Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Msinga hadi Masoka ili kupunguza adha kwa wananchi wa Moshi Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu kabla ya kuuliza maswali ya nyongeza nitoe pole kwa wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini, Kata ya Uru Kusini, ambao wamepata maafa. Kuna zaidi ya kaya sita hawana makazi kwa sababu ya mafuriko na nyumba zao zimebebwa na maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itajenga Barabara ya Kisawio mpaka Kaliwa, barabara ambayo imeleta maafa na kusababisha nyumba hizi kupelekwa na maji; ni lini Serikali itachukua mkakati wa ziada na wa makusudi kujenga hii barabara kwa sababu imekuwa inaleta adha kila mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali itajenga Barabara ya kuanzia Darajani mpaka kwa Seba, Kata ya Kindi kwa sababu barabara hii pia imekuwa kero na uchumi wa Moshi Vijijini unategemea barabara?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue fursa hii kuanza kwanza kumpongeza Mheshimiwa Felista Njau kwa maswali yake mazuri kabisa ambayo yanalenga kutaka kuona maendeleo katika sekta ya barabara katika Mkoa huu wa Kilimanjaro katika Wilaya ya Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali yake yote mawili kwa pamoja. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inafanya uwekezaji mkubwa katika kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara hizi zinazosimamiwa na TARURA. Ndiyo maana tutaona tangu Serikali hii ya Awamu ya Sita imeanza kazi na imeongeza bajeti ya TARURA kutoka bilioni 275 kwa mwaka hadi kufikia bilioni 710 kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Kilimanjaro, bajeti imeongezeka maradufu. Mwaka 2020/2021, bajeti ya ya TARURA Mkoa wa Kilimanjaro ilikuwa ni bilioni 10.7, lakini tunapozungumza leo kwa mwaka huu wa fedha, bajeti ya TARURA ni bilioni 34.1. Kwa hiyo, utaona dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha inafikia maeneo mbalimbali ya barabara zetu hizi za TARURA ili kuweza kuziboresha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali itafika katika Barabara hii ya Kisawio na Barabara ya Darajani mpaka Seba na kuhakikisha zinajengwa na kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii.

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Msinga hadi Masoka ili kupunguza adha kwa wananchi wa Moshi Vijijini?

Supplementary Question 2

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi. Jimbo la Newala Vijijini lina barabara nyingi ambazo zimeharibika na baadhi hazipitiki. Kwa mfano, Barabara ya Mkomatuchi – Memena haipitiki kabisa, Barabara ya Malatu Shuleni – Mchaulu – Mpalu, Mtopwa na Chilondolo. Je, Serikali ina mpango upi wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zinatengenezwa ili ziweze kupitika vizuri?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Maimuna Mtanda, kwa swali lake zuri kabisa lenye maslahi mapana kwa ajili ya wananchi wa Newala Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina nia thabiti ya kufikia mtandao mkubwa zaidi wa barabara hizi ambazo zinasimamiwa na TARURA (barabra zenye hadhi ya wilaya). Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafika kwenye barabara alizoziainisha kwa ajili ya kuzikarabati, kuzijenga ili ziwe kwenye hali nzuri na ziweze kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii.

Name

Nicodemas Henry Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Msinga hadi Masoka ili kupunguza adha kwa wananchi wa Moshi Vijijini?

Supplementary Question 3

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe….

NAIBU SPIKA: Ngoja kwanza, kwa nini umehama kwenye kiti chako? Ndiyo maana nimeshangaa, mimi najua siku zote wewe mwenye hela unakaa huku. Haya, endelea.

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa nimekuelewa. Barabara za Mbogwe zinazomilikiwa na TARURA ziko choka mbaya, zimenyeshewa na mvua, zilizojengwa mwaka 2024 zimekatika kwa mvua. Je, Serikali ina mpango gani wa kwenda kukarabati barabara hizi ambazo zimekatikakatika?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Maganga, kwa swali zuri ambalo linalenga kuwasaidia na kuwasemea wananchi wa Jimbo la Mbongwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita unaona kabisa imeongeza bajeti ya TARURA kutoka bilioni 275 mpaka bilioni 710 kila mwaka. Dhamira ya dhati ni kwamba, inataka kufikia mtandao mkubwa zaidi wa barabara zetu hizi za TARURA ili kuweza kuziboresha na ziweze kuwasaidia na kuwanufaisha wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata katika Jimbo lake la Mbogwe Serikali itaendelea kuleta fedha kwa ajili ya kuhakikisha barabara alizoziainisha zinaweza kukarabatiwa na kuwa katika hali nzuri na kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Msinga hadi Masoka ili kupunguza adha kwa wananchi wa Moshi Vijijini?

Supplementary Question 4

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Boma la Ng’ombe inayopita Ng’ingula – Masisiwe – Oidegenda mpaka Isanga wakati wa mvua haipitiki kabisa. Ni kwa nini Serikali isiikarabati? Kuna maeneo madogo tu kama mawili ambayo yanasababisha barabara hii isipitike muda wote. Je, Serikali iko tayari kuangalia sehemu ambazo ni korofi ili iweze kukarabati na kupitika muda wote? Ahsante sana.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Ritta Kabati, kwa swali lake zuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Barabara hii ya Boma la Ng’ombe itafikiwa na Serikali kwa ajili ya kukarabatiwa ili iwe katika hadhi nzuri na iweze kupitika katika kipindi cha mwaka mzima ili wananchi waweze kupata manufaa ya kiuchumi na waweze kufikia huduma za kijamii.