Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:- Ofisi nyingi za Balozi zetu katika nchi mbalimbali zimekodishwa. Aidha, ofisi nyingine ujenzi haujakamilika au hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu sasa na ofisi nyingine zina madeni makubwa. (a) Je, ni lini ujenzi wa baadhi ya ofisi za Ubalozi zitakamilika ikiwemo ya Msumbiji? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati ofisi chache za Ubalozi zilizopo pamoja na kununua samani mpya? (c) Je, kwa nini Serikali isilipe madeni ya Balozi zetu kwa wakati ili kuepusha aibu kwa Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, kumekuwa na utaratibu wa Watanzania wanaofariki nje ya nchi, ndugu zao wanaokuwepo hapa nchini hupata taabu, adha na kucheleweshwa kuletewa maiti. Inafikia familia za kimaskini zinauza hata vitu vyake ili kuweza kuleta ile maiti nchini. Je, ofisi za Ubalozi zimejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wenye hali duni maiti zao zinapopatikana kule ziletwe nchini haraka? (Makofi)
Swali la pili, kuna baadhi ya Balozi zina utaratibu wa kupanga siku maalum za kuwahudumia Watanzania, hususan tabia hiyo ilikuwepo katika Ubalozi wetu wa Afrika Kusini. Tabia ile ilileta matatizo na usumbufu kwa Watanzania ambao wanataka huduma katika ofisi za Ubalozi.
Je, sasa hivi wamejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wanaotaka huduma kwenye Balozi zao nje ya nchi yetu wanapata huduma haraka? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa nyakati tofauti kumeripotiwa baadhi ya Watanzania ambao wamefiwa na ndugu zao kupata taabu katika kusafirisha miili, lakini katika hali ya jumla Balozi zimekuwa zikisaidia sana pale wanapopata taarifa sahihi kwa wakati. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba mara nyingine ucheleweshaji unatokea kutokana na Balozi zetu kuweza kupata taarifa kwa wakati, lakini katika hali ya jumla, kati ya masuala ambayo Balozi wetu zinatakiwa zishughulikie ni kuhusu maslahi ya Watanzania wanaoishi huko ikiwa ni pamoja na pale wanapopata taabu, wanapopatwa na matatizo ikiwa ni pamoja na kifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna changamoto ambazo zimetokea, kila wakati Wizara imekuwa ikichukua changamoto hizo na kuzifanyia. Kwa hiyo, tunaamini huko mbele tunakoelekea, changomoto hizi zitaendelea kupungua na hasa sasa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejikita katika kuleta ufanisi na nidhamu katika utumishi wa umma. Kwa hiyo, tunaamini upungufu na changamoto ambazo zimekuwa zikitokea nyuma, zitapungua kama siyo kuondoka moja kwa moja.
Ni rai ya Mheshimiwa Mbunge kuhusu Balozi zetu kupanga siku maalum kwa ajili ya kuwatumikia na kutoa huduma kwa Watanzania, pendekezo la Mheshimiwa Mbunge ni zuri, Wizara italiangalia, lakini ifahamike kwamba hakujaripotiwa kwa kiwango kikubwa kuhusu Watanzania kushindwa kupata huduma za kibalozi, lakini kama nilivyosema tutalipeleka na kuliangalia na iwe ni moja kati ya njia za kususluhisha changamoto ambazo zinatokea.