Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Primary Question

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kupambana na rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ikizingatia kuna upungufu wa Watumishi pamoja na vitendea kazi?

Supplementary Question 1

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wataendelea kuwepo hapa kwa miezi mitatu inayokuja, lakini bado mazoezi kule kwenye majimbo yao yanaendelea kufanyika na kwa sababu Serikali imesema kwamba mwaka 2023/2024 imeajiri watumishi 350. Swali la kwanza; Je, idadi hii ndiyo idadi hitajika au bado kuna mahitaji na kama yapo nini kinafanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri ningeomba utusaidie kumekuwa kukijitokeza kwa dhahiri dalili za uvunjifu wa amani kwa lugha na kejeli na mambo mengi sana. Sasa ningeomba Serikali iliambie Bunge lako; je, wamejipangaje kama Serikali ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unaokuja utakuwa wa salama, wa uhuru na haki na hakuna mtu ambaye anaweza kuzuia uchaguzi kwa mujibu wa Katiba? Ahsante. (Makofi)

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Zahor majibu ya maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali ya Awamu ya Sita imeingia madarakani imeweka nguvu kubwa sana katika kuzuia na kupambana na rushwa. Katika kufanya hivyo tumeweza kupata vitendeakazi ambavyo kweli hatujawahi kupata kwa kiasi hicho toka chombo hiki cha TAKUKURU kuanzishwa. Kupata magari 178 kwa TAKUKURU ni jambo kubwa na imesaidia sana. Kwa sasa halmashauri zote zina magari mapya na ambao hawakupata magari mapya ya kwao ni mazima sana. Kwa hiyo itatusaidia katika kupambana katika ngazi ya wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka toka Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani 2022 mpaka 2025, hivi sasa tumeweza kuongeza watumishi 1,190. Watumishi hawa sisi tunaamini wanatosha karibu kila Ofisi sasa kwenye wilaya zetu zina watumishi kuanzia watano hadi 15. Sisi tunaamini hao wanatosha kuweza kupambana au kupeleka elimu kwa sababu sehemu kubwa ambayo tunataka kujikita nayo ni kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa njia mbalimbali kuhakikisha kwamba wananchi wanajua madhara ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zahor pia ameuliza juu ya wale ambao wameanza harakati au dalili za kutumia rushwa, lakini kuanza harakati ambazo zinapelekea uvunjifu hata wa amani. Ninataka niseme tu nchi yetu ina uzoefu mkubwa katika kushughulika na chaguzi na mpaka sasa tumeshafanya chaguzi takribani mara saba. Uzoefu huu unaifanya nchi yetu kuwa Mwalimu wa demokrasia katika ukanda wetu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mbunge kwamba kwa wale ambao wamejiandaa kuleta fujo au kuleta mambo ambayo yanaleta sintofahamu kwa jamii, Serikali hata siku moja huwa haipumziki wala hakuna gap. Serikali ipo na hata kama tuko hapa na wengine wako hapa lakini Serikali ipo na vyombo vyetu katika kusimamia sheria huwa vina ushirikiano. Kwa hiyo hakuna mahali ambapo kutakuwa kuna upungufu wa watu wanaosimamia sheria. Ninataka nimhakikishie Mbunge kwamba Serikali imejipanga katika kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kama ambavyo tumeshughulikia chaguzi nyingine kwa mafanikio makubwa.