Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Busanda
Primary Question
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:- Sheria ya madini inawataka wachimbaji wakubwa kama vile GGM - Geita, kila miaka mitano wamege sehemu ya maeneo na kuyarudisha kwa wananchi. (a) Je, ni lini Serikali itawarudishia wananchi maeneo ya Sami na Nyamatagata yaliyoombwa na wananchi kupitia vikao vyote hadi Mkoani? (b) Je, ni lini eneo la STAMICO - Nyarugusu litafanywa kuwa la wachimbaji wadogo wadogo kama ambavyo Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alivyokwisha tamka mara mbili?
Supplementary Question 1
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, hata hivyo napenda kusema kwa mfano wananchi wa Nyarugusu ni kipindi kirefu sana ni ahadi Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi wananchi hawa waweze kupewa eneo hili na harakati mbalimbali, viongozi wengi wamekuja katika eneo hilo kuahidi lakini hakuna kilichofanyika kwa hiyo wananchi wote wa Nyarugusu wanahitaji kusikia kwamba ni lini sasa wataweza kupewa eneo hilo la STAMICO?
Swali la pili, wananchi wa Geita wanategemea sana shughuli za uchimbaji ndio maana Wanyamatagata pamoja na Sami na maeneo mengine kama vile Mkaseme maeneo ya Magenge wananchi wanahitaji kupewa maeneo ya uchimbaji, ningependa kujua sasa nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapewa maeneo ya uchimbaji? (Makofi)
Name
Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Answer
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, na ndugu zangu wa Nyarugusu, nadhani unataka tutoe jibu la ukweli kabisa na hili ndiyo litakuwa la ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hilo eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea ni leseni kati ya STAMICO na kampuni ambayo kuna Watanzania na Wacanada, kilichotokea ni kwamba kuna mgogoro mkubwa kweli na Mheshimiwa Naibu Waziri nilivyomuagiza aende kule alivyotoa tamko tu, lile tamko likasambazwa dunia nzima.
Kwa hiyo, naomba wananchi wafahamu kwamba eneo hilo halitatolewa mpaka hiyo kesi iishe. Watanzania tuwe makini sana, tumesaini mikataba na makampuni na mkataba mkubwa ni ule MDA (Mineral Develepment Agreement), tukicheza na hiyo kesi na Wabunge kama wanataka tuandikishiane na Wabunge kwamba Serikali ikishtakiwa Wabunge husika watabeba gharama za hiyo kesi kwenye mahakama za nje ya Tanzania. Kesi bado ipo, wananchi wavute subira mpaka hiyo kesi ikamilike kuhusu huo mgodi wa Nyarugusu na huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo, ahadi zitatolewa, ahadi zisitolewe tena hapa mpaka hiyo kesi iishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo sasa wa Geita na sehemu zingine, ni kwamba tunatoa maeneo kwa wachimbaji wadogo, na hivi juzi nilikuwa naenda kutoa ruzuku ya awamu ya tatu, lakini tumegundua kwamba ruzuku awamu ya pili waliochukua fedha kwa kupitia TIB hawakuchukua fedha walipewa vifaa, vile vifaa vingine havipo huko kwenye migodi.
Kwa hiyo, kabla hatujatoa ruzuku ya awamu ya tatu imesimamishwa mpaka tufanye tathmini ya awamu ya pili na awamu ya kwanza, hapo ndipo tutaenda kutoa ruzuku ya awamu ya tatu. Lakini wachimbaji wadogo Serikali ina dhamira kubwa kwelikweli ya kuwaendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tuheshimu sheria, na ninawaomba Wabunge, tuna Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inatambua utoaji wa leseni na MDAs hizo. Sasa Wabunge wenyewe hatuwezi kushabikia kuvunja sheria ambazo tuliziweka. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved