Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Primary Question

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:- Je, lini Serikali itaipatia Gari la Wagonjwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ni kweli Kituo cha Afya cha Duthumi ndiyo kina ambulance inayohudumia zaidi ya kata tano ambazo ni Kata ya Bwakira Juu, Kata ya Mngazi, Kata ya Singisa na kinahudumia pia kwenye vituo vya afya vya Kata ya Kisaki na Kata ya Kasanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kiuhalisia ni kwamba bado tunahitaji ambulance kwa ajili ya kusaidia kutoa referrals kwenye hospitali ya wilaya kupeleka kwenye hospitali ya mkoa. Kwa sababu hizo kilometa 20 wakati gari iko kwenye maeneo mengine ambayo ni zaidi ya kilometa 40 wagonjwa wanapata matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; je, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ina upungufu wa wataalam wa usingizi. Tunaye mtaalam mmoja tu. Ni lini Serikali itatupatia mtaalam mwingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kata ya Singisa tayari tumeshaandaa eneo kwa ajili ya kituo cha afya cha mkakati kile ambacho tumeahidiwa na wataalam wa afya wilaya wameshafika kukagua eneo. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili hicho kituo cha afya kijengwe? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninawapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwa sababu Serikali ilinunua magari ya wagonjwa na ilitoa maelekezo kwamba magari hayo yapelekwe kwenye vituo vyenye idadi kubwa zaidi ya wananchi ili huduma za rufaa ziwe na ufanisi mkubwa zaidi. Kwa hiyo, kupeleka katika Kituo cha Afya cha Duthumi ambacho kinahudumia zaidi ya kata tano zinazokizunguka kituo cha afya ulikuwa ni uamuzi mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inatambua kwamba tunahitaji gari lingine la wagonjwa kwa ajili ya hospitali ya halmashauri. Ninamhakikishia Mheshimiwa Kalogeris kwamba, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kunua gari hilo la wagonjwa ili hospitali ya wilaya pia ipate gari kwa ajili ya huduma za rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, tunafahamu Serikali imeweka mkakati wa kujenga vituo vya afya katika kata za kimkakati ikiwemo kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja na tayari wataalam wameshafanya tathmini ya ukubwa wa eneo. Ninapenda kumhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni suala la muda, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo kwa awamu. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:- Je, lini Serikali itaipatia Gari la Wagonjwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro?

Supplementary Question 2

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Hanang ina vituo vya afya nane na hospitali ya wilaya moja. Magari yako mawili kwenye hospitali ya wilaya. Je, ni upi mpango wa Serikali kupeleka gari kwenye vituo hivi vya afya kwa sababu umbali wa kijografia kutoka tarafa hadi tarafa ni mbali na hakuna tarafa yoyote yenye gari la kubebea wagonjwa. Ni upi mpango wa Serikali wa kuongeza gari katika wilaya hii? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Hanang ina magari mawili ya kubebea wagonjwa kwa maana ya ambulance. Pia tunao mpango wa kupeleka magari ya wagonjwa katika vituo vya afya vya kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang na vituo vyake vya afya ni moja ya vituo ambavyo vimewekwa kwenye mpango wa kupelekewa magari ya wagonjwa ili kuboresha huduma hizo za rufaa. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:- Je, lini Serikali itaipatia Gari la Wagonjwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro?

Supplementary Question 3

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niulize swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Kiponzelo ambacho kipo Kata ya Maboga, Jimbo la Kalenga, kinahudumia zaidi ya vijiji saba na wananchi wanapata adha kubwa sana kwa sababu gari lake ni bovu kabisa. Ni lini Serikali itapeleka gari kwa ajili ya kuwahudumia wananchi hao? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na magari ya wagonjwa kwenye vituo vya afya na ndiyo maana katika mgao wa hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na Jimbo la Kalenga pia lilipata magari ya wagonjwa na tunafahamu kwamba hayatoshelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge; kwanza, ninamwelekeza Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Halmashauri kuratibu ipasavyo magari haya ya wagonjwa ili Kituo cha Afya cha Kiponzelo nacho kipate huduma za rufaa pale inapohitajika tena kwa wakati. Pili, napenda kumhakikishia kwamba, Serikali iko kwenye mpango wa kutenga fedha wa ajili ya kununua magari wenye vituo vya afya vya kimkakati vyenye uhitaji mkubwa na Kituo cha Afya cha Kiponzelo pia tutakipa kipaumbele. Ahsante. (Makofi)

Name

Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Primary Question

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza:- Je, lini Serikali itaipatia Gari la Wagonjwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro?

Supplementary Question 4

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kutuingizia shilingi milioni 250 kwenye Kituo cha Afya cha Negero. Nataka kujua ni lini Serikali itatupa gari kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kilindi? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kilindi ni moja ya hospitali ambazo zinahitaji gari la wagonjwa na Mheshimiwa Omari Kigua amekuwa mara kwa mara akiwasemea wananchi wa Jimbo lake la Kilindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itakaponunua magari ya wagonjwa katika awamu inayofuata, tutahakikisha pia Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi inapelekewa gari hilo. Ahsante. (Makofi)