Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jafari Chege Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 1
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa ujenzi na utekelezaji wa huu Mradi wa Miji 28 kwa maana ya Rorya – Tarime na tuna imani utakapokamilika wananchi wengi wanakwenda kunufaika na mradi huu. Pamoja na kazi nzuri hiyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi zaidi ya Kata tatu kwa maana ya Nyamagaro, Nyamtinga na Kiangasaga ni moja ya kata zinazozunguka chanzo cha maji eneo lilipojengwa chanzo hiki. Wananchi hawa waliridhia wakati chanzo kinajengwa kupisha maeneo yao bila kulipwa fidia yoyote na Serikali, ili iweze kulaza bomba na kujenga chanzo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue, Serikali sasa haioni umuhimu wakati mradi huu ukiendelea, wananchi wa kata hizi waweze kunufaika na maji kabla ya mradi huu haujakamilika kwa 100% ili angalau eneo la chanzo wananchi hawa waanze kunufaika na mradi wa maji safi na salama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; chanzo cha maji cha Mradi wa Kinesi kinahudumia zaidi ya wananchi 20,000. Chanzo hiki kimeanza kutitia kwa sababu ya ongezeko la maji kwenye eneo hili na siyo salama kabisa kwa watoa huduma kwa maana ya maafisa wanapotoa huduma pale inapotokea changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nijue, Serikali haioni kuna umuhimu wa kutoa fedha na kubadilisha ujenzi mwingine wa chanzo hiki ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza, kwa sababu sasa hivi siyo salama na kimekaa muda mrefu na kiukweli kimechakaa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kuna umuhimu sasa wa kujenga chanzo hiki pembeni ili kunusuru madhara yanayoweza kutokea kutokana na changamoto ya chanzo hiki cha maji mradi wa Kinesi? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na pia namshukuru sana Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Rorya, kwa namna ambavyo anaendelea kuwapigania wananchi na kwa namna ambavyo anaendelea kushirikiana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Nyamagaro, Kiangasaga pamoja na Nyamtinga, kwanza kabisa ninawapongeza sana wananchi wa kata hizi kwa kujitolea na kuhakikisha kwamba mradi huo unapita bila fidia yoyote, na ahadi ya Serikali bado ipo pale pale kwamba, mradi huu utawanufaisha wananchi wale ambao wapo kwenye chanzo. Pale ambapo chanzo kinapoanza, basi wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, umekuwa ni utaratibu wetu Wizara ya Maji kuhakikisha kwamba miradi ambayo haihitaji kukamilika kwa 100% kama kuna existing infrastructures ambazo zina uwezo wa kupokea maji ambayo tayari yameshazalishwa, basi haihitaji kusubiri mradi ukamilike kwa 100% ili wananchi wapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Jafari, wananchi wake kabla mradi haujakamilika kwa 100% wataanza kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali la pili, chanzo chetu cha Kinesi kweli kimekuwa na changamoto. Hivyo, nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji kumwelekeza RM Mkoa wa Mara kwenda kwenye chanzo hicho na kukikagua, kujiridhisha changamoto iliyopo kama itahitaji kukihamisha, basi Serikali itafanya hivyo na tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, wananchi hawapotezi hicho chanzo ambacho kimekuwa ni msaada kwao, nakushukuru sana. (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiwekeza katika vyanzo vipya vya maji ili kukidhi mahitaji ya maji kwa wahitaji hasa katika Jiji la Mwanza ikiwemo na Ilemela Manispaa. Wameanzisha chanzo cha maji Butimba, vilevile wamekarabati Capri Point na tayari wanakarabati Igombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo, ongezeko la watu linasababisha maji yasifike kwa watu kama ambavyo ilivyo kutokana na uchakavu wa miundombinu. Je, ni lini sasa Serikali itabadilisha miundombinu chakavu ambapo kunakuwa na upotevu wa maji mengi, na wamejenga matenki kwa ajili ya kupokea maji na kusambaza lakini hayawafikii walengwa kama ambavyo ni kusudio la Serikali? