Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Agnes Elias Hokororo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:- Je, lini ahadi ya ujenzi wa Reli ya Kusini itaanza kutekelezwa?
Supplementary Question 1
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili. Swali la kwanza; je, Serikali inatambua hasa umuhimu na uwezo wa reli ya Kusini katika uchumi wa nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, katika majibu ya msingi amesema itajengwa kwa utaratibu wa PPP, utaratibu huu unapohusisha uwekezaji wa ujenzi wa reli na uendeshaji ninaamini itachukua muda mrefu. Hapa ninaomba nitoe ushauri, ninaishauri Serikali yangu sikivu ifikirie upya badala ya kusubiri ubia ione namna ambavyo itajenga reli ya kusini yenyewe, halafu mwekezaji aje kufanya uendeshaji. Ahsante.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge umepokelewa kwa sababu ni jukumu la Bunge kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza ni kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa reli ya Kusini, hii inatokana na ukweli kwamba upande wa Kusini kwa maana kutoka Mbamba Bay mpaka Mtwara na matawi yake kuna fursa kubwa ikiwemo uwepo wa makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 426, kuwepo kwa ikiwemo vanadium, titanium, lithium pamoja na kwenye eneo la Dangote zaidi ya tani milioni 232 za simenti. Pia umuhimu wa reli hiyo ndiyo unakwenda kuongeza matumizi makubwa ya Bandari yetu ya Mtwara ambayo Serikali imeweka pesa za kutosha pamoja na Mbamba Bay.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba tukifanikiwa kuanzisha reli hiyo itaweza kusaidia madini ambayo nimeyataja na hivyo Serikali kupunguza kuagiza madini kutoka nje na chuma kutoka nje. Pamoja na umuhimu huo napenda nimhakikishie Mheshimiwa muuliza swali Mheshimiwa Hokororo kwamba Serikali imeshafanya mambo mengi sana ili kutambua na kuthamini umuhimu wa reli hiyo. Kwanza tumeshaanza maboresho mbalimbali ya bandari tatu, moja hivi ninavyozungumza ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay umekwishaanza na zaidi ya bilioni 80 Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezielekeza pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumefanya maboresho makubwa Bandari ya Mtwara kwa kuweka zaidi ya bilioni 157. Tatu, kwa sababu tunajua sehemu kubwa ya malighafi zitakazotoka pande wa Liganga na Mchuchuma itakuwa ni pamoja na bidhaa chafu au makaa ya mawe tunajenga bandari mpya ya Kisiwamgao ambapo zaidi ya bilioni 835 zimeelekezwa kwenye bandari mpya kabisa hii yote inadhihirisha na kuthibitisha namna ambavyo Serikali hii ya awamu ya sita inatambua umuhimu wa bandari hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwishalipa fidia pia kwa zaidi ya wananchi 1000 waliopo kwenye eneo la Liganga na Mchuchuma ili kupisha maeneo yale yote hiyo inaonyesha ni kwa namna gani Serikali inatambua jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaanza kufanya jambo la kwanza tunakuja la pili. Tumeshaanza kujenga reli ya kati kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza mpaka Kigoma na mpaka nje ya nchi ambayo inagharimu zaidi ya dola bilioni 12, zaidi ya takribani trilioni 30 hii inamaanisha nini? Inamaanisha utayari wa Serikali sasa ya Awamu ya Sita kuamua kuwekeza kwenye upande wa reli especially SGR.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoanza maboresho makubwa kwenye reli yetu ya Kusini kwa maana ya TAZARA yote hiyo inaonyesha kwamba nchi yetu imeamua kufanya uchumi wake kuwa uchumi na uchukuzi, kwa hiyo nimtoe mashaka nimuombe aendelee kuwa na subira wakati Serikali inakamilisha mambo ambayo imeshaanza kuyafanya na siyo muda mrefu neema ipo mlangoni, watu wa kusini wajiandae Serikali itaanza kujenga reli hiyo. (Makofi)
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:- Je, lini ahadi ya ujenzi wa Reli ya Kusini itaanza kutekelezwa?
Supplementary Question 2
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, Nyanda za Juu Kusini ni wakulima wakubwa wa zao la parachichi na horticulture kwa ujumla. Je, ni lini Serikali itaweka mfumo wa cold-room katika baadhi ya mabehewa katika Reli ya TAZARA ili kuhakikisha kwamba wakulima wakubwa wa mazao hayo wanasafirisha mazao hayo kufika Dar es Salaam kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi yakiwa na ubora? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama lilivyoulizwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Zambia pamoja na China ilijenga Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilomita 860. Kwa sasa reli hiyo iliyojengwa ilikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni tano, lakini kutokana na sababu mbalimbali hatukuweza kufikia hata 30% ya lengo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaanza maboresho mbalimbali kwa ajili ya kuboresha reli yetu hiyo ya TAZARA, hivyo ninachukua ushauri wake Mheshimiwa Mbunge tuone namna ya kutazama, siyo tu kuweka cold room kwa ajili ya mazao ya parachichi ambayo yapo Mkoa wa Njombe, lakini kuangalia chain nzima katika njia nzima kuanzia inapotokea Kapiri Mposhi mpaka Dar es Salaam ili iweze kuwa sehemu ya kuchechemua uchumi wa maeneo ambapo reli hiyo inapita.
Name
Vedastus Mathayo Manyinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Primary Question
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:- Je, lini ahadi ya ujenzi wa Reli ya Kusini itaanza kutekelezwa?
Supplementary Question 3
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Mwanzoni kulikuwa na mpango wa kujenga reli kutoka Tanga – Arusha kuelekea Musoma na sasa, badala yake mpango huo umebadilika kwamba, reli inapita Simiyu. Je, ni lini sasa mchakato huo wa ujenzi wa reli hiyo ya kwenda Musoma utaanza?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumjibu Mheshimiwa Manyinyi, swali lake alilouliza; Mpango wa Serikali ni kuunganisha Bandari yetu ya Tanga na Mikoa ya Kaskazini kwenda mpaka Ziwa Tanganyika. Mpango huo upo, hatujali sana imepita wapi, lakini tunaangalia kiuchumi ni wapi ipite na kadhalika. Kwa mfano, katika njia hiyo kuna madini mbalimbali, ikiwa ni pamoja na magadi soda, Engaruka kuna madini kule Dutwa, nickel na kadhalika. Kwa hiyo, njia specific pengine naweza nisizungumzie hapa, lakini kwa maana ya mpango huo ambao Serikali inao itakwenda kujenga baada ya hatua za awali kukamilika, ikiwa ni pamoja na usanifu wa kina.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved