Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abeid Ighondo Ramadhani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 1
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ambaye pia, alifika katika Kijiji cha Mrama kuzindua kile kisima, pia, ninaomba nitoe masahihisho kidogo; kwanza Wananchi wa Gairu hawapati huduma katika Mradi wa Sagara kwa sababu, uko mbali na pia, kule ni Bonde la Ufa, Gairu wako Bonde la Ufa na Sagara iko juu kwa hiyo, ni tabu kwao kupanda mlima kwenda kupata maji pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo hayo, sasa ninaomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; badala ya kuchukua maji kwenye source au kisima, ule Mradi wa Sagara, kwa nini tusichukue maji kutoka chanzo cha mradi mkubwa wa Kinyamwenda, ambao unatoa maji lita elfu ishirini kwa saa na unaweza kusambaza hata vijiji vitano, ili tupeleke na Kitongoji cha Misuna, ambacho kiko karibu na Kitongoji cha Gairu, ambacho kinapata maji yasiyo salama kwa matumizi ya binadamu na pia, hapohapo tungeweza kuchukua maji ya Sagara tukayapeleka Mangida?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kitongoji cha Muungano kilichoko Kijiji cha Pambaa hawana maji; kitongoji hicho kina Miradi ya Migodi ya Madini ya Dhahabu, lakini wananchi wanapata taabu, hawana maji. Je, Serikali ina mpango gani kuwapatia wananchi hawa kisima kizuri cha maji ambacho kinaweza kikaondoa tabu hii, lakini pia, kusambaza maji kwenye maeneo ya migodi ya madini? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Ighondo kwa kazi nzuri sana ambayo anaendelea kuifanya kwa wananchi wake. Pia, namshukuru sana kwa namna ambavyo ameshirikiana na Serikali kwenye kusimamia upanuzi na uboreshaji wa Mradi huu wa Sagara, lakini pia, kwa kutoa taarifa, kama ambavyo sasa amesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mradi huu wa Sagara kwenda Gairu kuna umbali na lengo la Serikali ni kwamba, mradi unapokamilika basi maji yawe yanapatikana kwa gharama nafuu. Tunapoyatoa maeneo ya mbali, maana yake ni kwamba, yanapofikishwa kwa watumiaji gharama yake ya kuyalipia inakuwa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge nikitambua kwamba, kuna mradi wetu wa shilingi milioni 950 maeneo ya Kinyamwenda. Nitatumia fursa hii kuwaelekeza RM upande wa Singida, wakafanye utafiti na kujiridhisha ni namna gani maji haya tunaweza tukayafikisha Gairu, lakini pia, tunaweza tukayapeleka Misuna, katika vijiji na vitongoji vingine ambavyo vimezunguka katika eneo hilo. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kadri anavyoendelea kuwapigania wananchi wake na sisi Serikali tuko pamoja naye kuhakikisha kwamba, tunafikisha huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipengele cha pili, pia, ni kweli kabisa lengo la Serikali ni wananchi kupata huduma ya maji safi na salama. Sisi tumejipanga na kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, tunalipokea, tutaenda kufanya utafiti pale tujiridhishe ukubwa wa tatizo, kama ni kuchimba kisima tutachimba kisima na kama ni kupanua skimu nyingine ifikishe maji tufanya hivyo, lengo ni kwamba, wananchi wapate huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
Name
Jafari Chege Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 2
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na Serikali kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maji, lakini bado changamoto ya maji kwenye maeneo mengi, hasa maeneo ya vijijini, imeendelea kuwa kubwa. Ninataka nijue, kwa nini sasa Serikali msifanye tathmini ya kujiridhisha maeneo yote, hasa maeneo ya vijijini, ambayo yana changamoto ya maji, waje na mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba, angalau kwenye bajeti ya mwaka 2025/2026 maeneo haya yote, ambayo wananchi wanaathirika waweze kupata mradi wa maji?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Chege, lakini pia, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025 imeelekeza uhitaji wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama kwa kiwango cha 85%, sasa tumeshafikia 80.1% na vilevile kwa mjini kuwafikishia kwa kiwango cha 95% na sasa tumeshafikia kiwango cha 91.6%. