Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Primary Question

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:- Je ni lini Tanzania itaridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kujikinga na Bidhaa za Nyuklia?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza pamoja na shukrani kwa jibu zuri. Swali la kwanza; swali langu lilihusu Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Vitendo vya Kigaidi kwa kutumia Nyuklia (International Convention for the Suppression of Acts of Nuclear Terrorism). Sasa jibu limehusu Mkataba wa Kimataifa wa Kujikinga na Bidhaa za Nyuklia. Je, wana maana hiyo hiyo au ni mkataba mwingine tofauti?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama jibu ni ndiyo, je, mnafahamu kwamba tukijiunga na mkataba huo wa kuzuia vitendo vya kigaidi kwa kutumia nyuklia (ICSANT), hakuna malipo yoyote ya mwanzo wala ya kila mwaka...

SPIKA: Mheshimiwa Sanga, keti kwanza. Malizia swali lako la pili.

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama jibu la swali la kwanza ni ndiyo, je, Serikali inafahamu kwamba tukijiunga na huu mkataba wa Kimataifa wa kuzuia vitendo vya kigaidi kwa kutumia nyuklia, hakuna malipo yoyote ya mwanzo au ya kuendelea na kila mwaka (initially). (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Rweikiza, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ameuliza kuhusiana na swali lake na jinsi ambavyo tumelijibu kama ni sahihi. Kujikinga na kutokomeza, yote ni katika tafsiri na mikataba hii ya kimataifa iko katika maeneo matatu. Moja, upo mkataba wa kimataifa unaozuia kugandamiza vitendo vya kigaidi, huo ni wa mwaka 2005, lakini pia tunao mkataba wa kimataifa unaohusiana na masuala ya kutokomeza silaha za kinyuklia wa mwaka 2021. Yote hii inalenga katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na matumizi sahihi ya nyuklia pamoja na matumizi salama ya nyuklia duniani.

Mheshimiwa Spika, katika ile mikataba ni crosscutting kwa maana kwamba inahusianisha pia Wizara nyingi, Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Elimu, kwa maana kwamba sisi tuna tume maalum ambayo ni Tume ya Nguvu za Atomu. Ambapo kwa pamoja waliweza kufanya kazi kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu, kuweza kuhakikisha kwamba tunaingia kwenye mkataba huo tukiwa tunatambua kwamba utakuwa salama na utaleta matumizi sahihi ya kinyuklia.

Mheshimiwa Spika, tunatambua sisi tunayo uranium hapa nchini, hatua ambazo tumekwisha kuzifikia katika kuipembua mikataba yote hiyo ile ambayo inatengeneza bidhaa za madawa, silaha au kemikali zinazoweza kuleta athari, yote hii tunaipitisha katika chujio la kuanza kwanza na hatua ya kupitiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili ni kuwa na maoni ya wadau mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya hizo nyuklia na hatua ya tatu ni kupeleka katika Kamati ya Baraza la Mawaziri kwa ajili ya ushauri na baadaye mapendekezo hayo yataletwa Bungeni na kama itapendeza basi Bunge hili litaweza kusaini na kuridhia mikataba hiyo ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili aliuliza kuhusiana na kwamba, Serikali inatambua kuwa ni bure. Ni kweli mikataba mingi ambayo inahusianisha United Nations Council hasa Security Council, inayoleta matumizi ya kemikali hasa zile ambazo zinaweza zikaathiri aidha usalama au uhai wa wanadamu, kwa mara nyingi imekuwa ni jitihada ya Umoja wa Mataifa pamoja na nchi wanachama kuweza kuhakikisha kwamba wanachama hawaingii kwenye gharama au tozo ili kuweza kuhakikisha kwamba dunia inakuwa sehemu salama.

