Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Shinyanga na Tabora katika eneo la Ushetu na Kaliua ambao umechukua muda mrefu sana?

Supplementary Question 1

MHE. EMMANUEL P. CHEREHENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, kwanza mimi niseme kwamba, mgogoro upo na hata kipindi Mheshimiwa Rais ameteua wale Mawaziri wanane waliokuja Shinyanga, Mkoa ulitoa taarifa juu ya mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifikia hatua wananchi wangu zaidi ya 17 wakakamatwa kimakosa wakiwa na vibali na mali zao zikataifishwa zikapelekwa Kaliua na kuna kipindi ilifikia hatua kati ya Askari wa TFS upande wa Kaliua na wa Halmashauri yetu ya Ushetu wakakutana pale kwenye mipaka baada ya kuona mipaka ya Hifadhi ya Igombe ilihamishwa kuja kwenye eneo la Ushetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamishna wa Ardhi aliagizwa na alishafika akafanya tathmini na timu yake yote ya kusoma kutafsiri upya ramani. Kilichokuwa kimebakia ni Waziri kuja kutangaza tu mipaka ikae wapi? Naomba kujua, ni lini Mheshimiwa Waziri wa Ardhi atakuja kutafsiri na kusoma mipaka ili kuondoa mwingiliano uliopo kwa wananchi wangu?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli historia aliyoitoa Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, kwamba kumekuwa na changamoto ya tafsiri ya mipaka katika eneo la Hifadhi ya Msitu wa Igombe River pamoja na Hifadhi ya Msitu wa Ushetu Ubagwe. Hifadhi moja ikiwa iko chini ya TFS na hifadhi nyingine ikiwa ipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu. Kama yeye mwenyewe alivyotoa historia, jambo hili limefanyiwa kazi na kufikia ukingoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamana ya tafsiri ya mipaka ya ardhi ikiwemo mpaka kati ya Hifadhi hii ya TFS na Hifadhi hii ya Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ipo chini ya Wizara ya Ardhi. Tayari Mheshimiwa Waziri wa Ardhi suala hili analifahamu, na kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Waziri ataweza kulishughulikia aweze kupitia Wizara ya Ardhi kutoa tafsiri ya mipaka na kuweza kukamilisha kabisa kumaliza huu mgogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ndilo ninaloweza kumjibu Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, akae na amani, Serikali ipo kazini na itakuja kutatua mgogoro huu katika jimbo lake.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri pia kuna nyongeza kutoka kwa Naibu Waziri wa Ardhi, karibu.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba swali hili lilikuwa lielekezwe kwenye Wizara yetu kwa sababu lina mechanism ya kiutendaji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya maswali na majibu, tutakutana ili tuweze kulijengea hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba lilishafanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa sana, na hivyo baada ya kipindi cha maswali na majibu tutakutana na mhusika ili tuweze kuyajenga vizuri kuyafikisha kwenye eneo halisi.