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba, Serikali imefanya kazi kubwa sana, lakini bado inatambua kuna maeneo ambayo bado hatujayafikia na tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba, tunafika katika lengo ambalo tumejiwekea. Ahsante.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Wariku kuna mradi wa shilingi bilioni 1.6 utakaowanufaisha wakazi 3,000, lakini mpaka sasa hivi haijatoka hata shilingi. Ni lini sasa mtatoa pesa ili Wakazi wa Wariku, Kangetutya, Kamkenga, Majago na Rwabu waweze kupata maji safi na salama?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru dada yangu, Mheshimiwa Ester Bulaya na ninafahamu anavyoendelea kupambana kwa ajili ya wananchi hao. Sisi Wizara ya Maji consumption capacity yetu ni kubwa na tunaweza kutumia bajeti yetu vizuri sana, lakini pia, madai kama haya sisi tunaendelea kufanya majadiliano mazuri kabisa na wenzetu wa Wizara ya Fedha na tumefikia hatua nzuri. Tunaamini kwamba, muda umefika sasa, tutawalipa hawa wakandarasi, ili miradi hii iweze kukamilika na watu waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
Name
Aysharose Ndogholi Mattembe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 4
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwa kuwa, Vijiji vya Winamila, Tumbi, Dadia, Itetemo na Kitalaro katika Jimbo la Manyoni Mashariki havina kabisa mtandao wa maji. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka maji katika vijiji hivyo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana dada yangu kwa kuendelea kutukumbusha. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, upande wa Manyoni ameweka mradi wa shilingi bilioni 26, Mradi wa Miji 28 na sasa umefikia 40%, lakini pia, tuna programu ya visima 900 ambao unaendelea katika kila jimbo visima vitanovitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kabisa kwamba, miradi hii itakapokamilika kuna visima vina uwezo wa kutengenezewa extension na kufikisha katika maeneo mengine ambayo hayana maji. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, miradi hii itakapokamilka tutaangalia sehemu ambayo tutakuwa hatujafika, ili tuweze kuona namna gani tutawafikishia wananchi wa maeneo hayo. Ahsante sana.
Name
Zaytun Seif Swai
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 5
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Wilaya za Meru na Arumeru wana changamoto kubwa ya floride kwenye maji, ambayo inawasababishia madhara makubwa ya kupinda viungo na akinamama wajawazito kushindwa kujifungua. Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha maji haya yanasafishwa kabla ya matumizi? (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Wilaya za Meru na Arumeru wana changomoto kubwa ya floride kwenye maji, ambayo inawasababishia kupinda kwa viungo na changamoto kubwa kwa akinamama wakati wa kujifungua. Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha maji haya yanasafishwa kabla ya matumizi? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vyetu vya maji ambavyo vimekuwa na changamoto za floride na chloride, kuna vyanzo ambavyo tunaweza kutibu kwa kutumia kemikali tulizonazo ambazo zimepitishwa, lakini kuna maeneo mengine ile concentration inakuwa ni kubwa sana kiasi kwamba, gharama ya kuyatibu inakuwa ni kubwa sana. Tunachokifanya ni kubuni miradi mingine mbadala, ambayo inaweza ikatusaidia kufikisha maji katika maeneo ambayo wananchi hao wanaishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba, tunaondokana na gharama kubwa ya kutibu maji, ambayo, eventually, gharama hizo zinakwenda kumwangukia mwananchi. Lengo ni kwamba, wapate maji na yawe na gharama nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ni kwamba, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, suala la Meru na Arumeru tayari tumeshalipokea katika ofisi yetu ya Wizara ya Maji na tunalifanyia kazi tukiwa tunaendelea kubuni miradi mbadala ya kuwafikishia huduma ya maji safi na salama. Ahsante.