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula, Mbunge wa Ilemela ni zuri, kwa sababu, kwanza kabisa miundombinu ikiwa chakavu hata pale maji yasipofika kwa wananchi, tunapohitaji kuweka booster station katikati ili ya-pump iwekwe, maana yake ile pressure ikishakuwa kubwa na miundombinu ikiwa chakavu maana yake itakuwa ina-burst na matokeo yake maji yanazidi kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, Serikali tumeshaliona hilo na sisi tunachukua hatua kuhakikisha kwamba tunaendelea kurekebisha miundombinu iliyochakaa ili kuhakikisha kwamba tunazuia upotevu wa maji na wananchi wanaendelea kupata zao la maji kama ilivyokusudiwa, ahsante sana. (Makofi)
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 3
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, na pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara kwa kutupatia shilingi bilioni 12 kwa ajili ya Mradi wa Maji Sigino, Babati. Imebaki shilingi milioni 400 kwa ajili ya Kitongoji cha Endasago. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika ukatuahidi kwamba tutapatiwa hizo fedha. Ni lini hizo fedha zitafika?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Gekul kwa sababu nakumbuka tulienda katika miradi hiyo na aliwasemea wananchi wake na anaendelea kuwasemea wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jana aliongea na Mheshimiwa Waziri, lakini sisi tayari tumeshawasilisha madai haya Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba fedha hizi zinapelekwa kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unaendelea vizuri, ahsante. (Makofi)
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 4
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mkoa wa Tabora hususan Jimbo la Tabora Mjini kuwa na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, lakini baadhi ya kata ambazo zina mazingira ya vijiji bado hazipati maji yanayostahili. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na TUWASA, ili kuona namna bora wananchi hawa wanaoishi mjini na kwenye kata za vijijini nao waweze kupata maji kama ambavyo kata nyingine zinapata? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Hawa kwa kuwasemea Wanatabora. Ni jukumu la kila Mbunge kuhakikisha kwamba anawasemea wawakilishwa. Ni kweli kabisa Mradi wa Ziwa Victoria ambao uliigharimu Serikali shilingi bilioni 680 umekuwa ni game changer katika Mkoa wa Tabora na hasa upatikanaji wa maji katika Mji wa Tabora kwa sasa ni 99%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunatambua kwamba 99% ni katika wale waliopo katika mtandao ambao tayari upo. Tunatambua kwamba, kuna maeneo mengine mtandao bado haujafika na Serikali sasa tumeweka mkakati wa kuendelea kupanua wigo ili kila mwananchi afikiwe na mtandao, maji yaweze kumfikia na kuhakikisha kwamba kila mwananchi wa Tabora awe kijijini au mjini anafikiwa na huduma ya maji safi na salama, ahsante.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 5
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninashukuru kwa ukamilishaji wa mradi wa maji kwenye Kata ya Manyamanyama, na Mheshimiwa Waziri alikuja kuzindua, lakini kuna mradi ambao umeanzishwa Kata ya Mcharo kwa ajili ya usambazaji wa mabomba ya maji na hasa ukizingatia kuna Chuo cha Kisangwa ambapo wanafunzi wanasoma, hakuna maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ni lini mtakamilisha mradi huu, ili wananchi wa Nyamatoke, Changuge, Mcharo, Kisangwa na maeneo mengine kwenye kata hiyo waweze kupata maji safi na salama? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na pia namshukuru sana Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuendelea kuwapigania Wanabunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi huu tayari tumeshaanza kusambaza mabomba, pia tupo ndani ya muda wa mkataba. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira, pale ambapo tutafikia kulingana na mkataba ninaamini kabisa mradi utakuwa umekamilika, ahsante sana.
