Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuinua lugha ya Kiswahili kupitia vyombo vyake vya habari vya kitaifa?

Supplementary Question 1

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu sawia, majibu mwanana. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti nyingi zinazohusu masuala ya kawaida ya Watanzania zinafanyika kwa lugha ya kigeni hasa Kiingereza. Je, Serikali mpaka sasa haioni umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili kwa kuelekeza kupata tafsiri katika lugha hii adhimu katika utafiti wa kisayansi na maendeleo ya kiteknolojia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Je, Serikali kupitia mamlaka husika za ustawishaji wa lugha ya Kiswahili imeweza kujifunza nini kutoka mataifa mengine ulimwenguni ambayo yamefanikiwa kutumia lugha zao rasmi za kitaifa?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Asha Abdullah Juma maarufu kama Bi. Mshua kwa uzalendo na mapenzi ya dhati. Maana haya siyo mapenzi tu, ni mahaba ya dhati kwa lugha ya Kiswahili. Sisi wapenzi wenzako wa Kiswahili akiwemo ndugu yangu Ahmed Ally na Mkandaji Kibu Dennis tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kujibu maswali yake, hoja aliyoleta Bi Mshua ni ya msingi sana na kasi ya mabadiliko ya kidunia inapaswa kuwafikia Watanzania kwa lugha waliyoizoea ambayo ni lugha ya Kiswahili. Kwa kufahamu hilo, Baraza la Kiswahili la Taifa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar wameandaa na kusanifu msamiati wa utafiti kwenye sayansi na teknolojia kwa lugha ya Kiswahili na machapisho kadhaa yameshatengenezwa kwa lugha hiyo, yakiwemo machapisho ya Kamusi ya awali ya sayansi na teknolojia. Halikadhalika, kuna Kamusi ya Fizikia, Kemia, Biolojia, Kamusi ya Kompyuta na machapisho mengine kadha wa kadha.

Mheshimiwa Naibu Spika, fauka na hayo, machapisho mengine katika nyanja husika yametengenezwa kwa Kiswahili na sasa hivi jitihada ya Serikali inayoifanya ni kuhakikisha tunawashawishi watafiti kufanya tafiti zinazofuata kwa lugha ya Kiswahili na kutafsiri tafiti ambazo walishazifanya kwa lugha nyingine kwa lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu tulichojifunza ni muhimu kuwa na vyombo imara na mahsusi kwa ajili ya kusimamia lugha. Hivyo, Serikali imeongeza uwekezaji kwenye Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar ili kuviimarisha vyombo hivi na kuhakikisha lugha ya Kiswahili inasimamiwa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwekezaji unaofanywa, yamefanya mambo mengi yakiwemo makongamano nje ya nchi kujaribu kukieneza Kiswahili na kukipa hadhi inayostahili. Pia, tumejifunza kuhusu umuhimu wa kusambaza lugha kwa kutumia mifumo ya kidigitali, kwa vile dunia sasa imebadilika na mifumo ya kidigitali ndiyo hasa inayotumika kueneza mambo mbalimbali ambayo yanatakiwa kwenda kwa kasi duniani, ahsante sana. (Makofi)