Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini TARURA itaanza ujenzi wa barabara ya Vwawa- Iganduka hadi Isalalo kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 1
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa, majibu yanasema kwamba Serikali itajenga kipande cha kilomita mbili kwa awamu ya kwanza na eneo kubwa ambalo limekuwa na usumbufu mkubwa ni kuanzia Hasanga – London mpaka Mto Nkana, je, Serikali itakuwa tayari katika hii awamu ya kwanza kuongeza kilomita tatu zaidi ili zifikie tano, kusudi lile eneo ambalo lina shida liweze kupitika? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa katika barabara hii kutoka Vwawa – Isalalo haitakuwa chini ya mpango huu ambao unausema kuna kilomita zitabaki nje. Je, Serikali itakuwa tayari kutafuta chanzo kingine cha fedha ili kuhakikisha kwamba hii barabara ambayo ni kiungo muhimu inakamilika hadi Isalalo? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi wa wapigakura wake. Naomba nijibu maswali yote mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, nimemweleza Mheshimiwa Mbunge, Japhet Hasunga kwamba Serikali kupitia mradi huu maalum kabisa wa TACTIC utajenga kilomita mbili kwa kiwango cha lami katika jimbo lake, kwa sababu wao kama Vwawa wapo katika kundi la tatu la miradi hii ya TACTIC, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunaanza na kilomita mbili ambazo tayari zimeshawekwa katika utaratibu, zinafanyiwa usanifu na zitajengwa kwa kiwango cha lami. Lengo na madhumuni ni kuendelea kuongeza mtandao wa lami ili uweze kufika katika maeneo mengi zaidi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ukiacha tu huu mradi wa TACTIC ambao unatekeleza ujenzi wa hizi barabara za lami katika Jimbo lake, bado kuna fedha na bajeti ya TARURA ambayo inakuja kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, ameongeza bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 275 kwa mwaka mpaka sasa ni shilingi bilioni 710 kwa mwaka. Kwa hiyo, fedha zinazidi kuongezeka kwa ajili ya kuhakikisha maeneo mengi zaidi yanafikiwa na barabara zetu zinajengwa kwa viwango ambavyo vitawezesha kupitika kwa mwaka mzima. (Makofi)
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini TARURA itaanza ujenzi wa barabara ya Vwawa- Iganduka hadi Isalalo kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 2
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya kutoka Ilula – Ibumu ipo katika mpango wa RISE wa kujengwa kwa lami kilomita 28. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu mkubwa sana wa hizi barabara zetu za Wilaya kiuchumi, pia kufikia huduma msingi kabisa za kijamii, inaendelea kuhakikisha kwamba inaongeza bajeti na inafikia maeneo mengi zaidi kwa ajili ya kujenga na kuimarisha miundombinu ya barabara hizi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kupitia huu mradi wa RISE, barabara hii ya Ilula – Ibumu yenye kilomita 28 itajengwa. Serikali inaendelea na taratibu zake na zitakapokamilika Mkandarasi atakabidhiwa site ili aweze kuanza ujenzi.
Name
Josephine Johnson Genzabuke
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini TARURA itaanza ujenzi wa barabara ya Vwawa- Iganduka hadi Isalalo kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Mgombe – Kagera Nkanda, ni barabara inayotumiwa na wakulima kwenda mashambani, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha barabara hiyo imeharibika vibaya mno. Je, Serikali iko tayari kuitengeneza barabara hiyo kwa udharura? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri sana. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua barabara zetu hizi za Wilaya zina umuhimu mkubwa sana wa kiuchumi, lakini zinawawezesha wananchi kufikia huduma muhimu za kijamii. Ndiyo maana Serikali inafanya jitihada dhahiri shahiri kabisa kuongeza bajeti na kufikia maeneo mengi zaidi kwa ajili ya kwenda kuimarisha mindombinu ya barabara.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali kwa kutambua uharibifu mkubwa uliotokea kwenye barabara zetu ambao umetokana na mvua za El-Nino mpaka muda huu imeshatumia gharama za shilingi bilioni 88 kwa ajili ya kufikia maeneo korofi yaliyo katika mawasiliano na kuweza kurudisha mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha inafika katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo hili ulilolitaja la Kagera Nkanda ili kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa na wananchi wanaweza kuitumia.
Name
Venant Daud Protas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini TARURA itaanza ujenzi wa barabara ya Vwawa- Iganduka hadi Isalalo kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 4
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TARURA ilisaini mikataba mingi mwezi wa Tisa, mwezi wa Saba mpaka leo wakandarasi hawapo site. Je, Serikali ina mpango gani kuwarudisha wakandarasi ili waendelee na ujenzi wa barabara kwa mikataba mliyosaini, hasa Jimbo la Igalula na barabara nyingi zimekufa? Ahsante. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa hili swali lake zuri kabisa kwa manufaa ya wapigakura wake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imekuwa ikipokea fedha kutoka Wizara ya Fedha kuja TARURA kwa ajili ya kuwafikia wakandarasi na kuhakikisha wanapata malipo na kuanza ujenzi wa barabara hizi.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, inawapatia fedha hawa wakandarasi na inahakikisha kwamba wanafika site kwa ajili ya kuanza kazi za ujenzi. Nimhakikishie hata kwenye Jimbo lake atawaona wakandarasi wanafika site, wanaanza kufanya kazi. Serikali inasimamia kuhakikisha hilo linafanyika.
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Primary Question
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: - Je, ni lini TARURA itaanza ujenzi wa barabara ya Vwawa- Iganduka hadi Isalalo kwa kiwango cha lami?
Supplementary Question 5
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri, TARURA katika Mji wa Babati hawajapewa fedha tangu mwaka 2024 na barabara ni mbovu sana. Ni lini TARURA watapewa fedha hizo waanze kutengeneza barabara? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Pauline Gekul kwa swali hili zuri kabisa lenye lengo la kuhakikisha kwamba wapigakura wake wanapata miundombinu bora kabisa ya barabara zetu hizi za Wilaya. Naomba nimhakikishie kwamba, Serikali italeta fedha kuhakikisha kwamba bajeti ya ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya barabara katika Jimbo lake inapatikana.