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 6
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji uliopo Kihesa, Mgagao, Masege na Masalali katika Jimbo la Kilolo, atalipwa, kwa sababu wananchi wameusubiri kwa muda mrefu sana, ili waweze kupata maji safi na salama? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Iringa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Mgagao, Masalali uliopo Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa ni mradi ambao unagharimu shilingi bilioni 1.3 na tayari umefikia 85% ya utekelezaji wake. Sasa Serikali imebakiza kipengele cha pump peke yake na inatafuta fedha ili kumlipa Mkandarasi aweke pump na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante. (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 7
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Rorya, Tarime unatakiwa kuhudumia majimbo matatu. Nilishiriki kwenye kutia sahihi, mradi ukasimama tukashiriki kupiga kelele fedha imeenda. Juzi Mheshimiwa Balozi Dkt. Nchimbi amefanya ziara pale Mogabiri kwenye tenki la maji, nikasikitika kuona kwamba hakuna matoleo ya maji kwenda Makao Makuu ya Halmashauri yangu ya Nyamwaga ambayo inaweza ikahudumia Kata ya Binagi, Nyarero, Nyamwaga, Kibasuka, Kanyange, Nyakonga na Muriba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri aniambie tulichoongea alikaa akabadilisha, akatoa maelekezo kule Musoma Mara, au yale makubaliano yanaendelea kule ili mimi nisiende kukaangwa? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Waitara Mbunge wa Tarime kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi unapokuwa unajengwa unakuwa umesanifiwa na design yake ndiyo inaonesha scope ya kazi na maeneo ambayo yatapata maji, lakini kama kuna changamoto hiyo, kama Serikali ninaomba niipokee na nielekeze wataalamu wetu waende waangalie ili watupatie majibu ya uhakika kama tumeenda kinyume na usanifu ulivyofanyika, basi tutachukua hatua kama Serikali ili kuhakikisha watu wa Mheshimiwa Waitara wanapata huduma ya maji safi na salama baada ya mradi huo kukamilika. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Hussein Nassor Amar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 8
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa tuliomba fedha kwenye bajeti hii ya 2025, shilingi bilioni 4.3 kwa ajili ya kukamilisha usambazaji wa maji kwenye Kata ya Kaboha, Shabaka, Mwingiro, Nyabulanda, Nyugwa, Bukwimba, Busolwa na Nyang’hwale, je, Serikali itatoa fedha hiyo ili tuweze kukamilisha mradi huo? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge na amekuwa akifanya ziara kwenye kata yake, na nilibahatika kufanya ziara katika Jimbo lake, tulienda katika baadhi ya kata. Nimhakikishie kwamba ahadi ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Watanzania wanasambaziwa huduma ya maji safi na salama wakiwemo wananchi wa Nyang’hwale. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatoa fedha, ahsante sana. (Makofi)
Name
Boniphace Nyangindu Butondo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 9
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mradi wa Igaga – Mwamashele – Lagana umekamilika sasa kwa zaidi ya mwaka mmoja na ulianza kufanya kazi, lakini ghafla miezi mitatu pamepatikana breakdown ya kawaida tu, wananchi hawapati huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutoa maelekezo, ili utatuzi wa marekebisho na matengenezo ya mabomba maeneo yaliyoharibika yafanyike haraka na huduma hiyo ianze kutolewa kwa wananchi hao? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninamshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Butondo Mbunge wa Kishapu. Ni kweli kabisa Mheshimiwa Butondo kwanza kabla ya kuuliza swali hili, tayari ameshatuwasilishia Wizarani jambo hili na tayari tumeshaanza kuchukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yangu ni kwamba, kuwepo na uharakishwaji wa ukamilishaji wa hiyo breakdown iliyokuwa imetokea ili wananchi wa Mheshimiwa Butondo waendelee kupata huduma nzuri ya maji safi na salama, ahsante.
