika mwaka unaokuja wa fedha. Ahsante. (Makofi)

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:- Je, lini Serikali itatenga fedha za Ujenzi wa Barabara ya Makofia - Mlandizi - Mzenga hadi Maneromango kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 4

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, ujenzi wa Barabara ya Mnivata – Newala hadi Masasi umeshaanza; na Kwa kuwa, ujenzi huu una miradi ya kijamiii ambayo mkandarasi anatakiwa aijenge kama CSR. Je, ni lini miradi hiyo ya kijamii itaanza kujengwa?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi huu ambao unafadhiliwa na African Development Bank, una miradi ambayo tunaita complementary projects. Miradi hii inajengwa tutakapokuwa tumekamilisha taratibu zote, ikiwa ni pamoja na usanifu na kuhakikisha kwamba, itasimamiwaje. Kwa kawaida, labda kama kuna changamoto, inatakiwa iende sambamba na ujenzi wa barabara yenyewe, lakini kama kuna changamoto kuanza. Basi naomba nikutane na Mheshimiwa Mbunge, ili tuone kama kuna mkwamo sehemu yoyote, basi tuweze kuikwamua kwa sababu, fedha hiyo ipo. Ahsante. (Makofi/Kicheko)