Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARY F. MASANJA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa na Watumishi Kituo cha Afya Budushi Wilayani Kwimba?

Supplementary Question 1

MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kwa kunipa nafasi hii. Kwanza niipongeze Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imejenga majengo mazuri ya vituo vya afya, na leo hii wananchi wanaendelea kuyatumia. Kwa hiyo, tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kituo cha Afya cha Budushi kinahudumia zaidi ya wananchi 80,000 ambao ni wa Tarafa ya Ngulla. Wananchi hawa wanatumia Kituo cha Afya cha Budushi, lakini kituo hiki hakina gari la wagonjwa, gari ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri analiongelea ni la hospitali ya mission ambalo wananchi wanalipia. Hivyo, naiomba Serikali ipeleke gari pale ili hawa wananchi zaidi ya 80,000 waweze kuhudumiwa kwa huduma bora na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kituo cha Afya cha Budushi hakina mtumishi wa maabara na watumishi wengine mbalimbali. Tunatambua ya kwamba, mgonjwa yeyote anapoenda hospitali, cha kwanza kabisa ni lazima apimwe afya na pale hakuna mtumishi wa maabara. Naiomba Serikali impeleke mtumishi pale mara moja ili wananchi hawa wapate huduma iliyo bora, ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nipokee maombi ya Mheshimiwa Mary Francis Masanja. Maombi haya yanatokana na nia yake ya kuona kwamba wananchi, ikiwemo wanawake kutoka katika Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Kwimba wanapatiwa huduma nzuri za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inafanya uwekezaji mkubwa sana kwa upande wa afya msingi na ndiyo maana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, zaidi ya shilingi trilioni 1.29 zimewekezwa kwenye upande huu wa afya msingi. Tayari magari ya kutolea huduma ya kubeba wagonjwa (ambulances) 382 yamenunuliwa na kusambazwa kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mary Masanja kwamba, tutazingatia uhitaji huu wa gari la kuhudumia wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Budushi. Serikali itatafuta fedha ili iweze kununua gari hilo na kulileta kwa ajili ya kuwahudumia wananchi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mtumishi wa maabara, Serikali ya Awamu ya Sita katika uwekezaji wake kwenye sekta hii ya afya msingi katika kipindi cha mwaka 2021/2024 imeajiri watumishi 25,936 wa kada ya afya na bado mwaka 2024 vibali vilitolewa na Serikali kwa ajili ya kuajiri watumishi zaidi ya 8,000 katika kada hii ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutazingatia katika ajira hizi mpya kumpanga mtumishi wa kwenda kutoa huduma katika maabara kwenye Kituo hiki cha Afya cha Budushi.

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. MARY F. MASANJA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa na Watumishi Kituo cha Afya Budushi Wilayani Kwimba?

Supplementary Question 2

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunaishukuru Serikali kwa kujenga vituo vingi vya afya kwenye Wilaya ya Tanganyika. Swali langu la msingi ni kwamba, kwa kuwa, Serikali imejenga vituo vya afya, na vingi havina magari ya kubebea wagonjwa, ni lini Serikali itapeleka gari kwenye vituo vya afya, Tarafa ya Karema, Mwese na Kabungu, eneo la Mishamo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha huduma za afya na hasa huduma ya afya msingi. Ndiyo maana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, siyo tu Serikali imejenga hospitali za halmashauri 129, pia imejenga vituo vya afya 367.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa muktadha wa swali la Mheshimiwa Kakoso kuhusiana na kupeleka magari ya kubebea wagonjwa (ambulance), tayari Serikali imeshanunua magari hayo 382 na kuyasambaza kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba bado kuna uhitaji mkubwa sana wa kuendelea kununua na kusambaza magari hayo ili yaweze kutoa huduma bora zaidi ya afya msingi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kutafuta fedha inunue magari haya ya kuwabebea wagonjwa (ambulance) na kuweza kuyasambaza kote nchini, ikiwemo kwenye jimbo lake katika Wilaya ya Tanganyika.