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 10
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 upotevu wa maji umefikia 36.8% sawa na hasara ya shilingi bilioni 114. Nini mkakati wa Serikali kudhibiti huu upotevu wa maji ili tusiingie hasara? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, upotevu wa maji unaokubalika ni kati ya 15% - 20%. Mheshimiwa Paresso ameonesha namna ambavyo Serikali inaweza ikapoteza fedha. Ni kweli kabisa, kwanza mkakati wa Serikali ni kuanzia pale kwenye usanifu wenyewe. Tunapofanya ule usanifu, tunahakikisha kwamba hakuna kitakachopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, miundombinu ambayo imekuwa na uchakavu. Tunahakikisha kwamba na yenyewe inaendelea kuboreshwa. Cha tatu, ni utoaji wa huduma yenyewe. Pale ambapo utoaji wa huduma unaweza ukawa na watu ambao hawaelewi namna ya utoaji wa huduma na penyewe tunaendelea kudhibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kuu ni kwamba mnyororo mzima wa utoaji wa huduma ya majisafi na salama usiwe na chembechembe za upotevu wa maji ambao unatokana na uzembe ambao tuna uwezo wa kuuzuia, ahsante sana.
Name
Godwin Emmanuel Kunambi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 11
MHE. GODWIN KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake njema ya kumtua mwanamke ndoo kichwani wa Tarafa ya Mlimba kwa kupeleka fedha bilioni 7.4. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, swali langu, mradi ule kwa mujibu wa mkataba ulipaswa ukamilike ndani ya miezi 12, sasa yapata miaka miwili. Wale wananchi wa Tarafa ya Mlimba wangependa kujua ni lini mradi huu utakamilika? Ahsante. (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na pia namshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Mlimba, kaka yangu Mheshimiwa Kunambi. Ni kweli kabisa mradi huo ulitakiwa kukamilika ndani ya mkataba ambayo ni miezi 12, lakini kulikuwa na changamoto zilijitokeza hapa, na bahati nzuri tumezi-accommodate tayari, na tunaamini kabisa kwamba, mkandarasi sasa atarudi site kwa ajili ya kwenda kuukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tukifahamu kabisa kwamba changamoto ilikuwa ni malipo ambayo mkandarasi tuliyekuwa tumefikia katika sehemu ya kujadiliana namna bora ya kumlipa, sasa tayari tumeshawasilisha kwa ajili ya malipo. Nitarajie kwamba huo mradi utakamilika kabla tunapoenda kwenye Uchaguzi Oktoba, 2025 ahsante sana.
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji Miji 28 Rorya - Tarime utakamilika?
Supplementary Question 12
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kufahamu, ni nini mkakati wa Wizara? Kwa sababu hapa karibuni kama utakumbuka, Serikali ilitoa visima zaidi ya vitano kwenye kila Jimbo, lakini bado Majimbo mengi visima hivyo havijafungiwa pump baada ya kuvichimba na wananchi wanakosa huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nataka kufahamu, ni lini pump kwenye Kijiji cha Masiku na maeneo mengine kwenye Jimbo la Ndanda zitafungwa ili wananchi waweze kupata huduma ya maji baada ya kuchimbiwa visima kwa muda mrefu?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Cecil Mwambe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba, Serikali kupitia Programu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya visima 900 ambapo ni visima vitano kwa kila Mbunge wa Jimbo tayari vimeshachimbwa vya kutosha. Kuna baadhi ambavyo vilikosa maji, lakini vile ambavyo vimeshapata maji, mtandao wake (point source) kituo rahisi cha kuchotea maji vimeshakamilika. Tulikuwa tumetoa kandarasi kwa baadhi ya wazabuni ili waweze ku-supply hizo pump.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwamba wameshaanza ku-supply kwenye maeneo mengine na tayari wameshaanza kufunga. Tunaamini kabisa kwamba na Jimbo la Mheshimiwa Cecil na vijiji vyake vitafikiwa kabla ya mwaka huu wa fedha kuwa umeisha, ahsante sana.