Mheshimiwa Spika, ninatambua kwamba Mheshimiwa Rweikiza ni Member wa Parliamentary for Global Action, nafahamu kwenye vikao vyao wanayajadili haya. Kwa hiyo, tunatambua hilo na ndiyo maana tunapitisha mchakato sahihi wa Serikali ili tukiridhia tuweze kuwa na faida na tija kwa ajili ya Taifa letu. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Rweikiza, huu Mkataba wa International Convention for the Suppression of Acts of Nuclear Terrorism, ni wa mwaka gani?
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, mkataba huu ni wa mwaka 1971.

SPIKA: 1931!

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, 1971.

SPIKA: 1971?

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, najua haya majibu yametayarishwa na Wizara ya Elimu, sasa wao wametaja mkataba tofauti na ule ambao Mheshimiwa Mbunge ameuliza. Kwa sababu yeye ameuliza International Convention for the Suppression of Acts of Nuclear Terrorism wa 1971. Humu kwenye majibu kunaonekana mkataba uliotajwa ni mwingine.

Kwa hiyo, ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge alikuwa anauliza ni wenyewe au siyo wenyewe. Kwa hiyo, kwa bei ya jina, mkataba ni tofauti na kama yote inalenga kitu kimoja, sidhani kama ingetengenezwa miwili halafu yote inatoka sehemu moja, labda kama huu mwingine umekuja kwa ajili ya kujazia ule mwingine, lakini Mheshimiwa Mbunge alipaswa ajibiwe kwa mkataba ule ambao yeye ameuulizia.

Kwa hiyo, kwa sababu hili jibu limetayarishwa na Wizara nyingine, ninashindwa kukuuliza wewe maswali mengine. Ninaona unataka kusema jambo?

Nataka niwarejeshee ili wamjibu Mheshimiwa Mbunge swali ambalo yeye ameuliza. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kimsingi kilichojibiwa hapa na Wizara kwa kutumia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ushirikiano na Tume ya Nguvu Kazi za Atomu, ambayo ilifanya kwa pamoja kwa ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Kiatomu, majibu yaliyotolewa hapa ni yale ya ujumla ya mikataba yote inayohusiana na masuala ya kinyuklia, ambayo...

SPIKA: Yeye ameuliza wa kwake maalum, ndiyo maana alikuwa anauliza lile swali la kwanza. Kwa sababu yeye ameulizia mkataba fulani; yeye hataki yale ya jumla, nyuklia na nini, yeye anataka wa kwake ujibiwe. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, itakuwa ni context ya swali, lakini bado haidhuru pia, tuko tayari kulijibu kwa jinsi ambavyo utaona inapendeza. Ahsante.

SPIKA: Aaah, kwa hiyo, uko tayari kumjibu hapa au niwarejeshee ili wakalete majibu ya Mbunge?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ninadhani swali liwe customized ili tuweze kujua specific ili kuwa na majibu sahihi ambayo yanaendana na hilo. Kwa hiyo, tuko tayari kulipokea kwa ajili ya marekebisho.

SPIKA: Sawa Mheshimiwa, ahsante sana.

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza litajibiwa upya na Serikali ili liweze kujibu kile ambacho Mheshimiwa Mbunge alikuwa ameuliza. Pia, kwa sababu hii ndiyo Wizara ya Elimu, kwa kweli tunapaswa kujielimisha na kwenye mambo mengine.

Hiki Kiswahili cha “Mkataba huo umeshawasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kufanyiwa Uridhiwaji”, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hairidhii mikataba. Kwa hiyo, ukileta jibu kama hili na hii ndiyo Wizara ya Elimu, kidogo inaleta mtihani.

Haya maneno hapa mwisho ya kufanyiwa uridhiwaji, kwanza hicho Kiswahili sijakielewa, sijui kitenzi ni kipi, sijui kipi ni kipi? Tunaelekea kwenye Kiswahili fasaha jamani. Kufanyiwa uridhiwaji, aah Hapana! Siyo Kiswahili sanifu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwenye swali lako 132, majibu yataletwa mapya. Watakapokuwa tayari watatuletea na tutalipanga kama utaratibu ulivyo. (Makofi)