Name
Noah Lemburis Saputi Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 6
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali. Je, ni lini Serikali itatoa fedha, kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Oldonyosambu, Tarakwa, Siwandeti, Tiranyi na Kimnya?
Name
Kiteto Zawadi Koshuma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja; tayari tumeshapokea madai hayo na tumeshawasilisha kwa mchakato wa kulipa. Ahsante sana.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 7
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vitano vilielekezwa kwenda Nyabisaga, Kiyongera, Kitenga, Nyakalima na Kubhiterere na wananchi wakawa na matumaini makubwa sana. Ninaomba nijue, ni lini sasa vijiji hivi, ile miradi itakamilika watu wapate maji, kama ambavyo tuliahidi na wakapokea kwa shangwe kubwa sana? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jana na juzi tuliongea na Mheshimiwa Waitara, kuhusiana na maeneo haya. Nimtoe hofu, Serikali imeshalipokea na inalifanyia kazi. Tutahakikisha kwamba, mkandarasi analipwa, ili vijiji hivyo viweze kukamilika na kuhakikisha kwamba, wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali tuwe na availability accessibility na affordability; vipengele vitatu lazima tunavizingatia kuhakikisha kwamba gharama ya mradi unapokamilika basi ikaendane na uwezo wa wananchi kumudu huduma hiyo ya maji ambayo itakuwa inatolewa. Ahsante sana.
Name
Yustina Arcadius Rahhi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 8
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Je, ni lini Serikali itakamilisha zoezi la kusambaza maji kutoka mradi mkubwa wa Laizeri katika Wilaya ya Kiteto, mabomba yako pale na vifaa, uende Vijiji vya Dongo na Ndotoi?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibi swali la nyongeza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza. Ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, tumekuwa tukishirikiana vizuri sana na ameendelea kuwapambania sana akinamama, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na kwa ushauri wake ambao umeendelea kutupatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utakamilika ndani ya muda wa mkataba, ambapo bado mkataba huo uko active na hatujapata changamoto yoyote. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na sisi ili uweze kukamilika bila kuwa na changamoto yoyote. Ahsante sana.
Name
Shamsia Aziz Mtamba
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Mtwara Vijijini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 9
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Likwidi imekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu sana tangu tumepata uhuru. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inawatua ndoo kichwani akinamama wa Kata hii ya Likwidi?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana dada yangu kwa kazi nzuri sana ambayo anaendelea kuifanya. Nilikuwepo Mtwara, tulikuwa naye; lakini pia ni dhamira ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kumtua mama ndoo kichwani na pia ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vile visima vitano vitano tunatambua kwamba hiyo kata haikuweza kufanikiwa kupata kisima. Ninaomba nimtoe hofu, katika bajeti hii tunakwenda kuweka bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaenda kupata maji safi na salama katika kata hiyo. Ahsante sana
Name
Vita Rashid Kawawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu, Kijiji cha Sagara ambacho wanatumia maji yenye chumvi?
Supplementary Question 10
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba nianze kuishukuru Serikali kwa kuniletea mabomba ya nchi nane kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Mgombasi na pia kutatua tatizo la Mradi wa Mchomola ambao sasa kazi inaendelea. Swali langu; tuna Mradi wa Limamu na Mradi wa Luchiri pale Msufini, je, ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huo ambao ipo katika bajeti hii ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakumbuka wiki tatu zilizopita aliuliza swali kuhusu haya mabomba na akaomba kuhusu fedha. Serikali iko kazini na ndiyo maana tayari leo ameongea kwa furaha sana kuonyesha kwamba Serikali imetenda kulingana na jinsi ambavyo alikuwa ameomba. Nimtoe hofu na hili ambalo amelisema, kwa sababu bajeti yetu ya fedha ya mwaka wa fedha 2025/2025 haijapita, nimtoe hofu kwamba tunakwenda kulifanyia kazi ili mradi huo nao uweze kupata fedha kama ambavyo leo amekiri kabisa kwamba tayari mradi kwanza alioombea pesa Serikali ya Dkt. Samia Saluhu Hassan imekwishapeleka. Ahsante sana.