Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Condester Michael Sichalwe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: - Je, kwa nini Serikali iliamua kujenga bandari Karema wakati upande wa DRC bado hawajajenga?
Supplementary Question 1
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza naomba nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa ujenzi mkubwa sana wa bandari wa zaidi ya shilingi bilioni 49, na kwa zaidi ya miaka miwili, sasa umekamilika pamoja na kwamba haujaanza kufanya kazi. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mosi, pamoja na mikakati hii mizuri ambayo Serikali inayo, na bandari hizi zitakapokamilika kwa upande wa DRC lakini itakuwa ni bandari tu zimekamilika, ipo haja ya kupatikana barabara kutoka Bandari ya Moba mpaka kufika Lubumbashi ambako Watanzania wengi ndiko soko wanakolitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi, alipofanya kikao na Country Manager wa TPA pale Lubumbashi na Ubalozi wetu mdogo, walimthibitishia umuhimu wa hii barabara. Je, ni upi mkakati wa kuanza ujenzi wa barabara kutoka Moba mpaka Lubumbashi ili kuiunganisha nchi yetu ya Tanzania moja kwa moja na DRC bila kupitia nchi ya Zambia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa tunatambua jitihada hizi ambazo zinafanywa na Serikali zinaweza zikachukua muda mrefu kwa sababu ni uwekezaji mkubwa, na bado mpaka sasa hivi wafanyabiashara kulifikia Soko la Lubumbashi ambao ni miongoni mwa miji mikubwa ambayo inawapatia Watanzania wengi pesa, bado wanapitia changamoto kubwa na kadhia kubwa wanapopitia nchi ya Zambia kutokana na vita ya uchumi iliyopo kwa sababu kila mtu analiangalia Soko la DRC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni ipi hatua madhubiti ya Wizara hii ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Wizara nyingine kukaa chini kuendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara wanaoliendea Soko la Lubumbashi ambazo wanapitia kwenye nchi ya Zambia? Ni upi mkakati wa haraka na dharura ili Watanzania wasiendelee kuumia? Ahsante (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Uchukuzi, natumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Sichalwe kwa jinsi anavyofuatilia. Mheshimiwa Sichalwe ni moja ya wadau muhimu wanaofuatilia sana namna ambavyo Serikali inaweza ku-access Soko la Kongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba nchi yetu imebarikiwa kuzungukwa na nchi nyingi zisizo na bandari, na upande wa Zambia tuna zaidi ya mzigo wa tani milioni saba, na upande wa Kongo zaidi ya mzigo wa tani milioni 10 na nchi nyinginezo. Hata hivyo, bado hatujafikia inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpa pongezi hizo, naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza ambayo ameyauliza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ameuliza habari ya suala la barabara kutoka Moba kwenda Lubumbashi. Huu ni ushauri anaoutoa mara kwa mara, nasi Serikalini tumeshaupokea na tumeshaanza kuandaa taarifa ya wataalamu ili kutazama fursa zilizopo na mchakato mzima wa namna ya kufikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendelea na hilo, ukizingatia swali lake la msingi aliuliza ni kwa nini Serikali ilianza kujenga Karema wakati upande wa pili hatujaanza pengine kupatumia, Serikali kwa kushirikiana na wenzetu wa Kongo tayari tumeshaanza kufanya utilization ya bandari hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza, ukienda pale Kongo upande wa Katanga eneo la Manono, tuna madini mengi ya lithium na copper ambapo ujenzi wa barabara kilometa 450 kutoka kule Manono – Katanga – Kalemie umeshaanza sambamba na usanifu wa awali ili hapo baadaye tuweze kujenga SGR.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa miaka mingi sana Bandari ya Kalemie ilikuwa haitumiki na imekuwa ni kilio cha Wabunge wengi sana wanaotumia Ziwa Tanganyika. Tayari ujenzi huo umeanza kama nilivyozungumza na wenzetu wa Kongo kwa kutumia mwekezaji wanajenga Bandari ya New Kalemie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo peke yake haliishii hapo. Ili kuona Serikali imetambua umuhimu wa fursa zilizopo katika Ziwa Tanganyika, inakwenda sambamba na ujenzi wa meli nne ili wawekezaji hao waweze kusafirisha mzigo wa lithium na copper na madini mengine kutoka kule Katanga kuja hapa kwetu, kwenda mpaka Bahari ya Hindi ambapo tunaanza na meli nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tayari wameshaanza kujenga meli ya kwanza tarehe 1/4/2025 na meli nyingine nne zitakuwa zimekamilika ndani ya miaka hii miwili. Tunategemea mzigo zaidi ya metric tons 1,500,000 katika mwaka wa kwanza utaanza kupitishwa. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa kwa kufuatilia jambo hili na nimeona nitoe kwa ufafanuzi mkubwa zaidi ili aweze kupata picha hiyo kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nakubaliana na changamoto zilizopo kwenye upande wa madereva wetu wanapotoka hapa kwenda upande wa Kongo kupitia upande wa Zambia. Changamoto hizo zinaendelea kushughulikiwa kwa kushirikiana na nchi hizi mbili kidiplomasia kwa lengo la kuboresha biashara hiyo ili sisi sote kwa sababu wao ni wanufaika na sisi ni wanufaika na maeneo mengine tuweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wetu mzuri na wa kudumu zaidi ni kutazama namna ya kuweza kufikia nchi specific kupitia Ziwa Tanganyika kama ambavyo nimeeleza kwenye maelezo ya awali, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved