Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Atashasta Justus Nditiye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Primary Question
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITILE (K.n.y MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:- Miji mingi nchini inakabiliwa sana na uhaba wa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji. (a) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kuajiri Maafisa hawa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu? (b) Je, ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kununua vifaa vya kupimia ardhi kama vile darubini, GPS na kadhalika na kuvisambaza kwenye Miji yetu ikiwemo Mji wa Kasulu?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya kutia moyo ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa migogoro ya ardhi katika Halmashauri zetu na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imekuwa mingi sana, je, Serikali ina mpango gani wa kuziwezesha ofisi za Kanda ku-speed up utoaji wa hati ili kupunguza migogoro ya ardhi? (Makofi)
Sehemu ya pili, moja kati ya vitu vinavyosababisha migogoro mikubwa sana ya ardhi, hasa mijini ni uwepo wa baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi wasiokuwa waaminifu katika Halmashauri zetu, watumishi hawa wamekuwa wakikaa muda mrefu sana sehemu moja ya kituo cha kazi. Je, Serikali ina mpango wowote wa kuwabadilisha mara kwa mara ili kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na watumishi hao wa Idara ya Ardhi? Ahsante.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikiwezesha Ofisi za Kanda na tuna Kanda nane na zote zinafanya kazi hiyo ya usajili kama alivyosema, pengine labda kama kuna eneo ambalo lina upungufu na kazi hazifanyiki vizuri tungeomba kufahamu, kwa sababu ninavyofahamu mimi Kanda zote nane zinafanya kazi ya usajili na ndiyo maana tumefanya hivyo ili kurahisisha usajili katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kama kuna sehemu kuna tatizo basi ni vizuri tukafahamu maaana lengo la Serikali ni kurahisisha na kupunguza ule muda wa kusubiri, kwa sababu sasa hivi ndani ya mwezi mmoja tunasema hati inakuwa imeshasajiliwa. Lakini kama lengo letu halifikiwi maana yake kuna tatizo mahali fulani, sasa nitashukuru sana Mheshimiwa Mbunge kama atatuambia kwamba pengine kanda hiyo ambayo anatoka yeye hakuna ufanisi mzuri katika suala zima la usajili.
Mheshimiwa Spika, swali la pili anasema uwepo wa watumishi wasio waaminifu na wa kukaa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, nadhani ni azma ya Serikali kuona kwamba watumishi wanapokuwa katika maeneo wanafanya kazi zao kwa uadilifu na weledi mkubwa kama ambavyo dhamana hiyo wamepewa. Lakini pale inapotokea pengine mtumishi amekaa eneo moja muda mrefu na amekuwa mzoefu kawa kama ni mwanakijiji katika eneo lile au ni mwanamji wa pale na ameshindwa kufanya kazi aliyoifanya, basi tutawasiliana na Wizara husika ili tuweze kuona nini cha kufanya. Kwa sababu kumhamisha pale kama ameshindwa kufanya kazi na kumpeleka eneo lingine unakuwa hujamsaidia, kama ana tatizo kubwa basi tujue tatizo lake ni nini ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa. Pengine kuwahamisha tu inaweza ikawa siyo solution, lakini kikubwa ni kujua madhaifu yake ni nini ili tuweze kuona hatua za kinidhamu kuweza kumchukulia mtumishi kama huyo.
Name
Magdalena Hamis Sakaya
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Primary Question
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITILE (K.n.y MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:- Miji mingi nchini inakabiliwa sana na uhaba wa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji. (a) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kuajiri Maafisa hawa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu? (b) Je, ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kununua vifaa vya kupimia ardhi kama vile darubini, GPS na kadhalika na kuvisambaza kwenye Miji yetu ikiwemo Mji wa Kasulu?
Supplementary Question 2
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru kwa nafasi, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa utendaji mbovu na kutokuwajibika kwa watendaji wa ardhi waliopo kwenye Halmashauri kunachangiwa pia na muundo mzima kwamba watendaji wale hawapata order wala maelekezo kutoka kwenye Serikali Kuu kwa maana ya kwenye Wizara, na hasa wanapokosea inakuwa ni vigumu kwa Waziri kutoka juu kumchukulia hatua kwa sababu anasikiliza sana kwenye Halmashauri.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa, kwa unyeti wa Wizara hii na kuondoa migogoro ndani ya nchi yetu kuhakikisha kwamba watendaji wote wa ardhi wanapokea order kutoka juu na hata wanapokosea waweze kuchukuliwa hatua kutoka juu ili kuondoa migogoro ndani ya nchi yetu?
