Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga vituo vya kuegesha malori katika maeneo ya Nyakahura na Biharamulo Mjini?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini ninazo hoja mbili. Kwanza, kwenye hii ya ujenzi wa Kituo cha Malori cha Nyakahura ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Alitoa maelekezo tarehe 21, mwezi wa tisa, 2021 alipotembelea Wilaya ya Biharamulo. Wakati anaenda Ngara, alisimama Nyakahura pale, akatoa maelekezo tutafute eneo, kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa eneo tayari tumeshalipata na hiki kinachosemwa siyo ujenzi. Ujenzi wa standard parking ya malori unaenda 3.4 billion. Sasa hapa tumetafuta eneo, tumesawazisha kwa sababu, barabara hii kutoka Lusahunga kwenda Benako iko kwenye ujenzi. Sasa kuondoa adha kwa wananchi imebidi itafutwe hii kwa ajili ya kupaki malori, lakini siyo standard parking yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu ni maelekezo ya Waziri Mkuu, na Naibu Waziri yuko hapa, na kwenye ziara ile aliambatana na watu wa TAMISEMI; naomba sasa Waziri aelekeze Halmashauri ya Biharamulo kupitia kwa Mkurugenzi na RAS wa Kagera waandae lile andiko haraka liletwe kwa ajili ya wananchi wale wa Nyakahura kuweza kuandikiwa mradi ule wa kimkakati na kupata hii huduma ambayo ina-cost almost 3.4 billion?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, habari ya Biharamulo Mjini, tunategemea baada ya SGR kukamilika na kwa sehemu kubwa mizigo mingi inayoelekea Uganda na maeneo mengine itashushiwa Isaka. Sasa Biharamulo is the last point kama unataka kuingia kwenye Pori la Kasindaga. Kwa hiyo watu wengi wana-opt kulala Biharamulo Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili linalosemwa, ni nje kidogo ya mji, na hivyo huwezi kulazimisha madereva walale kule ambako unakutaka wewe. Hii ni biashara. Sasa naomba, kwa sababu tayari maeneo yapo pale Biharamulo Mjini, TAMISEMI kupitia kwa Waziri, wako tayari kuelekeza andiko jipya lingine kwa ajili ya kupaki malori Biharamulo Mjini ili watu ambao wanakimbizana kwenda Kazindaga walale pale kwa ajili ya kutoa huduma na waweze kutoa huduma ndani ya Biharamulo Mjini?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ezra John Chiwelesa amekuwa akifanya jitihada kubwa sana ya kusemea miradi ya kimkakati katika jimbo lake. Hii siyo miradi ya mwanzo ambayo anaizungumzia, kwa maana ya kimkakati. Miradi hii inayoibuliwa ni miradi inayowezesha kimapato halmashauri au mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii miradi inajengwa kwa taratibu mbili. Kwanza ni kupitia mapato ya ndani ya halmashauri pia kupitia Serikali Kuu. Serikali Kuu pia na yenyewe inaongeza fedha kuhakikisha kwamba baadhi ya miradi hii inaweza kupata fedha na kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa miradi hii miwili naomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwagiza Mkurugenzi afanye tathmini ya viability ya miradi hii miwili, na akijiridhisha waweze kuandika andiko ambalo litakuja Ofisi ya Rais, TAMISEMI na sisi tutalipeleka Tume ya Mipango. Tume ya Mipango wakishali-approve litakwenda Wizara ya Fedha kwa ajili ya upatikanaji wa fedha kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza kujenga miradi hii ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kauli yangu kwa leo iwe hiyo kwa Mheshimiwa Ezra John Chiwelesa ambaye kwa kweli anapambania sana miradi ya kimkakati kwenye jimbo lake. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved