Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha Taasisi na Mashirika yanatoa fursa kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kufanya mazoezi kwa vitendo?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kuhusu swali langu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; wanafunzi wanapokwenda kufanya mafunzo kwa vitendo muda unakuwa mfupi kutokana na kukosekana kwa fedha. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha taasisi zinapata fedha ya kutosha ili muda wa mafunzo kwa vitendo usipungue?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mara nyingi wanafunzi wanapopangwa katika mashirika au taasisi kufanya mafunzo kwa vitendo wanapokuwa kwenye zile taasisi hawapangiwi zile sehemu ambazo ndizo fani zao bali huwepo pale na kupangiwa mambo mengine ambayo hayaendani na fani zao. Je, Serikali inatoa kauli gani katika suala hilo? Ahsante sana.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Nahato, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na jambo la kwanza kuhusu suala la muda, ninaomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba taratibu hizi za kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vyetu vikuu kila fani inapangiwa muda wake maalum. Kuna maeneo ambayo wanakwenda mwezi mmoja, kuna maeneo ambayo wanakwenda kwa miezi miwili na wengine wanakwenda kwa miezi mitatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la muda kuwa mfupi tunaomba tulichukue twende tukalifanyie tathmini ya kina jambo hili ili kuweza kuangalia kwenye mitaala yetu ile, muda ule uliotolewa kwa mujibu wa mitaala kama unatosheleza au la, lakini kimsingi kila fani imepangiwa muda wake na tutakwenda kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kuhusiana na maeneo ambayo wanafunzi wanakwenda na labda wanapangiwa maeneo mengine tofauti, ninaomba tulichukue nalo jambo hili twende tukalifanyie kazi. Ninachofahamu ni kwamba wanafunzi hawa wanapokwenda maeneo haya ya mafunzo kwa vitendo mara nyingi kunakuwa na supervisors ambao wanakwenda kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji vilevile kwenda kufanya upimaji wa kile ambacho wamekwenda kujifunza katika eneo hilo. Tunashirikiana sasa na hawa supervisors na Wakuu wa Taasisi ili kuhakikisha wanafunzi hawa wanapokwenda wanakwenda kwenye yale maeneo ambayo tunayahitaji kwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hiyo nadhani Mheshimiwa Dkt. Nahato unafahamu Serikali yetu ya Awamu ya Sita tumefanya maboresho ya mitaala vilevile tumefanya maboresho ya sera yetu ambayo kwa sasa tunakwenda kuanzisha ule mkondo wa amali, kuanzia katika elimu ya kidato cha kwanza mpaka vyuo vikuu tunaamini kabisa katika elimu hii ya amali itakwenda kuhakikisha kwamba vijana wetu wanakwenda kuwa hands-on katika muda wote kuanzia darasani mpaka kule maeneo ya viwanda wanapokwenda. Ninakushukuru sana.