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, utendaji mbovu wa watumishi hasa kwenye sekta ya ardhi nadhani siyo suala tu pia la kujua kwamba anapokea order kutoka mamlaka ipi. Ni kweli katika ule mlolongo uliopo pengine unaweza ukaliona hivyo, lakini nia ya Serikali kugatua madaraka na kusogeza huduma katika Halmashauri zetu ilikuwa ni nia njema na dhamira ya dhati ya kutaka kuona kwamba huduma zile zinafanyika kwa wakati mahali ambapo watu wanahitaji.
Mheshimiwa Spika, lakini hili kama limekuwa ni tatizo, nadhani suala la msingi ni ndani ya Serikali kuweza kuona namna ya kuweza kudhibiti udhaifu huu au utendaji huu mbovu uliopo ili tuweze kujua kwamba hapa kinachotakiwa kufanyika, kama mtumishi ambaye anafanya utendaji wake katika viwango visivyostahili na akitarajia tu kabisa kwamba mamlaka yenye sauti kwake ni mamlaka fulani, hilo halimfanyi yeye asamehewe katika kosa alilolifanya.
Kwa hiyo tunachosema, ugatuaji wa madaraka ilikuwa ni kusogeza huduma, lakini kama suala la kitaaluma au suala la kitendaji linaonekana lina ugumu katika namna ya kudhibiti watendaji hawa, nadhani ni suala la kuongea kati ya Wizara zote mbili husika tukajua ni jinsi gani watu hawa tutaweza kuwasimamia vizuri zaidi ili wafanye kazi zao kwa weledi.
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Primary Question
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITILE (K.n.y MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO) aliuliza:- Miji mingi nchini inakabiliwa sana na uhaba wa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji. (a) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa kuajiri Maafisa hawa moja kwa moja wanapohitimu Vyuo Vikuu? (b) Je, ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kununua vifaa vya kupimia ardhi kama vile darubini, GPS na kadhalika na kuvisambaza kwenye Miji yetu ikiwemo Mji wa Kasulu?
Supplementary Question 3
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Pamoja na uhaba wa Maafisa wa Ardhi na uhaba wa fedha, lakini zoezi la kupima ardhi nchini limekuwa likisuasua na mahitaji ya wananchi kujenga yamekuwa yakiongezeka, kwa hiyo ukiangalia katika hali ya kawaida wananchi wengi wamekuwa wakijenga katika maeneo ambayo hayajapimwa, sasa nataka kauli ya Serikali, ipi ni kauli ya Serikali juu ya wananchi wote wanaojenga katika maeneo ambayo hayajapimwa na Serikali bado inasuasua kwenye kupima maeneo hayo ya ardhi? Ahsante.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kasi ya wananchi kujenga ni kubwa kuliko speed ya Serikali katika kupima maeneo, na ni maeneo mengi ambayo kwa sasa yamekaliwa katika mpangilio usio sahihi na ndiyo maana Wizara imeliona hili na tukaja na programu ile ya miaka mitano ya kuhakikisha kwamba wale ambao wamekuwa na speed kali kuliko Serikali tunajaribu kurasimisha maeneo yao ili wakae katika utaratibu mzuri waweze kutambuliwa na Serikali iweze pia kupata kodi zake kupitia katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, lakini katika kuona hili pia tunalifanyia kazi, Serikali imesajili makampuni, ina makampuni karibu 55 ambayo yanafanya kazi ya upimaji katika maeneo, na upimaji wao wanaofanya wanafanya kulingana na mipango iliyoko katika maeneo hayo kwa maana ya ile mipango miji kwenye yale maeneo, masterplan zao ambazo wameziweka pale.
Kwa hiyo kikubwa tunachosema, kasi ya wananchi ni kubwa, Serikali ina speed ndogo na eneo lililopimwa ni dogo, kwa hiyo tunaomba Halmashauri zilizotayari ziyatumie haya makampuni ambayo tumeyabainisha katika suala zima la upimaji, na nilisema pia wakati najibu swali hili tarehe tisa, nikasema orodha tayari tunayo, Halmashauri yoyote iliyo tayari tuwasiliane ili tuwape ile orodha waweze kufanya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lengo letu ni kuhakikisha Miji imekaa vizuri na imepangika na tunawaomba wananchi, tunawasihi wasianze kuvamia maeneo ovyo sasa hivi kwa sababu kadri tunavyozidi kuweka mikakati ndivyo jinsi ambavyo wao watakuwa katika hatua nzuri ya kuweza kupangiwa maeneo yao, kwa hiyo wasikimbie sana kwa sababu tayari kama Wizara tunaamua kufanya kazi hii kwa weledi mkubwa.