Name

Prof. Makame Mnyaa Mbarawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkoani

Primary Question

MHE. MARY F. MASANJA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa na Watumishi Kituo cha Afya Budushi Wilayani Kwimba?

Supplementary Question 3

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nianze kwa kumpa pole Mkuu wangu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, pamoja na Mkuu wa Wilaya, Godfrey Mnzava, wananchi wa Mbokomu na familia zilizopata msiba kwa ngema ambayo imeua watu watatu, kwa tukio lililotokea jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niulize swali lifuatalo: Zahanati ya Funduhu katika Kata ya Old Moshi Mashariki ina uhaba mkubwa wa maabara pamoja na vifaa tiba. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wananchi wanaopata huduma katika zahanati hii ili waweze kupata huduma kutoka kwenye Serikali yao?

Name

Gibson Blasius Meiseyeki

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Magharibi

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Profesa Ndakidemi kwamba, Serikali katika kipindi cha miaka minne imeongeza mara dufu bajeti kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani ilikuta bajeti kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba ni shilingi bilioni 35, lakini wakati huu tunaozungumza, bajeti ile imepanda maradufu hadi kufikia shilingi bilioni 181.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie kwamba, fedha zipo kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kumwagiza RMO pamoja na DMO wakishirikiana na Mkurugenzi kusimamia na kuhakikisha kwamba, vifaa na vifaa tiba vinapatikana kwa sababu, fedha ipo na inapatikana kwa ajili ya kwenda kutoa huduma bora zaidi katika zahanati hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo la maabara, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, inaboresha miundombinu katika sekta ya afya kwa kuendelea kujenga majengo ya kutolea huduma za afya msingi, ikiwemo zahanati. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali kupitia fedha za mapato ya ndani na kupitia fedha kutoka Serikali Kuu itaendelea kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya kutolea huduma ya afya msingi na itakuja kufika katika jimbo lako, kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika zahanati hii aliyoitaja.

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. MARY F. MASANJA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa na Watumishi Kituo cha Afya Budushi Wilayani Kwimba?

Supplementary Question 4

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea Kituo cha Afya Mkulwe. Je, ni lini tutapata gari la kubebea wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Mkulwe?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imenunua magari 382 ya kubebea wagonjwa na kuyasambaza kote nchini, lakini Serikali inatambua bado kuna uhitaji wa magari haya (ambulance). Serikali inaendelea kutafuta fedha ili iweze kuendelea kununua magari haya na kuendelea kuyasambaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Condester Sichalwe kwamba, katika kituo cha afya alichokitaja, Serikali itatafuta fedha inunue gari hili la kubebea wagonjwa ili iweze kulileta katika kituo hicho cha afya ili huduma za afya msingi katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge ziweze kuimarika.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. MARY F. MASANJA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa na Watumishi Kituo cha Afya Budushi Wilayani Kwimba?

Supplementary Question 5

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa wilaya zilizobahatika kupata gari la wagonjwa, lakini jiografia ya Wilaya ya Nkasi ni mbaya sana. Serikali mna mkakati gani wa kupunguza vifo vya wanawake, hasa wajawazito, kwa kuwapelekea gari karibu?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari mpaka wakati huu imeshanunua magari 382 ya kubebea wagonjwa na kusambazwa kote nchini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma za afya msingi zinaimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjibu Mheshimiwa Aida kwamba tunatambua kuna umuhimu mkubwa sana wa kuendelea kupeleka magari haya ya kubebea wagonjwa katika jimbo lake kwa sababu, kama alivyosema mwenyewe, magari haya pia kwa kiasi kikubwa yanatumika kuwasaidia akina mama wajawazito pindi wanapokuwa wamepata dharura kuweza kuwatoa kwenye kituo kimoja kuwapeleka kwenye kituo kingine, kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Aida kwamba Serikali inatambua umuhimu huo, ndiyo maana inatafuta fedha ili ziweze kununua magari mengine ya nyongeza baada ya haya 382 kununuliwa kwa ajili ya kuendelea kusambazwa katika vituo vyetu, na kwenye Jimbo la Nkasi tutafika.