Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Primary Question
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:- Mafunzo na mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na Chuo cha Polisi (CCP) katika eneo la Kata ya Donyomorwa katika Wilaya ya Siha yamesababisha maafa makubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wananchi kuuawa kwa risasi na mabomu yanayotumika katika mazoezi hayo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamisha mafunzo hayo kutoka kwenye maeneo ya makazi ili kuepusha maafa yanayowapata wananchi wa maeneo hayo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ieleweke kuwa wananchi wa Siha siyo kwamba wanachukia polisi kuwepo katika eneo hilo lakini kilichoonekana ni kwamba watu wameongezeka sana katika eneo hili na ushahidi upo kwamba wameshakufa watoto wanne na tarehe 18/08/2016 kuna mtoto ambaye risasi ilimfuata nyumbani na mpaka sasa ana ulemavu. Maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isione ni busara sasa na ni wakati muafaka ikafuata ushauri wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Siha ya kwamba mazoezi ya polisi yapelekwe katika eneo la heka 500 ndani ya NARCO lakini hilo eneo likagawanywa katika sehemu tatu? Sehemu ya kwanza ni kutoa eneo ambalo litasaidia kupunguza ukata wa ardhi kwa wananchi wa Siha hasa walioko upande wa milimani, sehemu ya pili ikatolewa kwa ajili ya kufanya utalii wa kimila. Kama mnavyokumbuka mwaka huu Waziri wa Utamadumi alikuja pale na alifanya tukio kubwa ambalo linafanyika East Africa yote kwa ajili ya utalii. Kwa hiyo, Wizara ya Utamaduni na Idara ya Mambo ya Kale ikakabidhiwa chini ya Halmashauri eneo lingine kwa ajili ya kufanya utalii wa kimila. Eneo linalobaki tukajenga Chuo Kikuu cha Polisi badala ya kufanyia mazoezi yanayowaathiri wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba…
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Huwa sichanganyikiwi mkiongea sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, wananchi walioumia na huyu mtoto aliyepata ulemavu Serikali iko tayari kutoa fidia lakini vilevile Waziri kutembelea kuwaona waathirika?
Name
Charles Muhangwa Kitwanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo alilopendekeza ametaja kwamba ni eneo la NARCO na NARCO iko chini ya Wizara nyingine na Wizara husika wana mpango wa matumizi wa eneo hilo. Ninachotambua ni kwamba ni kweli Wilaya ya Siha pamoja na Mkoa mzima wa Kilimanjaro una matatizo makubwa ya ardhi. Mkoa pamoja na Wilaya kwa kushirikisha Wizara ya Ardhi mara kwa mara wamekuwa wakiangalia mpango bora wa matumizi ya ardhi na sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ni sehemu ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata eneo. Hata hivyo, kwa sasa yale niliyoyasema kwenye jibu la msingi yanasimama kwa maana tunatarajia kupima eneo lile ambalo linatumika kwa ajili ya mafunzo, kuweka alama na wananchi hawa waweze kutafutiwa maeneo mbadala ambapo mazungumzo yameendelea katika maeneo tofauti na Waziri wa Ardhi alishafika kule kuweza kuangalia njia bora ya kuwapatia vijana maeneo ya ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili ambalo amelisemea la kijana aliyeumia, kwa niaba ya Wizara na Serikali nitoe pole na tumepokea hayo ambayo ameyasema kama mapendekezo. Tutaongea na wataalam tuone ni kitu gani wamekuwa wakifanya punde yanapotokea mambo ya aina hiyo.
Name
Juma Selemani Nkamia
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Primary Question
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:- Mafunzo na mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na Chuo cha Polisi (CCP) katika eneo la Kata ya Donyomorwa katika Wilaya ya Siha yamesababisha maafa makubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wananchi kuuawa kwa risasi na mabomu yanayotumika katika mazoezi hayo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamisha mafunzo hayo kutoka kwenye maeneo ya makazi ili kuepusha maafa yanayowapata wananchi wa maeneo hayo?
Supplementary Question 2
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la usalama ni jambo la msingi sana kwa raia wa Tanzania, kumekuwa na matukio mengi sana ya watu kupigwa na wengine kuuawa katika mpaka wa Kiteto na Chemba. Polisi wa eneo hili hasa wale wa Wilaya ya Chemba walioko Mrijo wanashindwa kufuatilia matukio haya kutokana na ukosefu wa vifaa ikiwemo magari, wengi wanaazima pikipiki na wakati mwingine baiskeli. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vifaa vinapatikana katika maeneo ambayo kuna matatizo kama haya ili kunusuru wananchi na mali zao?
Name
Charles Muhangwa Kitwanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Nkamia kwa kulisema jambo hili na niwahakikishie tu wananchi wa Chemba kwamba Mheshimiwa Nkamia amekuwa akifuatilia sana suala hili. Ameshakuja mara kadhaa ofisini na mimi nimemuahidi kwamba tutakapopata magari kwa ajili ya Wilaya mpya na Wilaya Chemba tutaipa kipaumbele zikiwepo na Wilaya nyingine kama Mkalama ambapo Mheshimiwa Allan Kiula naye amekuwa akisumbua mara kwa mara. (Makofi)
Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Nkamia suala la magari pamoja na nyumba za askari katika Wilaya yake mpya tutalipa kipaumbele kwa kutambua mazingira tete ya eneo hilo ambapo pana changamoto za kugombania matumizi ya ardhi ambayo yanahitaji sana askari kuwepo katika maeneo hayo. Nitoe rai kwa wananchi wa maeneo husika watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi punde mtu mmoja anapokuwa amekiuka sheria katika maeneo husika ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Name
Maryam Salum Msabaha
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:- Mafunzo na mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na Chuo cha Polisi (CCP) katika eneo la Kata ya Donyomorwa katika Wilaya ya Siha yamesababisha maafa makubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na wananchi kuuawa kwa risasi na mabomu yanayotumika katika mazoezi hayo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamisha mafunzo hayo kutoka kwenye maeneo ya makazi ili kuepusha maafa yanayowapata wananchi wa maeneo hayo?
Supplementary Question 3
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zama hizi tumeona askari wakifanya mazoezi katika barabara wakiwa na silaha za moto na kwa mujibu wa sheria vikosi vyote vya ulinzi na usalama wana maeneo yao maalum ya kufanyia mazoezi. Je, Serikali haioni kwamba wanawapa maadui nafasi kuona udhaifu wa askari wetu na kuingiza maadui kupambana na vyombo vya ulinzi na usalama? Ni kwa nini vyombo hivi visibaki sehemu zao za kufanyia mazoezi huko huko vilikopangiwa?
Name
Charles Muhangwa Kitwanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza vikosi vya ulinzi na usalama kufanya mazoezi ni sehemu ya maisha yao…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Na kila siku kwao ni mazoezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili alilosema kwamba kufanya mazoezi barabarani wanawafanya maadui wajue udhaifu wao, nimwambie tu mazoezi yale wanayofanyia barabarani ni ya viuongo na ni sehemu tu ndogo kati ya yale mazoezi makubwa wanayofanya ya kukabiliana na wahalifu. Na mimi niseme tu kwamba kwa mwananchi yeyote ambaye havunji sheria hana haja ya kushtuka anapoona askari wanafanya mazoezi. Wanafanya mazoezi hayo kwa ajili ya wahalifu, kwa hiyo, kama siyo mhalifu huna haja ya kuwa na mashaka.