Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Primary Question

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:- Wananchi wa Bonde la Mwakaleli, Kata za Kandete, Isange na Luteba wanaoishi kando ya Hifadhi ya TANAPA wamekuwa wakinyanyaswa sana na watumishi wa TANAPA kwa kisingizio kwamba wamevamia Hifadhi wakati TANAPA ndio waliovamia makazi ya wananchi kwa kuweka mipaka mipya tofauti na ile ya zamani hali inayofanya baadhi ya shule na taasisi zingine kuonekana kuwa ndani ya Hifadhi ya TANAPA kwa sasa:- Je, ni lini Serikali itarudisha mipaka ya zamani ili wananchi wasiendelee kuishi kwa wasiwasi, lakini pia waendelee na shughuli za kilimo kama ilivyokuwa zamani?

Supplementary Question 1

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo wananchi wa Busekelo hawajaridhika nayo, kwa sababu wananchi hawa wako pale tangu miaka ya 1950 na mipaka imefanyika mwaka 2006/20007, ni mwaka wa tisa sasa bado wananyanyaswa sana na watu wa TANAPA.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na watumishi wa TANAPA ambao wanawanyanyasa wananchi na wanashindwa hata kuendeleza maeneo yao ya kilimo, shule pamoja na makanisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, atakuwa tayari tuongozane twende akajionee kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa Bonde la Mwakaleli ili ukajithibitishe hiyo mipaka?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASISILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wanaosimamia utekelezaji wa sheria upande wa misitu na wanyamapori, wanaosimamia hifadhi walio wengi wanajitahidi kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, kwa wale wachache ambao wanafanya hayo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge ya unyanyasaji na tabia nyingine zozote ambazo si nzuri, zinazoipaka matope Serikali wanafanya makosa na tunaomba pale ambapo inajitokeza, wanaohusika watolewe taarifa katika vyombo vinavyohusika watachukuliwa hatua zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenda, niko tayari kati ya Mkutano huu na Mkutano ujao, hebu tukutane baadaye tuweze kupanga vizuri ratiba, tunaweza kwenda wote kuangalia na kupata ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kwamba, Serikali imejipanga sasa na kwa sababu matatizo haya ni ya muda mrefu, sasa tumejipanga vyema zaidi na katika kipindi cha muda mfupi ujao mtashuhudia tunavyoweza kurudia kuweka mipaka kwa namna kabisa ya maelewano ya wale tunaopakana nao ili baada ya kuwa tumeshaweka mipaka hiyo, tunatarajia wananchi wataheshimu mipaka hiyo na wataacha kuvuka mipaka hiyo kwenda kwenye maeneo ya hifadhi.