Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, lini Serikali itapunguza Mlima Mang’ula Kona Kilombero ikiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi?
Supplementary Question 1
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kweli kwa jambo hili, na leo wananchi wangu watakuwa na furaha kubwa kwa sababu lilikuwa ni jambo muda mrefu. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini ujenzi wa barabara kubwa ya TANROADS inayotoka Kikwawila – Mbasa – Katindiuka – Lipangalala – Daraja la Magufuli – Malinyi itaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tulikuwa tuna mkandarasi tumempata wa Barabara ya Ifakara – Mlimba kwa muda mrefu sana yule mkandarasi hajaanza kazi na ile barabara ina shida kubwa sana pamoja na daraja la Lumemo ambapo tulitarajia mkandarasi akianza atatusaidia kuweka ule mto vizuri ili wananchi wasipate mafuriko kama ambavyo wamepata jana. Je, ni lini huyu mkandarasi ambaye yuko Barabara ya Mlimba ambaye amekaa site muda mrefu ataanza ujenzi ule?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Ifakara – Malinyi ni barabara ambayo inaenda mpaka Songea. Barabara hii hata katika bajeti yetu na tayari tupo kwenye mchakato sasa hivi mkandarasi tulishampata ambaye atajenga kilometa 112 ni kati ya zile barabara ambazo zilikuwa kwenye Mpango wa EPC+F. Kwa hiyo, hii barabara itajengwa, tutaanza na kilometa 112 kwa Mpango wa Sanifu, Jenga, kuanzia Ifakara – Lupilo hadi Mtimbira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara yake ya pili ya kutoka Ifakara kwenda Mlimba, tunajenga kilometa 100 ambazo tuna lot mbili. Wakandarasi wote wameshapatikana, na ambacho bado hakijakamilika, tumesham-advance, lakini tunaendelea kum-advance ili aanze kazi, lakini tayari ameshaanza kufanya mobilization wakati mkandarasi wa pili tunatafuta advance ili naye aweze kuanza kazi. Kwa hiyo, tuna hakika katika kipindi hiki ambacho mvua inakatika, wakandarasi wote watarudi site. (Makofi)
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, lini Serikali itapunguza Mlima Mang’ula Kona Kilombero ikiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi?
Supplementary Question 2
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kukarabati Barabara ya Kusini kwa maana ya Barabara ya Dar es Salaam kwenda Lindi – Mtwara na kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Ujenzi ya ule ukarabati, naomba kuuliza swali dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kuijenga upya barabara nzima badala ya kuendelea na ukarabati ambao kila mwaka tunaingiza fedha za walipakodi kukarabati; na barabara yote kwa kweli imeoza? Nadhani wakati umefika wa kuijenga upya barabara nzima ya kutoka Dar es Salaam – Lindi kwenda Mtwara. (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Nape, Wabunge wa Kusini, pamoja na Watanzania wote kwamba Barabara ya Dar es Salaam – Kibiti – Lindi hadi Mingoyo, kweli ni barabara ambayo imechoka, lakini pia ni barabara ambayo imekuwa ikikumbwa sana na mafuriko. Kwa hiyo, tuna mipango mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kwanza ndiyo huo aliousema Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kujenga madaraja kwa kiwango cha usanifu ambao upo madaraja ya kudumu yenye ukubwa ambao umesanifiwa kulingana na mafuriko yanayotokea. Kwa hiyo, wakandarasi wako site kwenye madaraja yote ambayo yamekuwa yanakumbwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa pili ni kwamba, maeneo yote ambayo yamechoka na yameainishwa, tutaanza kuyajenga. Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha bajeti, amesema kwamba kwenye vipande vile vikorofi vyote ambavyo vimeharibika sana tutaanza kuvijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hilo haitoshi kwa kuwa ni barabara yote tunaona imechoka. Mpango mkubwa ni kwamba hivi tunavyoongea sasa hivi, Wizara inatoa kipaumbele cha kwanza katika hiyo barabara na tuko kwenye mazungumzo na wenzetu wa World Bank ili kuijenga barabara yote. Huo ni mpango wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa pili, tuna mpango wa kuja na infrastructure bond ambayo tayari tumesham-engage consultant ili kupitia Road Fund kama tutapata ile infrastructure bond, basi kipaumbele pia ni kuijenga hiyo barabara yote. Kwa hiyo, tuna hakika katika hiyo mipango miwili ya kudumu ambayo itatupatia fedha za kuijenga barabara yote. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved